Awashangaa wanaomzushia kifo
** Asema wanamtakia maisha marefu
** Kisa: Siasa za makundi urais 2015
Waziri wa Maji, Profesa Marck Mwandosya amesema bado yupo hai na anaendelea vizuri na matibabu anayopatiwa nchini India.
Kauli hiyo ya Profesa Mwandosya inafuatia uvumi uliozagaa kuwa amefariki dunia kutokana na maradhi yanayomsumbua.
Aliwataka wananchi kupuuza taarifa zilizosambaa kuwa amefariki dunia.
Akizungumza kwa njia ya simu na Radio One kutoka nchini humo jana, Profesa Mwandosya alisema uvumi huo hauna ukweli wowote na umesambazwa na watu wachache wasiomtakia mema.
Alisema kwa ujumla afya yake inazidi kuimarika siku hadi siku tangu aanze kupata matibabu ya maradhi yanayomkabili.
Profesa Mwandosya alisema kutokana na kuimarika kwa afya yake anaamini muda wa kubaki hospitalini hapo ni mchache kuliko aliokaa.
Mwandosya alisema hawezi kukasirishwa na habari hiyo na badala yake anaamini Mungu bado anampenda na ataendelea kupokea dua zake na Watanzania wengi wanaotaka arejee salama.
“Mtu akikutakia kuzimu ni dalili njema, ni baraka kubwa kwani anakutakia maisha marefu,” alisema.
Aliendelea kueleza “Sisi waumini wa Mungu hatujui siku ya kufa hatujui saa, dakika wala sekunde, sasa kama watu wanasema hayo ninaamini wanaingilia uwepo wa Mungu,” alisema.
Akieleza kwa kuwathibitishia Watanzania kuwa anaendelea vizuri, juzi aliweza kusoma kitabu na kumaliza kurasa 120 kati ya kurasa 800 za kitabu hicho.
Alisema anaamimini wengi wa wananchi wanamtakia afya njema na ndio maana kila siku anapokea simu zaidi ya 30 za wanaomtakia mema na kuna baadhi ya wachache kwa sababu wanazozijua wanamtakia mabaya.
“Kuna watu wengi wananiombea mema ili niweze kurudi na afya njema, lakini wachache wanataka nirudi kwenye sanduku, naamini Mungu atasikia maombi yao pamoja na familia yangu nirudi huko salama niendelee na kazi ya kulijenga Taifa,” alisema.
Akizungumzia juu ya lini atarejea, Mwandosya alisema bado hajapata taarifa kamili kutoka kwa madaktari wake, hata hivyo alisema itakuwa mapema baada ya madaktari, wauguzi na wataalamu mbalimbali kuona kukubali anaweza kufanya hivyo.
Kufuatia uzushi huo wa kifo cha Mwandosya wanasiasa mbalimbali wametaka jambo hilo lilaaniwe, huku wakilihusisha na siasa za makundi katika kuelekea uchaguzi mkuu 2015
Akizungumzia uvumi huo, aliyekuwa mbunge wa Vunjo Aloyce Kimaro, alisema hilo ni jambo lililopangwa kwa ajili ya mbio za urais mwaka 2015.
“Mimi sitaki kujiingiza sana katika mambo hayo lakini ukweli ni kwamba uvumi huo wa kusikitisha, malengo yake ni siasa za uchaguzi mkuu ujao,”alisema. Aliwataka wanasiasa kuwa wastaarabu, kwani kumzushia mtu kifo maana yake ni kumuombea afe, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kimaro alisema serikali inapaswa kuwashughulikia watu wanaopenyeza uzushi kwenye jamii.
Naye Kada wa CCM, Tambwe Hiza alisema ameshangazwa na taarifa hizo.
Tambwe alipopigiwa simu na gazeti hili alisema kwa mshangao “He, wanamzushia kifo rais mtarajiwa? Hii mbaya sana”.
Mwanasiasa huyo alisema inawapasa waliosambaza uvumi huo kulaaniwa na Watanzania wote.
“Hebu fikiri, wewe una baba yako kisha unaambiwa kwamba kafariki, utakuwa kwenye hali gani? Nawapa pole familia ya Mwandosya kwa vile bila shaka ilikuwa katika wakati mgumu,”alisema
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Categories: