Posted by newstz.blogspot.com
0
comments»
Showing posts with label UDSM. Show all posts
Showing posts with label UDSM. Show all posts
Fidelis Butahe
WANAFUNZI wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) jana walichafua hali ya hewa katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho baada ya kumzomea Rais Jakaya Kikwete.
Rais Kikwete ambaye alikuwa ameambatana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa pamoja na viongozi wengine wa Serikali alikutwa na zomeazomea hiyo saa 6:23 mchana wakati akiingia katika Ukumbi wa Nkrumah ambapo yalifanyika maadhimisho hayo. Wanafunzi hao mbali na kumzomea Rais huyo wa awamu ya nne pia walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali huku wakiimba, “Kama sio juhudi zako Nyerere mafisadi wangesoma wapi, hatukutaki ondoka,”.
Baadhi ya mabango hayo yalikuwa yameandikwa, ‘’Wao walisoma bure sisi tunalala nje, Miaka 50 ya uhuru mikopo hatupati, Tusiilipe Dowans, Wanafundisha UDSM makazi Bagamoyo je ni haki?, Kama sio juhudi zako Nyerere mafisadi wangesoma wapi.
Awali wanafunzi hao walionekana wakiwa wameshika mabango hayo lakini walizuiwa na polisi na kuelezwa kuwa kama ni ujumbe tayari ulishafika hivyo waendelee na shughuli nyingine.
Hata hivyo, wanafunzi hao ambao hawakutaka kutaja majina yao walizunguka nyuma ya Ukumbi wa Nkrumah na kuyaficha mabango hayo, huku wengine wakijipanga tayari kwa kumpokea Rais Kikwete ambaye alikuwa bado hajafika eneo hilo.
Mara baada ya Rais Kikwete kufika chuoni hapo alikwenda kusaini katika kitabu cha wageni na wakati akielekea katika ukumbi huo huku akipunga mkono, wanafunzi hao walikuwa kimya.
Rais Kikwete wakati akiendelea kuwapungia mkono wanafunzi hao, walianza kumzomea na kutoa mabango yao waliyokuwa wameyaficha huku wakiimba, “Kama sio juhudi zako Nyerere mafisadi wangesoma wapi”.
Polisi waliokuwa eneo hilo wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana walilazimika kutumia busara kuwanyamazisha wanafunzi hao ambao waliendelea kuzomea na kuimba licha ya kuwa Rais Kikwete alikuwa ameshaingia katika ukumbi huo.
Wakati shughuli za maadhimisho hayo zikiwa zinaendelea wanafunzi hao walikuwa bado wakiimba nyimbo hizo na kuzomea, mpaka walipoombwa kutoendelea kuimba na baadhi ya polisi ambao waliwaeleza kuwa kuzomea hakuwezi kuwaletea mikopo vyuoni, bali wajenge hoja za msingi na kuziwasilisha sehemu husika.
Hata wakati Rais Kikwete akisoma hotuba yake na kugusia maendeleo ya chuo hicho pamoja na uboreshwaji wa utoaji mikopo vyuoni, wanafunzi hao waliokuwa wakifuatilia hotuba hiyo kupitia Televisheni kubwa walikuwa wakizomea.
“Hivi Rais anajua jinsi tunavyopigika hapa chuoni, wengine inaonekana tumepewa mikopo, lakini mpaka leo hatujapata, hivi anajua tunaishi vipi huyu, anajua tunalala wapi,” walisikika wakisema baadhi ya wanafunzi.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika alisema kuwa kilichofanywa na wanafunzi hao kinatakiwa kutazamwa kwa macho mawili.
Mnyika alisema kuwa ahadi zilizotolewa na Rais Kikwete kuhusu maendeleo ya chuo hicho zinatakiwa kutekelezwa na kufafanua kuwa hata katika utawala wa Mwalimu Nyerere matatizo vyuoni yalikuwapo na kwamba dawa ni kuyatatua.
Akizungumzia kitendo cha wanafunzi hao kumzomea Rais Kikwete mbele ya Rais Museveni, Mnyika alisema kuwa hilo ni jambo la kawaida kwa kuwa Museveni amewahi kusoma katika chuo hicho na anajua harakati za wanafunzi.
“Wakati Museveni akisoma alikuwa na kikundi chake ambacho kilikuwa na msimamo mkali na kutoa kauli za kimapinduzi kwa viongozi mbalimbali wa Afrika, Museveni anakijua hiki chuo,”
CHANZO: MWANANCHI
Posted by newstz.blogspot.com
0
comments»
Rais Jakaya Kikwete akimkabidhi Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya CRDB Tully Mwambapa picha ya Mwalimu Julius Nyerere iliyonunuliwa na Benki hiyo kwa kiasi cha Sh.milioni 35,wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa na Ofisi ya Rais kwa ajili ya kukusanya pesa za upanuzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam juzi na kupatikana Sh.722 milion.Fidelis Felix
Na Aziza Masoud
RAIS Jakaya Kikwete juzi usiku alionja adha ya kukatika kwa umeme alipokuwa akiendesha hafla ya kuchangia ujenzi wa kituo cha wanafunzi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 5:43 usiku takriban saa nne tangu hafla hiyo ianze.
Rais Kikwete alifika ukumbini hapo saa 2:33 muda mfupi akitanguliwa na viongozi wengine wa Serikali. Baadhi ya viongozi hao ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawambwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki. Kukatika huko kwa umeme, kuliwafanya wageni waliokuwapo ukumbini kuanza kupiga kelele za: “Ngeleja... Dowans... Ngeleja... Dowans... Ngeleja... Dowans.”
Tukio hilo lilidumu kwa dakika mbili kabla uongozi wa Mlimani City kuwasha genereta. Katika hafla hiyo, Rais Kikwete alichangisha Sh720 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kinachotarajiwa kujengwa katika Kampasi ya Mlimani katika kumbukizi ya Miaka 50 ya Uhuru. Kituo hicho kitakuwa na maeneo ya kupumzika wanafunzi, hosteli, sehemu za michezo, maktaba, huduma za vyakula, benki, ofisi za serikali ya wanafunzi na kituo cha intaneti.
Akizungumza kabla ya uchangishaji huo, Rais Kikwete alisema lengo la kuchangisha fedha hizo za kujenga kituo cha wanafunzi ni kuboresha mahitaji ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambayo kwa sasa yamekuwa changamoto kubwa inayosababisha wanafunzi kupata elimu katika mazingira magumu.
“Mara nyingi ukipita katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, unakuta wanafunzi wamezagaa katika maeneo mbalimbali na wengine chini ya miti. Hii yote inatokana na kukosa eneo maalumu la kujisomea na kupumzika mara wanapomaliza au kusubiri kuingia katika vipindi,” alisema Kikwete.
Alisema kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kimaendeleo, chuo hicho kwa sasa kinakadiriwa kuchukua wanafunzi 20,000 kwa mwaka, tofauti na miaka ya nyuma kilipokuwa kinachukua wanafunzi 14,000. Alisema kutokana na hali hiyo, wahitimu wanapaswa kuchangia maendeleo ya chuo hicho kwa kuwapatia wanafunzi nafasi za malazi ambazo kwa sasa hazitoshi na kuwalazimu wengine kulala nje ya eneo la chuo.
Awali, Dk Kawambwa alisema kukutana kwa wanafunzi na wahitimu wa chuo hicho ni kuendeleza utamaduni unaotumika duniani kote wa kuchangia maendeleo ya shule au vyuo wanavyotoka. “Jambo tunalolifanya jioni hii lina maana kubwa, tunajenga utamaduni wenye manufaa katika nchi yetu kuendeleza elimu nchini kwa kuchangia maendeleo ya shule au chuo,” alisema.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema kituo hicho kitagharamu Sh17bilioni na hatua ya kwanza ya kupata fedha za ujenzi huo ni kuandaa kampeni hizo za uhamasishaji na uchangiaji kutoka kwa wadau mbalimbali. “Hafla ya uzinduzi wa michango hiyo ilifanyika Januari 27 mwaka jana.
Iliwahusisha wanajumuiya ya chuo na wajumbe wa baraza la chuo na tulibahatika kupata Sh1.2bilioni, nyingi zikiwa ni ahadi za wafanyakazi,” alisema Profesa Mukandala. Alisema baada ya hafla hiyo, kulifanyika hafla nyingine Ikulu mwezi huohuo iliyokuwa ikiongozwa na Rais Jakaya Kikwete. Katika hafla hiyo jumla ya Sh1.5bilioni zilikusanywa.
Alisema hafla ya tatu ilikusanya Sh658 milioni za ambazo zilitolewa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye naye ni muhitimu wa chuo hicho. Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba aliwataka wahitimu waliosoma chuoni hapo kuwa mstari wa mbele kuchangia maendeleo yake.
Katika hafla hiyo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) iliahidi kutoa Sh150 milioni, Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro Sh130 milioni, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Sh100 milioni, Mikumi Interprises Sh20 milioni, Benki ya NMB Sh20 milioni. Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) ilitoa Sh30 milioni, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Sh30 milioni, Mfuko wa Pensheni wa PSPF Sh20 milioni na Mnyika alitoa Sh2milioni na kuahidi kutoa Sh milioni moja kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.
Benki ya CRDB ilinunua katika mnada wa kuchangisha fedha za ujenzi huo, picha ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa Sh35milioni. Rais ndiye aliyeendesha mnada wa picha hiyo.
Posted by newstz.blogspot.com
0
comments»
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza mweyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Hifadhi za Mbuga za Wanyama Tanzania TANAPA Bwana Modestus Lilungulu baada ya kukabidhi hundi ya thamani ya tsh.150m/- Milioni mia moja na hamsini ikiwa ni mchango wa Shirika hilo kwa ajili ya kujenga kituo cha wanafunzi katika chuo kikuu cha Dar es Salaam jana katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.Katika hafla hiyo iliyoandaliwa na Rais Kikwete kwaajili ya kuchangia ujenzi wa kituo hicho zaidi ya Shilingi Milioni Mia saba zilipatikana ikiwa ni michango kutoka kwa watu binafsi,mashirika binafsi na ya umma.kulia nia makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Seif Shariff Hamad(picha na Freddy Maro)
Posted by newstz.blogspot.com
0
comments»
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Balozi Fulgence Kazaura akimtunuku PhD Waziri wa ujenzi Dk. John Magufuli katika mahafali iliyopita ya Chuo Kikuu hicho
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Balozi Fulgence Kazaura kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kipindi kingine cha miaka minne.
Taarifa iliyotolewa leo, Jumanne, Oktoba 18, 2011, na Katibu Mkuu Kiongozi Phillemon Luhanjo imesema kuwa uteuzi huo unaanza mara moja leo hii.
Balozi Kazaura alikuwa Mkuu wa Chuo hicho katika kipindi kilichopita kilichoishia Julai, mwaka huu, 2011.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
18 Oktoba, 2011
Posted by newstz.blogspot.com
0
comments»





