Mkoani Dar es Salaam, mbio hizo zimeonekana kuwaweka pabaya Mwenyekiti wa UWT wa mkoa huo Zarina Madabida na Katibu wake, Tatu Maliaga baada ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, John Guninita kueleza kuwa viongozi hao watafikishwa kwenye kamati ya maadili kueleza kwa nini wamesitisha uchaguzi wilayani Kinondoni.
Habari kutoka Hanang' zimeeleza kuwa Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya hiyo imemwengua Dk Nagu na kuwabakiza wagombe wawili, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Leonsi Marmo.
Taarifa kutoka kwenye kikao hicho kilichofanyika juzi katika Ofisi ya CCM ya wilaya hiyo na kuhudhuriwa na wajumbe 12 zimeeleza kuwa Dk Nagu ameenguliwa kutokana na maelezo kuwa kanuni hazimruhusu kugombea.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa kanuni iliyomwondoa Dk Nagu kwenye kinyang’anyiro hicho ni ile inayowataka viongozi wenye kazi za kila siku; ubunge na uwaziri kutogombea.
Imeelezwa kuwa jitihada za wajumbe watano waliojipambanua katika kikao hicho kumtetea Dk Nagu ziligonga mwamba, baada ya wenzao saba kuunga mkono uamuzi huo.
“Kikao kilikuwa kizito, lakini tulitazama zaidi kanuni, sifa za wagombea na uwezo wa wagombea hasa katika nafasi hii nyeti ya Nec kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Alisema mapendekezo ya kikao hicho, tayari yamefikishwa ngazi ya CCM mkoa kwa uamuzi zaidi na baadaye yatafikishwa Kamati Kuu (CC) ya CCM.
“Sisi tumemaliza kazi yetu, tunaamini kuwa tumetenda haki kwa manufaa ya chama chetu Wilaya ya Hanang’,” alisema kiongozi huyo.
Hata hivyo, mjumbe mwingine wa kikao hicho alisema, mgawo wa mkopo wa matrekta ambao umekuwa ukiendelea Hanang’ umechangia kumwengua waziri huyo.
“Hapa kuna mambo mengi, nadhani hao waliokuwa na taarifa hizi, wameshindwa kueleza zaidi. Kuna mambo ya chinichini hasa baada ya baadhi ya viongozi kutounga mkono uamuzi wa Waziri Nagu kusaidia baadhi ya wanaCCM wakiwamo viongozi kukopeshwa matrekta,” alisema mjumbe huyo.
Kiongozi mmoja wa CCM Wilaya ya Hanang’ ambaye hakutaka jina lake litajwe, alikiri kufanyika kwa kikao hicho na kueleza kuwa tatizo la Dk Nagu ni kutoombewa kibali na kamati ya siasa wilaya au mkoa kama kanuni zinavyotaka.
Alieleza kuwa kanuni za CCM zinataka viongozi wenye majukumu ya kila siku kuombewa kibali kwanza na Kamati ya Siasa ya Wilaya au Mkoa kabla ya kugombea jambo ambalo halikufanyika kwa Dk Nagu.
“Hadi kikao hicho kinafanyika, Dk Nagu alikuwa hajaombewa kibali hicho na hili limetokana na migogoro ya kisiasa iliyoko wilayani Hanang’,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu hilo, Katibu wa CCM Wilaya ya Hanang’, Allan Kingazi alisema: “Ni kweli kikao kilifanyika, lakini mapendekezo yetu ni siri na hao waliokuambia wamekiuka kanuni. Sisi baada ya kumaliza kikao chetu, mapendekezo yetu tumeyapeleka ngazi ya mkoa ambako pia yataendelea kuwa siri hadi majina yatakapotangazwa rasmi,” alisema.
Uamuzi wa Dk Nagu kuamua kugombea NEC kupambana na Sumaye ambaye ndiye alimwachia jimbo hilo, ulitabiriwa kuibua mgawanyiko mkubwa ndani ya wana CCM wa Hanang’.
Jitihada za gazeti hili kumpata Dk Nagu kuzungumzia uamuzi huo zilishindikana baada ya simu yake ya mkononi kuita muda mrefu bila kupokewa.
Kuenguliwa kwa Dk Nagu kunatokana na sababu za kuwa na kazi za muda wote kumeibua hofu kuhusu hatima ya viongozi wengine waliochukua fomu ambao kwa mujibu wa kanuni iliyomwondoa Dk Nagu nao hawakupaswa kugombea.
Hao ni pamoja na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Abdallah Kigoda, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk Emmanuel Nchimbi.
Wengine ni Wabunge Deo Filikunjombe (Ludewa), Mussa Azzan Zungu (Ilala), Dk Hamis Kigwangalla (Nzega) na Andrew Chenge (Bariadi Magharibi).
Salma akosa mpinzani Lindi
Katika hatua nyingine Mke wa Rais, Salma Kikwete amerudisha fomu ya kuwania ujumbe wa Nec Taifa kupitia Wilaya ya Lindi Mjini.
Katibu wa CCM Wilaya ya Lindi Mjini Mohamed Kateva, alisema jana kwamba Salma ni mgombea pekee aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo katika wilaya yake.
Kateva alisema mwisho wa kurudisha fomu ilikuwa Agosti 28, mwaka huu na mpaka tarehe hiyo hakukuwa na mtu mwingine aliyekuwa amejitokeza kuwania nafasi hiyo.
Madabida kiti moto
Katika Mkoa wa Dar es Salaam, Madabiba na Maliaga watahojiwa kwa kukiuka uamuzi ya Halmashauri Kuu ya Mkoa.
Viongozi hao wanadaiwa kusimamisha uchaguzi wa UWT Wilaya ya Kinondoni ambao ulipangwa kufanyika Agosti 31, mwaka huu.
Alisema katika kikao chake cha Agosti 29, mwaka huu Nec Mkoa kilipitisha wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika wilaya zote tatu na kuagiza uchaguzi ufanyike.
CHANZO - MWANANCHI
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini ambapo bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepanda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo jana bei mpya zitaanza kutumika kuanzia leo.
"Sambamba na kupanda kwa gharama halisi za uagizaji wa mafuta kutoka kwenye Soko la Dunia, bei za jumla na rejareja kwa mafuta aina zote zimebadilika ikilinganishwa na taarifa iliyopita ya Agosti 1, 2012," ilieleza taarifa hiyo.
Kaguo katika taarifa hiyo alieleza kuwa bei za rejareja kwa Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimeongezeka, ambapo Petroli imepanda kwa Sh 291 kwa lita sawa na asilimia 14.50; Dizeli Sh 199 kwa lita sawa na asilimia 10.26; na Mafuta ya Taa Sh 67 kwa sawa na asilimia 3.47.
"Bei za jumla kwa kulinganisha matoleo haya mawili zimebadilika kama ifuatavyo: Petroli imeongezeka kwa Sh 291.54 kwa lita sawa na asilimia 15.07; Dizeli Sh 199.57 kwa lita sawa na asilimia 10.68 na mafuta ya taa kwa Sh 67.29 kwa lita sawa na asilimia 3.63," aliseleza katika taarifa hiyo.
Alisema kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo kama ilivyokokotolewa na kanuni mpya iliyopitishwa na Ewura na kuchapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 454 la Desemba 23, 2011.
INADAIWA kwamba askari waliokuwa katika operesheni ya kuzuia mkutano wa Chadema katika eneo la Nyololo wilayani Mufindi, Iringa na ambayo ilisababisha kifo cha Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi walitolewa katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Mbeya.
Tayari tukio hilo limeibua mjadala mzito kiasi cha kumfanya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kuunda tume huru kubaini chanzo cha tukio hilo. Marehemu Mwangosi alizikwa juzi nyumbani kwao Tukuyu, mkoani Mbeya.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana zilisema kuwa polisi hao kutoka mikoa hiyo mitatu wakiwa wamesheheni vifaa mbalimbali likiwamo gari la maji ya kuwasha, walisafiri siku moja kabla ya mkutano huo wa Chadema na baadaye kuzuka vurugu zilizosababisha kifo hicho.
Marehemu Mwangosi aliuawa kwa mlipuko unaodhaniwa kuwa ni wa bomu ambao ulisambaratisha vibaya sehemu kubwa ya mwili wake.
Chanzo cha habari kutoka mkoani Dodoma kilisema: “Hapa kwetu kuna askari 10 na tunawafahamu kwa majina. Waliondoka hapa siku moja kabla ya tukio hilo wakiwa na gari la washawasha.”
Chanzo hicho kilisema kwamba awali, hawakuwa wakifahamu kama baadhi ya wenzao walichukuliwa na kupelekwa Iringa. “Tulikuja kuona kwenye gazeti picha na tulipofuatilia tukaelezwa kuwa ni kweli Dodoma ilitoa askari kwenda Iringa.”
Askari mwingine aliyekuwa katika operesheni hiyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kitaaluma, alikiri kuwa hadi jana baadhi yao walikuwa bado wako Iringa na kwamba walikwenda kwa agizo la wakubwa wake wa kazi.
“Sisi ni Watanzania, lakini tumelazimika kuyafanya hayo kwa sababu ya mkate (malipo). Kwa kweli haikuwa haki, kuwatoa askari na silaha kutoka mikoa mitatu kana kwamba wanakwenda kupigana vita!”
Alidokeza kwamba, askari wote waliotoka Dodoma walikuwa njiani kurudi mkoani humo, jana lakini gari la maji ya kuwasha liliendelea kubaki huko Iringa likiwa na dereva wake na askari mmoja mwenye cheo cha inspekta. Askari huyo alisema kwamba gari hilo lililazimika kubaki kutokana na hitilafu.
“Wengine wamerudi lakini, kuna wengine wenye gari la kuwasha bado walikuwa Iringa, gari lao limepata hitilafu kidogo,” kilisema chanzo hicho kutoka mjini Dodoma.
Mmoja wa askari hao alidaiwa kwamba hiyo inaweza kuwa moja ya sababu ya askari hao kumshambulia marehemu Mwangosi wakati mwenzao anayemfahamu akijaribu kuwazuia. "Hii inaonyesha kuwa askari hao waliompiga walikuwa hawamjui na huyu aliyekuwa akiwazuia, alimjua.”
Makamanda watupiana mpira
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen hakukubali wala kukanusha na badala yake alisema: “Mambo yote hayo yanatakiwa kujibiwa na Kamanda wa Iringa.”
Aidha, alisema sakata la kifo cha mwandishi huyo kwa sasa liko katika vyombo vya uchunguzi hivyo asingekuwa tayari kulizungumzia.
“Siwezi kusema kama askari wangu walikwenda huko au hawakwenda, isipokuwa ninachoweza kusema ni kwamba suala hilo lipo katika vyombo husika hivyo waachiwe wao au Kamanda wa Iringa ndiye mwenye majibu.”
Alipotajiwa jina la mmoja wa askari aliyeonekana katika picha za video na magazeti za tukio hilo kwamba anatokea katika moja ya vituo vyake, kamanda huyo alisema: “Mimi yakitokea Dodoma nitazungumza wala siyo mtu mwingine kwa hiyo, mambo ya Iringa siwezi kuyazungumza na kama tutaanza kila Kamanda kuzungumza jambo hilo hamuoni kuwa itakuwa ni kama vurugu?”
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alipopigiwa simu yake iliita tu bila kupokewa.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile alisema kwa kuwa tukio hilo limefanywa na polisi, mambo mengi yatazungumzwa lakini akasisitiza kwamba hajapeleka askari Iringa.
Alisema hakukuwa na agizo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi wala ombi kutoka Polisi Iringa kutaka askari wa kuongeza nguvu... “Taarifa hizo ni za uzushi kwani hazina ukweli wowote.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani alikanusha pia kuwapeleka askari wake Iringa akisema: “Hizo taarifa siyo za kweli. Hakuna askari yeyote aliyekwenda Iringa wakati wa vurugu zile.”
Mkutano wa DCI wavunjika
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba hakutaka kuzungumzia suala hilo akisema: “Hayo yote yameundiwa tume ngoja tuiachie ifanye kazi yake.”
Awali, DCI Manumba aliitisha mkutano na waandishi wa habari mkoani Iringa, ambao hata hivyo, ulivunjika baada ya kutokea kutoelewana baina yao.
Manumba alitaka kueleza ripoti ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, lakini waandishi hao walikataa kumsikiliza wakisema hawauamini uchunguzi huo kwa kuwa ulifanywa na polisi peke yao.
Kabla Manumba, hajaanza kuzungumza, Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Iringa (IPC), Frank Leonard alisema kutokana na msimamo wa waandishi wa habari wa mkoa huo hakutakuwa na uhusiano wa kikazi na polisi hadi pale tume zilizoundwa kuchunguza kifo hicho zitakapotoa taarifa sahihi juu ya mauaji hayo.
“Msimamo wetu ni kusitisha uhusiano wa kikazi baina yetu na jeshi la polisi hususan Mkoa wa Iringa, tumekuja hapa kwa sababu DCI umetuita na kama unataka kutupa taarifa ya kifo cha ndugu yetu basi waambie hao maofisa wa jeshi wa Iringa watoke nje,” alisema Leonard.
Akijibu madai hayo Manumba alisema: “Nia yangu ni kutoa taarifa ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, ndiyo maana niliwasiliana na mwenzenu ili tuweze kuzungumza, Polisi Iringa wataendelea kuwepo na waandishi wa habari mtaendelea kuwepo, matukio kama haya yapo na yataendelea kuwepo.”
Licha ya maelezo hayo, hakuna mwafaka uliofikiwa na mkutano huo ukavunjika.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili baadaye, DCI Manumba alisema: "Ni vyema wao wangenisikiliza kujua ninataka kuwaambia nini. Lakini, kwa kuwa kuna mkanganyiko, nimeona ni vyema jambo hili lisubiri tume ndipo watakuja kulizungumza.”
Waikataa Tume ya Nchimbi
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeiponda tume ya Dk Nchimbi kikieleza kuwa imeundwa ili kurudisha uhusiano kati ya Polisi na waandishi wa habari na si kutafuta chanzo cha tatizo.
Juzi, Dk Nchimbi alitangaza kamati ya kuchunguza mauaji hayo inayoongozwa na Jaji Mstaafu, Steven Ihema na wajumbe, Mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga, Mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, Mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mngulu.
Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu alisema Dar es Salaam jana kwamba: “Hii si tume ya kuchunguza mauaji, bali ina lengo la kurudisha uhusiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari ili kuwasahaulisha wananchi kwa sababu imeundwa na waziri ambaye naye anatakiwa kuhojiwa.” “Tunamwomba Rais Jakaya Kikwete ateue tume kama anavyoelekezwa na Sheria ya Tume za Uchunguzi ya mwaka 1992, ambayo inaruhusu kumhoji yeyote kasoro yeye Rais.”
Lissu alisema Rais Kikwete angeunda tume hiyo na Waziri Nchimbi na IGP Said Mwema wanatakiwa kujiuzulu ili kupisha uchunguzi akidai kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba walitoa amri ya mauaji hayo.
“Dk Nchimbi anatakiwa kumuiga Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye alijiuzulu akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani baada ya kutokea mauaji, akijiuzulu atajijengea heshima tofauti na sasa kwani wananchi wamesikitishwa na mauaji hayo,” alisema Lissu.
Mwanasheria wa Chadema, Mabere Marando alidai kwamba kuna mkakati uliowekwa na Serikali wa kukidhoofisha Chadema baada ya kuonekana kwamba ni tishio kwa CCM.
Mbali na Chadema, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), pia limesema halina imani na kamati hiyo likisema imekuwa kawaida kwa Serikali kuunda tume ambazo hazileti ripoti kwa wananchi.
“Tume zimekuwa zikiundwa bila faida yoyote, huku zikipewa muda kuchunguza yaliyotokea lakini matokeo yake huwa hakuna ripoti wanayorudisha,” alisema Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta, Hezron Kaaya.
Kaaya alisema tume zimekuwa zikiundwa na kuigharimu Serikali fedha nyingi za walipa kodi, lakini ripoti zake zinaendelea kuwa siri.
Imeandikwa na Habiel Chidawali, Dodoma, Hamida Sharrif Morogoro, na Tumaini Msowoya, Iringa na Lasteck Alfred na Juliana Malondo.
Chanzo - http://www.mwananchi.co.tz
![]() |
Wanahabari wa Iringa Wakitoka nje ya ofisi |
Wanahabari wa Iringa mchana wa leo wamegoma kupokea taarifa ya awali ya
uchunguzi wa kifo cha Mwandishi Daudi Mwangosi, aliyeuawa juzi
jumapili katika mkutano wa ndani wa Chadema uliokuwa ufanyike katika
kijiji cha Nyololo Iringa. Mkuu huyo alikataa shariti la wandishi la
kumtaka atoe taarifa hiyo bila kuwepo kwa polisi yeyote katika mkutano
huo. Kitendo hicho cha mkuu huyo kukataa shariti la wanahabari
kikapelekea waandishi kutoka nje ya ukumbi huo.Hivyo zoezi hilo
kushindikana.
Picha na habari , Said Ng'amilo. Mjengwablog
• AJALI YA MV SKAGIT, URAIS 2015
VYAITESA
na Mwandishi wetu
UPEPO wa mabadiliko ya kisiasa
uliozikumba nchi nyingi duniani,
unaelekea kukiathiri Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ambacho sasa
kinahaha kujinusuru kung’oka
madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015.
Chama tawala hivi sasa kina
msuguano mkubwa wa kiuongozi
ambapo baadhi ya viongozi wake
wamekuwa wakimshutumu Katibu
Mkuu, Willison Mukama, kwa
kukwamisha mikakati ya kujiimarisha
na kurejesha matumiani yaliyofifia
miongoni mwa wanachama wake.
Licha ya Katibu wa Itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye, wiki hii kukanusha
kutokuwa na msuguano na Mukama,
makada wa chama hicho
wamelidokeza Tanzania Daima
Jumapili, kuwa vita ya makundi ya
kuwania uongozi na ile ya ufisadi
inakitesa chama hicho.
Mnyukano wa kisiasa unaonekana
wazi hivi sasa ni baina ya Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, dhidi ya
kundi linalomuunga mkono aliyekuwa
Waziri Mkuu, Edward Lowassa,
anayetajwa kutaka kuwania urais
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015.
Wakati hali ya mambo ikionekana
kutokuwa nzuri ndani ya chama hicho,
nguvu kubwa sasa imehamishiwa
kwenye Bunge kwa lengo la
kuwadhibiti wabunge wa CHADEMA
ambao wanaelezwa kutishia uhai wa
chama hicho.
Makada wa CCM wamedokeza kuwa
wamebaini wabunge wa CHADEMA
mwaka 2005-2010 walilitumia vizuri
Bunge kujenga hoja za msingi ambazo
ziliwasaidia kujijenga na hatimaye
kupata wabunge 22 wa majimbo
kutoka watano.
Waliongeza kuwa kutokana na kubaini
jambo hilo, chama hicho kimeamuap
‘kuzishughulikia’ hoja zinazotolewa na
CHADEMA bila kujali kama zina
masilahi kwa taifa au la.
Inadaiwa kuwa viongozi wa Bunge
nao wamepewa maelekezo ya
kukisaidia chama chao hasa
wanapoona kuna hoja zinazoelekea
kuwapatia umaarufu wabunge wa
CHADEMA.
Tanzania Daima Jumapili,
limedokezwa kuwa pamoja na
maelekezo hayo baadhi ya viongozi
wa Bunge wameonekana kushindwa
kukisaidia chama tawala kwa sababu
ya kutozijua ipasavyo kanuni, hivyo
kutumia ubavu kukataa jambo
linalotolewa na wapinzani, hivyo
kuwaongezea umaarufu.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai,
anatuhumiwa kutoa fursa zaidi kwa
wabunge wa CCM kurudia maneno ya
dharau na lugha ya kuudhi dhidi ya
wapinzani.
Kiongozi huyo pia juzi alionesha
‘ukada’ wake pale alipojifanya kukosea
jina la Mbunge wa Viti Maalumu, Rose
Kamili, kwa kumuita Rose Kamili Slaa,
ilhali akijua mbunge huyo
alishatarikiana na Dk. Slaa.
Hata hivyo CCM hivi sasa pia
kinakabiliana na wakati mgumu wa
kushutumiwa kushindwa
kuwachukulia hatua watendaji wake
wanaobainika kufanya uzembe katika
shughuli zao za kila siku.
Ajali ya mv Spice Islanders iliyotokea
mwaka jana na mv Skagit iliyotokea
wiki iliyopita inadaiwa ilichangiwa na
uzembe wa wataalamu kwa
kushindwa kukagua ubora wake.
Serikali ya CCM pia inalaumiwa kwa
kushindwa kuwa na vifaa vya kisasa
vya uokoaji licha ya kila mara
kukumbwa na matukio ya ajali za
baharini na ziwani.
Katika ajali hizo mbili za majini
zilizopoteza maisha ya Watanzania
zaidi ya 400, serikali ya CCM
inalaumiwa kwa kushindwa
kusimamia sheria za usafiri wa majini
na kuficha taarifa ya uchunguzi wa
ajali ya awali.
Mmoja wa wabunge wa CCM ambaye
jina lake limehifadhiwa, aliilaumu
serikali kwa kuunda tume kuchunguza
ajali ya mv Bukoba na Spice Islanders,
lakini haikutoa matokeo ya uchunguzi
huo.
“Serikali iliunda tume kuchunguza ajali
ya awali ya mv Spice Islanders na mv
Bukoba lakini ikaficha matokeo ya
uchunguzi wake. Leo imetokea ajali
nyingine na binafsi naamini kama
matokeo ya uchunguzi wa awali
yangetolewa, bila shaka ajali ya juzi
ingeepukika,” alisema kada huyo.
Kufichwa kwa matokeo ya uchunguzi
wa ajali za awali za majini,
kumeelezwa kuwa ndiyo sababu ya
Spika wa Bunge, Anne Makinda,
kuzima hoja za wabunge wa kambi ya
upinzani walioungana na wabunge
wote wa Zanzibar kutaka kujadili ajali
ya mv Skagit iliyosababisha vifo vya
zaidi ya watu 150.
Chanzo: FreeMedia
• WAPINZANI WANG’ANG’ANIA
ISIPITISHWE
na Salehe Mohamed, Dodoma
UTORO wa wabunge uliokemewa na
Spika wa Bunge, Anne Makinda, wiki
iliyopita jana ulikwamisha kupitishwa
kwa bajeti ya Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika.
Wiki iliyopita Makinda alisema utoro
kwa wabunge hivi sasa umekithiri na
akaonya kuwa kama wataendelea na
tabia hiyo ipo siku watakwamisha
upitishaji wa bajeti ya wizara husika.
Utabiri huo wa Spika Makinda, jana
ulitimia baada ya wabunge hasa wa
kambi ya upinzani kuibua hoja ya
kukwamisha upitishwaji wa bajeti ya
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
kwa mwaka 2012/2013 kutokana na
uchache wa wabunge.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia
(NCCR-Mageuzi), ndiye aliyekuwa wa
kwanza kutoa hoja kwa kutumia
kanuni ya 112 ambapo alitaka bajeti
hiyo isipitishwe kwa kuwa wabunge
waliopo hawajafikia nusu ya wabunge
wote.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni
inataka Bajeti ipitishwe ikiwa idadi ya
wabunge waliohudhuria itafikia nusu
ya wabunge wote.
“Hapa tulipo mimi nimeshahesabu
mara mbili wabunge wote hatuzidi
110, na tunajua idadi ya wabunge
wote ni 352 na nusu yake ni wabunge
175, ili tutende haki nakuomba
uhesabu idadi ya wabunge waliopo
kabla ya kupitisha bajeti hii ili
tuwatendee haki Watanzania,”
alisema.
Baada ya hapo alisimama Mbunge wa
Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-
Mageuzi) akitumia kanuni ya 77 (1) na
(2) kuwa wabunge waliopo hawafikii
nusu ya wabunge wote.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni ya
77 (1). Akidi kwa kila kikao cha Bunge
wakati wa kufanya maamuzi itakuwa ni
nusu ya wabunge wote, kama
ilivyofafanuliwa katika ibara ya 94 ya
Katiba, isipokuwa kwamba idadi hiyo
haitahusu hoja kuhusu uamuzi wa
kubadilisha masharti yoyote ya Katiba
kwa mujibu wa Ibara ya 98 ya Katiba.
“Mbunge yeyote aliyehudhuria
anaweza kumjulisha Spika kwamba,
wabunge waliopo ni pungufu ya akidi
inayohitajika kwa ajili ya shughuli
inayoendelea.
“Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Naibu
Spika, nasisitiza kuwa hatufiki nusu
humu ndani,” alisema.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses
Machali (NCCR-Mageuzi) naye
alisisitiza kanuni hiyo hiyo kipengele
cha tatu. “Endapo Spika ataridhika
kwamba kweli idadi ya wabunge walio
ndani ya Ukumbi wa Bunge ni
pungufu ya akidi inayohitajika basi
atasimamisha shughuli za Bunge kwa
muda atakaoutaja na atamwagiza
katibu kupiga kengele.”
Naibu Spika Job Ndugai, alisema idadi
hiyo inatakiwa wakati wa kupiga kura
ya mwisho ya kuipitisha bajeti hiyo si
wakati wa hatua za awali za kamati ya
matumizi.
Kauli hiyo ilimfanya Mnadhimu wa
Kambi Rasmi ya Upinzani, Tundu
Lissu, asimame na kutaka kiti cha
Spika kisiliburuze Bunge kwa kukiuka
kanuni na kuliomba Bunge liahirishe
shughuli hiyo.
Hata hivyo Ndugai hakukubaliana na
kauli ya Lissu. Ndugai huku akisema
kuahirisha shughuli za Bunge ni
gharama kubwa, alichukua muda
kuamua jambo hilo.
Ndugai aliamuru Kamati ya matumizi
iendelee huku Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),
William Lukuvi, alitoka nje
kuwahamasisha wabunge warejee
ukumbini. Mbali na juhudi za Waziri
Lukuvi pia kengele ilikuwa ikipigwa nje
ya ukumbi wa Bunge kuwahamasisha
warejee ukumbini.
Juhudi zakwama
Pamoja na jitihada za viongozi
mbalimbali wa serikali na Bunge
kuhakikisha idadi ya wabunge inafika
nusu, jambo hilo lilishindikana na
ndipo Ndugai alipoamua kuahirisha
shughuli za Bunge.
“Ni Vizuri wananchi waelewe kuwa
tuna huu msiba wa kitaifa
unaoendelea Zanzibar kuna wabunge
wenzetu wako kule Zanzibar hasa
kutoka Zanzibar kwa ruhusa ya
Spika…, kuna mawaziri na manaibu
wapo kule na wengine wako kule kwa
shughuli maalumu.
“Kuna wabunge kadhaa ambao mimi
mwenyewe nimewaruhusu wapo
kwenye msiba wa mazishi ya mama
wa mbunge mwenzetu, Mike Lekule
Laizer (CCM).”
Wakati Ndugai akiendelea kutoa
ufafanuzi huo, wabunge wa upinzani
walikuwa wakitoa kauli na kugonga
meza kuonesha kupinga utetezi huo.
Vitendo hivyo vilimfanya Ndugai
kuwataka wamsikilize badala ya kupiga
kelele ambazo haziwasaidii, kwakuwa
kiti cha Spika hakiwezi kumkandamiza
mtu.
“Nawaombeni ndugu zangu
tunaposikilizana kama watu wazima…
tupeane nafasi, mnalolitaka litakuwa
…..mkisema nyinyi nawapa
nafasi….mimi nikisema mnaanza
kupiga kelele.
“Inanisikitisha sana tunapovunjiana
heshima, tunakuwa kama watoto
wadogo, mimi sidhani kama
inatujengea heshima mahali popote
katika nchi yetu, tunafanya jambo la
msingi la taifa,” alisema.
Alisema kwa busara alizonazo
ameamua kuahirisha kikao hicho,
hatua ya kamati ya Bunge zima hadi
Jumatatu (kesho).
Baada ya kauli hiyo wabunge wengi
hasa wa upinzani walikuwa wakipiga
meza kwa kushangilia ‘ushindi’
walioupata.
NCCR-Mageuzi wakomalia
Mara baada ya Bunge kumalizika
wabunge wa NCCR-Mageuzi
walikutana na waandishi wa habari na
kuweka bayana kuwa hivi sasa
wanafanya uchunguzi kujua ni vikao
gani vilifanyika bila idadi ya wabunge
kutimia, baada ya hapo wapeleke hoja
kutaka maamuzi yaliyofikiwa
yatenguliwe.
Mbunge wa Kasulu Kusini, David
Kafulila, alisema maamuzi mengi
yamekuwa yakifanywa bila akidi
kutimia, jambo ambalo ni hatari kwa
maendeleo ya taifa.
“Tutaomba Spika atupe orodha ya
wabunge waliohudhuria katika kikao
hiki cha Bajeti na tukibaini tutaomba
maamuzi yaliyoafikiwa yatenguliwe,”
alisema.
Chanzo FreeMedia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete amesema kuwa
hali ya mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC)
inatia wasiwasi na hivyo Tanzania
inafuatilia kwa makini hali
inavyoendelea katika eneo hilo la
nchi hiyo jirani.
Aidha, Rais Kikwete amesema
kuwa Tanzania ingependa kuona
hali ya amani inarejea katika DRC
kwa sababu nchi hiyo inahitaji
kupata muda wa amani ili
waelekeze nguvu zake kwenye
maendeleo badala ya kupigana.
Rais Kikwete amesema hayo jana,
Jumanne, Juni 3, 2012, wakati
alipokutana na kufanya
mazungumzo na Profesa Ntumra
Luaba Alphonce, Katibu Mtendaji
wa Umoja wa Nchi za Maziwa
Makuu wa International
Conference on Great Lakes Region
(ICGLR) kwenye Hoteli ya Roca
Golf mjini Bujumbura, Burundi.
Rais Kikwete akifuatana na Mama
Salma Kikwete alikuwa mjini
Bujumbura kushiriki katika
Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa
Burundi na kurejea nyumbani jana,
3 Juni, 2012. Kabla ya kuja hapa,
Rais Kikwete alikuwa mjini Kigali,
Rwanda, kushiriki katika sherehe
za namna hiyo zilizofanyika Julai
Mosi, mwaka huu. Rwanda na
Burundi zilipata uhuru kutoka kwa
Wabelgiji Julai Mosi na Julai 2,
mwaka 1962.
Rais Kikwete amemwambia Katibu
Mtendaji huyo: “ Kwa hakika hali
mashariki mwa Congo inatutia
wasiwasi mkubwa na Tanzania
inafuatilia kwa makini hali hiyo.
Congo imekuwa katika vita muda
mrefu kupita kiasi kwa sababu
tokea mwaka 1997 imekuwa katika
vita mfululizo.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Wakati
umefika kwa Congo kutulia ili
nguvu inayoingia katika
mapambano na vita ielekezwe
katika maendeleo ya wananchi wa
nchi hiyo.”
Rais Kikwete pia ameunga mkono
wazo la kuitishwa kwa mkutano
wa mawaziri wa nchi wanachama
wa ICGLR ili kujadili hali ilivyo
katika mashariki mwa Congo
kufuatia ombi la DRC kutaka
kuitishwa kwa mkutano huo.
Hali katika mashariki mwa Congo
imeanza kutia wasiwasi baada ya
kikundi cha waasi wa Serikali ya
nchi hiyo wakiongozwa na jambazi
la kivita John Bosco Ntaganda
kuanza tena harakati zake za
kivita dhidi ya Serikali ya Rais
Joseph Kabila.
Usiku wa jana, Jumanne, Julai 3,
2012, alikutana na kufanya
mazungumzo na Rais wa
DRC,Mheshimiwa Kabila kuhusu
hali ilivyo mashariki mwa DRC.
Wakati akiwa Kigali,
Rwanda,mwishoni mwa wiki, Rais
Kikwete pia alikutana na kufanya
mazungumzo na Rais Paul Kagame
kuhusu hali ilivyo mashariki mwa
DRC.
Aidha, usiku huo huo wa kuamkia
jana, Rais Kikwete alikutana na
kufanya mazungumzo na Naibu
Waziri Mkuu wa Ubelgiji,
Mheshimiwa Didier Reynders
ambaye pia anahusika na masuala
ya nchi za nje, biashara ya nje na
masuala ya Umoja wa Ulaya (EU).
Katika mazungumzo Rais Kikwete
na Mheshimiwa Reynders
walizungumzia hali ya mashariki
mwa Congo pamoja na mchakato
wa ushirikiano ndani ya Jumuia ya
Afrika Mashariki (EAC).
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
4 Julai, 2012
Waziri wa Usalama wa ndani Profesa George Saitoti na Naibu wake Orwa Ojode wamefariki dunia katika ajali ya helikopta ya polisi iliyotokea leo asubuhi katika eneo la Kibiku, karibu na mji wa Ngong takriban kilometa ishirini kutoka mji mkuu wa Nairobi.
Abiria wote sita, wakiwemo marubani wawili na walinzi wa mawaziri hao waliokuwa kwenye helikopta hiyo wamefariki dunia na miili yao kuteketezwa kwa kiasi cha kutoweza kutambulika.
Kilichosababisha ajali hiyo bado hakijabainika. Bwana Saitoti na maafisa wengine wa juu katika wizara ya usalama wa ndani walikuwa wakielekea katika eneo la Sotik kwa mkutano wa usalama. Saitoti alikuwa miongoni mwa wanasiasa mashuhuri nchini Kenya waliokuwa wakipania kugombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Walioshuhudia ajali hiyo wamesema waliona helikota hiyo ikizunguka angani kabla ya kuanguka katika msitu wa Ngong.
Polisi wamezingira eneo la ajali hiyo na kamishna wa polisi Mathew Iteere aliyepo katika eneo la ajali anatarajiwa kutoa taarifa kamili kuhusiana na ajali hiyo.
Ajali hiyo ya helikopta imetokea katika siku ambapo Kenya inaadhimisha miaka minne tangu kutokea ajali ya ndege iliyowauwa mawaziri wengine wa serikali, Kipkalya Kones na Lorna Laboso.
Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amezuiwa kuwasilisha taarifa ya Tanzania kuhusu utekelezaji wa mpango wa Mpango wa kujitathmini wa Umoja wa Afrika (APRM), kwa sababu ya madeni makubwa yanayotokana na kutowasilishwa kwa michango kwa ajili ya uendeshaji wa sekretarieti ya mpango huo.
Ni kwa mantiki hiyo, Rais Kikwete alitarajiwa kuwasilisha ripoti ya Tanzania kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika (AU) utakaofanyika Lilongwe, Malawi Julai 10 mwaka huu, lakini habari zinasema deni hilo limekwaza mpango huo.
Twalib katika maelezo yake alikiri kwamba Rais Kikwete hatawasilisha ripoti ya Tanzania kwenye mkutano huo wa Lilongwe lakini akasema hilo halihusiani moja kwa moja na deni nchi inalodaiwa.
Hata hivyo, Twalib alisema licha ya kwamba Tanzania inapaswa kulipa madeni yake, lakini hakuna kipengele chochote kinachoipa Sekretarieti ya APRM mamlaka ya kuizuia nchi kutathminiwa katika mkutano wa wakuu wa nchi.
Alikiri kuwa deni hilo linachafua taswira ya Tanzania mbele ya nchi nyingine na kwamba lazima yalipwe kwani ilijiunga kwa hiari na kusaini makubaliano ya kutoa michango husika.
Deni la Tanzania
Rais Kikwete alipata taarifa za Tanzania kudaiwa na APRM katika kikao cha (NEC- CCM) Mei 15, mwaka huu mjini Dodoma na inaelezwa kwamba zilimsutua.
Taarifa iliyowasilishwa NEC ambayo Mwananchi limeiona, inaonyesha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2012/13 APRM Tanzania wameomba kuidhinishiwa kiasi cha Sh5.194 bilioni kwa ajili ya kugharamia kazi zake lakini maombi yaliyowasilishwa Hazina na wizara kwa ajili ya mango huo ni Sh1.149 bilioni tu.
Taarifa hiyo inaonyesha kwamba kiwango kinachopendekezwa kuidhinishwa na Bunge kinaweza kutosheleza kugharamia kazi za mchakato wa APRM nchini kwa miezi mitatu na kidogo ikilinganishwa na kile kilichoidhinishwa katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, mwaka huu ambacho ni Sh 2.04 bilioni.
Tanzania pia inatajwa kwenye taarifa ya Sekretarieti ya APRM ya mwaka 2010 kwamba ni miongoni mwa nchi ambazo zimewahi kuwasilisha michango yake mara moja tu tangu iliposaini na kuridhia kushiriki kwenye mchakato wa kutathminiwa utendaji wake.
Nchi nyingine ambayo imewahi kulipa michango yake mara moja ni Sierra Leone wakati Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Djibouti, Sudani na visiwa vya Sao Tome na Principe hazijawahi kutoa mchango wowote.
Tanzania ni nchi pekee katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati inayodaiwa fedha nyingi ililinganishwa na majirani zake ambazo zinadaiwa kiasi cha fedha kwa Dola za Marekani kwenye mabano, Rwanda (300,000), Zambia (200,000), Kenya (100,000) na Uganda (400,000).
Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ezekia Wenje katika maoni ya Kambi ya Upinzani Bungeni, Julai 22 mwaka jana alihoji sababu za Serikali kushindwa kulipa deni hilo ambalo alisema linalitia aibu taifa.
“Deni la nchi yetu katika Sekretarieti ya APRM ngazi ya Bara la Afrika na malimbikizo yanafikia Sh 1.07 bilioni. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuthibitisha taarifa hizi na kujieleza ni kwa nini kwa kipindi chote hicho haikulipa ada ya uanachama APRM na lini italipa fedha hizo, kwani hii ni aibu kubwa kwa Taifa,” alisema Wenje.
APRM Tanzania
Mchakato wa kujitathini wa nchi za Afrika ulibuniwa na viongozi wa Afrika mwaka 2002, taasisi hiyo ilianza rasmi mwaka 2003 baada ya idadi ya wanachama iliyotakiwa kusaini mkataba huo kutimia.
Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika taarifa yake mwaka jana ilisema: “Kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali kutenga fedha kwa ajili ya mchakato huo sanjari na kulipia michango na ada ya uanachama kwa wakati.”
Hivyo hatua ya Tanzania kuzuiwa kuwasilisha taarifa yake kunaifanya iendelee kuchelewa zaidi kwani tayari muda uliotarajiwa kukamilisha mchakato huo ulikwishapita.
Wenje katika hotuba ya upinzani alibainisha kwamba: “Ni dhahiri kuwa nchi yetu imechelewa sana. Ni dhahiri kuwa Serikali haikutimiza wajibu wake kuhakikisha mchakato huu wa kujitathmini unatekelezwa kwa wakati kwani takriban miaka sita imepita tangu Bunge hili lipitishe uamuzi wa kuingia kwenye mchakato wa APRM, lakini hadi leo hatujaweza kupata ripoti ya mwisho ya APRM kuhusu nchi yetu.”
“Kwa kawaida kazi ya kujitathmini inapaswa kufanyika mara moja ndani ya kila miaka mitano, lakini kwa Tanzania huu ni mwaka wa saba bila kupatikana kwa ripoti ya mwisho. Nchi nyingine kama Ghana,Uganda na Rwanda tayari zimejitathimini na kupata ripoti zao za mwisho.”
CHANZO: MWANANCHI
BAJETI ya Serikali ya mwaka 2012/2013 inatarajiwa kutumia Sh15 trilioni katika vipaumbele saba ikilinganishwa na Sh13.5 trilioni zilizotengwa mwaka 2011/12.Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa aliileza Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi kuwa matumizi ya kawaida ya Serikali yanatarajiwa kuwa Sh10 trilioni na fedha za maendeleo ni Sh5 trilioni.
Dk Mgimwa alieleza kuwa kipaumbele cha kwanza katika Bajeti yake ya kwanza tangu kuteuliwa hiyo ni miundombinu. Kwa mujibu wa waziri huyo, miundombinu imegawanyika katika makundi manne ya reli, umeme, maji salama, usafirishaji na uchukuzi ambavyo vimetengewa jumla ya Sh4.5 trilioni. Vipaumbele vingine vya Serikali ni kilimo, viwanda, rasilimali watu, huduma za jamii, utalii, biashara ya ndani na nje na huduma za fedha.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa katika bajeti hiyo, fedha zilizopelekwa Wizara ya Uchukuzi kwa ajili miradi ya maendeleo ni Sh252 bilioni huku sekta ya usafiri wa reli ikitarajiwa kutumia Sh130 bilioni. Katika Bajeti hiyo ya maendeleo, Wizara ya Ujenzi imetengewa Sh693 bilioni, wakati sekta ya nishati ikiwa nayo imepewa umuhimu na mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka mikoa ya kusini umetengewa Sh325 bilioni. Mwelekeo huo wa bajeti unaonyesha pia kwamba, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetengewa jumla ya Sh364 bilioni.
Serikali Kuuza mashangingi
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zilisema katika mkakati wa kubana matumizi, Serikali itapunguza matumizi ya magari ya kifahari kwa kiwango kikubwa. Katika hatua hiyo, inatarajiwa pia kupiga mnada baadhi ya magari hayo yanayotumiwa na mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na wakurugenzi na kununua magari madogo yenye gharama nafuu. Hata hivyo, chanzo chetu kilisema waziri huyo hakufafanua suala hilo akisema atalizungumza zaidi wakati wa kuwasilisha Bajeti hiyo Mjini Dodoma.
Takwimu za Serikali za mwaka juzi, zilionyesha kuwa Serikali Kuu hadi na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ilikuwa ikimiliki magari 40,000, kati yake 11,000 yakiwa ya kifahari.Tayari Wizara ya Ujenzi kupitia timu ya wataalamu mwaka Aprili, 2007 ilitoa ripoti ya namna bora ya kupanga matumizi ya magari ya Serikali kwa kuangalia kila daraja la kiongozi, lakini ripoti hiyo iliishia mezani kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.
Baadhi ya wabunge wa CCM wanatarajia kuibana Serikali katika Bunge lijalo wakidai kuwa imeshindwa kutekeleza kwa ukamilifu Bajeti ya mwaka jana pamoja na kuwawajibisha baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi.
Katika mkutano uliopita, wabunge waliibana Serikali wakitaka mawaziri wanane, manaibu waziri wawili na watumishi wengine wa umma waliotajwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), wawajibishwe. Lakini wabunge hao wamesema Rais Jakaya Kikwete aliwafuta kazi mawaziri sita na kuwahamisha wizara wawili na kuwang’oa manaibu waziri wawili miongoni mwa waliotajwa na hawajaona juhudi za kuwawajibisha watuhumiwa wengine.
Mawaziri waliofutwa kazi ni William Ngeleja (Nishati na Madini), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omari Nundu (Uchukuzi), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara) na Mustafa Mkulo (Fedha). Waliohamishwa wizara ni Profesa Jumanne Maghembe (Kilimo) kwenda Maji na George Mkuchika (Tamisemi) kwenda Ofisi ya Rais, Utawala Bora. Manaibu Waziri waliotemwa ni Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Athumani Mfutakamba (Miundombinu).








