TFF YAANZA KUVURUGA LIGI DARAJA LA KWANZA,WACHEZAJI 22 WA SMALL KIDS WATINGA UWANJANI KUIVAA POLISI IRINGA,MCHEZO WAVURUGIKA


SHIRIKISHO la mpira wa miguu Tanzania (TFF) lawamani kwa kuvuruga ligi daraja la kwanza ngazi ya Taifa baada ya timu mbili kugongana katika uwanja wa Samora mjini Iringa ambao ni uwanja wa nyumbani kwa timu ya Polisi Iringa zote zikitaka kucheza na polisi.

Tukio hilo lilitokea muda mufupi kabla ya kuanza kwa mchezo huo wa fungua dimba la ligi hiyo daraja la kwanza kwa timu ya polisi Iringa kuwakaribisha wageni wake timu ya Small Kids kutoka mkoa wa Rukwa .

Katika hali iliyoishangaza timu ya polisi Iringa na mashabiki waliofika katika uwanja wa Samora kushuhudia mchezo huo ni baada ya kuona timu mbili za Small Kids kutoka Dar es Salaam na Small Kids kutoka Rukwa kuingia uwanjani huku zote zikiwa zimevalia jezi nyeupe zikitaka kukaguliwa ili kucheza na polisi Iringa.


Kutokana na timu hizo za Small Kids kutoka Dar es Salaam na Small Kids kutoka Rukwa kuingia uwanjani na kufanya uwanja kuwa na wachezaji 33 kwa timu zote tatu ikiwemo ya polisi Iringa ambayo ni timu pekee kufuata kanuni kwa kuingia na wachezaji 11 ,waamuzi wa mchezo huo na msimamizi wa kituo hicho cha Iringa ambaye ni mjumbe wa TFF Taifa Eliud Mvella 'Wamahanji " walilazimika kutumia busara ili kuepusha vurugu katika uwanja huo.

Msimamizi huyo alilazimika kukutana na waamuzi na kulazimika kuuvunja mchezo huo ili kutoa nafasi kwa TFF kujipanga upya na kuamua timu mmoja pekee ambayo inapaswa kucheza mchezo wa ugenini na Polisi Iringa badala ya kuja kufanya uvamizi kwa Polisi Iringa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi msimamizi wa kituo hicho Wamahanji alisema kuwa amelazimika kuuvunja mchezo huo hadi hapo Rukwa watajkapojipanga na kuleta timu moja badala ya kuleta timu yenye wachezaji zaidi 22 uwanjani .

Hata hivyo alisema aliweza kuwasiliana na TFF ili kujua timu yenye uhalali wa kucheza mchezo huo na kudai kuwa na timu ya Small Kids kutoka Dar es Salaam ila kwenye chumba cha ukaguzi timu zote mbili ziliingia kukaguliwa na uwanjani zote ziliingiza wachezaji .

Kaimu katibu wa chama cha mpira wa miguu mkoa wa Rukwa (RUREFA) Adolph Choma akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu alisema kuwa chanzo cha kuvurugika kwa mchezo na ligi hiyo ni uongozi wa TFF kutokana na hatua yake ya kubariki njama za kutaka kuiba timu hiyo zilizofanywa na wadau watatu wa michezo katika mkoa wa Rukwa.

Alisema kuwa anachotambua kuwa timu hiyo ambayo inajiita Small Kids ya Dar es Salaam ni timu yenye jina la Cosmo Poltan ambayo ilishuka daraja mwaka jana mkoani Tanga .

Alisema kuwa timu ya Small Kids usajili wake upo wilaya ya Mpanda mkoa wa Rukwa na sio Dar es Salaam na kuwa iwapo TFF itaiendelea kuitambua Small Kids ya Dar es Salaam basi iweze kuonyesha usajili wa timu hiyo.

Hata hivyo alisema kuwa maamuzi ya kuuza timu ni lazima uitishwe mkutano mkuu wa wanachama wote pamoja na chama cha soka cha wilaya husika lazima kiwe na taarifa huku chama cha soka mkoa ni lazima kiwe na taarifa juu ya uamuzi wa kuuzwa kwa timu husika japo kwa upande wa timu hiyo ya Small Kids ya Rukwa hakuna mkutano ulioitishwa kwa ajili ya kuuza timu hiyo na hata chama mkoa hakitambui kuuzwa kwa timu hiyo.

Categories: ,