Tumaini Msowoya, Iringa
WAKATI mitihani ya kidato cha nne ikiendelea nchini, mwanafunzi wa kidato cha sita Sekondari ya Tosamaganga, wilayani Iringa, amekamatwa akijiandaa kumfanyia mtihani huo mwanafunzi wa Sekondari ya Mwembetongwa, Kata ya Makorongoni, Manispaa ya Iringa.
Mwanafunzi huyo ambaye namba yake ya usajili Tosamaganga ni TSS 191226, aliamua kuingia kwenye chumba cha mtihani wa kidato cha nne, shule ya Mwembetogwa akiwa amevaa sare za shule kama wanafunzi wengine, ili kufanikisha lengo lake kwa kumsaidia mtihani wa kidato cha nne, mwanafunzi mmoja (jina tunalo).
Kwa mujibu wa Ofisa Elimu Mkoa wa Iringa, Joseph Mnyikambi, tukio hilo lilitokea juzi wakati wanafunzi hao wakijiandaa kufanya mtihani wa somo la Kiingereza.
“Kilichotokea ni kwamba, alijifanya mwanafunzi wa Mwembetogwa, hivyo akaingia kwenye chumba cha mtihani kama kawaida, akiwa amevaa sare kama wenzake. Akakaa kwenye kiti na kupewa karatasi ya kujibia ambayo aliiandika namba ya mtihani ya (mwanafunzi mhusika), aliyetakiwa kufanya mtihani huo, ndipo akakamatwa,” alisema Mnyikambi.
Akisimulia tukio hilo, Mnyikakmbi alisema dakika tano kabla ya kuanza kwa mtihani huo, msimamizi mkuu wa mitihani shuleni hapo, alipita kwa watahiniwa kuhakiki namba na picha zao, kupitia fomu maalumu inayoitwa ‘Photo entry Form’ kuthibitisha kama wanafunzi waliopo ndiyo wanaostahili kufanya mtihani.
Hata hivyo, alipofika kwenye kiti alichokuwa amekaa mtuhumiwa, alibaini picha iliyopo kwenye fomu yenye namba tofauti na sura ya mtahiniwa na kwamba, baada ya kuchunguza akabaini kuwapo kwa udanganyifu.
Ofisa elimu huyo alisema baada ya kubaini hilo, alipewa taarifa na kwenda shuleni hapo haraka kujua ukweli wa jambo hilo, kumtambua mwanafunzi aliyetaka kumfanyia mwenzake mtihani huo kinyume cha Sheria za Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).
“Mara ya kwanza alijifanya anasoma Tukuyu, lakini baada ya kubanwa zaidi ilibidi aseme ukweli kwamba, yeye ni mwanafunzi wa kidato cha sita Tosamaganga, akichukua masomo ya Fizikia, Kemia na Bailojia (PCM) na kwamba, ameamua kumsaidia mwenzake baada ya kuombwa,” alisema Mnyikambi.
Hata hivyo, Mnyikambi alisema mwanafunzi halisi aliyepaswa kufanya mtihani huo alikuwapo kwenye mazingira ya shule, aliyekamatwa hakuwa ameanza kujibu maswali, aliruhusiwa kuendelea na mtihani wake wakati suala hilo likishughulikiwa ngazi nyingine.
Alisema katika maelezo yake, mwanafunzi huyo wa Tosamaganga alisema hakupewa kiasi chochote cha fedha kumfanyia mwenzake mitihani, bali ni kutokana na urafiki uliopo baina yao.
Alisema mtuhumiwa alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa saa kadhaa, kabla ya kuachiwa kwa dhamana.“Ni ajabu mwanafunzi wa PCM kumfanyia mwenzie mtihani wa Kiingereza, suala la kuingia kwenye chumba cha mtihani ni kosa. Tayari tumetoa taarifa Baraza la mitihani na masuala mengine ya kisheria yatafuata...kwa sababu tumezuia uhalifu, labda angekuwa amemjibia,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sekonsari ya Mwembetogwa, Mbatta alipofuatwa kutolea ufafanuzi jambo hilo, alikataa kuzungumzia akitaka apatiwe barua itakayowatambulisha waandishi wa habari na jambo wanalolitaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Evarist Mangala, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kwamba, taarifa rasmi itatolewa baada uchunguzi kukamilika.
CHANZO: MWANANCHI
Categories: