Showing posts with label Godbless Lema. Show all posts
Showing posts with label Godbless Lema. Show all posts

MWENYEKITI WA CHADEMA AFIKISHWA MAHAKAMANI JIJINI ARUSHA LEO


Habari Na Mery Ayo,Arusha.

Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo(chadema) Bw Freeman Mboye leo amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi kwa makosa mawili ambayo aliyafanya mjini hapa na kukiuka sheria za nchi

Akisomewa mashtaka na mwendesha mashtaka wa serikali Bw haruna Matagani mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Bi Devotha Kamuzora, mtuhumiwa mboye alidaiwa kufanya makosa hayo wakati wa mkutano wa hadhara.

Aidha iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa katika kosa la kwanza mtuhumiwa alikuwa ni miongoni mwa watu ambao waliongoza mkutano baada ya muda wa mkutano kuisha jambo ambalo ni kinyume cha sheria na taratibu za jeshi la polisi.

Pia kosa la pili ni pamoja na kukataa kutii amri ya jeshi la polisi ambapo amri hiyo iliwataka kutawanyika kwa ajili ya sababu za kiusalama zaidi jambo ambalo mtuhumiwa huyo alikataa.

‘jeshi la polisi liliwataka wafuasi watawanyike baada ya kumazika kwa mkutanoa ambao ulikuwa na kibali halali lakini haikuwa hivyo badala yake waliendeleza mkutano pamoja na jeshi hilo kuwasihi juu ya kutawanyika hivyo sheria na amri za polisi zilikiukwa” iliongezwa mahakamani hapo.

Kutokana na mashitaka hayo mtuhumiwa huyo alikana mashitaka yote ambayo amesomewa na hivyo kuweza kuahirishwa kwa kesi hiyo mpaka November 22 mwaka huu ambapo itasomwa tena mahakamani hapo na mahakama iliridhia kumuachilia huru mara baada ya kukidhi masharti ya dhamana.

Hata hivyo kwa upande wa washitakiwa hao wanaotetewa na wakili methody kimomogoro ambaye pia ni wakili kwa upande wa watuhumiwa wengine.

Katika hatua nyingine mji wa arusha umeonekana kuwa shwari zaidi baada ya kusitishwa kwa maandamano ambayo yalikuwa yamepangwa kufanyika hali ambayo mpaka sasa inaonekana kuleta amani na utulivu
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

Mbowe amfuata Lema Magereza

** Amtaka atoke mahabusu kesho ili kuleta utulivu
**JK, Prince Charles wa Ungereza watakuwa Arusha
**Mkutano wa Mnyika waingia dosari, Polisi wavamia

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demekrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, atatoka mahabusu kesho (Jumatatu) na kufanya mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya NMC Ltd.
Mbowe ambaye alifika jijini hapa kumuona Lema katika Gereza la Kisongo, ambako amewekwa mahabusu tangu Jumatatu iliyopita, alisema amemwelekeza atoke kesho.
“Nimekuja hapa kumpa maelekezo Mbunge Lema atoke Jumatatu kwa sababu Jumanne vikao vya Bunge vinaanza na ni muhimu kwake kuhudhuria,” alisema.
Alisema wakati akienda kumuona gerezani, tayari makamishna wawili kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, pamoja na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha na Ofisa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha, walimtembelea mahabusu kumsihi akubali kutoka ili kuleta utulivu jijini hapa.
Alisema chama chake kimekubali kumwekea dhamana na kumwelekeza atoke mahabusu, kwa sharti walilowapa polisi kwamba baada ya kutoka mahakamani apokelewe na wafuasi wake na kusindikizwa hadi viwanja vya NMC Ltd ambako atazungumza na wapiga kura wake kuelezea yaliyojiri.
Alisema wameamua kufanya hivyo kutokana na vikao vya bunge kuanza Jumanne na kwamba anahitajika kuwepo bungeni.
Awali alisema chama hicho kilipanga kufanya mikutano mikubwa ya hadhara kwa muda wa siku saba kuanzia Jumatatu.
Alisema mikutano hiyo ilipangwa kuanza majira ya saa 4 asubuhi hadi saa 12 jioni, lakini Jeshi la Polisi limewaomba wasitisha kufanya mikutano hiyo kwa sababu katika wiki hiyo kutakuwa na ugeni wa watu mashuhuri jijini hapa.
Alisema polisi walisema ugeni wa kwanza ni ujio wa mtoto wa mfalme wa Uingereza, Prince Charles, ambaye atawasili jijini hapa tarehe 9 na baadaye atakuja Rais Jakaya Kikwete.
Kutokana na ugeni huo, Mbowe alisema polisi wameomba mikutano hiyo isifanyike ili kuleta hali ya utulivu.
Hata hivyo, alisema chama chake kimebeba dhamana hiyo na kuamua kusitisha kwa sharti kwamba Lema aruhusiwe kusindikizwa na wapiga kura wake baada ya kutoka mahakamani hadi kwenye viwanja vya NMC na kuzungumza na wananchi.
Alisema iwapo atazuiwa kufanya hivyo, basi chama chake kitatoa taarifa ya kufanyika kwa mikutano hiyo, licha ya kuwepo kwa ugeni huo.
“Polisi wasijaribu kuzuia wanachama kumpokea Lema wakati akitoka mahakamani Jumatatu wala kuzuia mkutano wake akizungumza na wananchi…mbunge amekaa mahabusu kwa wiki nzima, hivyo alikuwa na ujumbe mzito wa kuueleza umma, ni vema akipewa nafasi ya kuzungumza na wapiga kura wake,” alisema.
Alisema yapo mambo mengi yanayolalamikiwa kama vile suala la umeya, udiwani, manyanyaso ya polisi ambayo watayaeleza katika mkutano huo.
Alisema iwapo polisi watamzuia kufanya mkutano huo, watalazimika kufanya mikutano yao kama kawaida na kwamba ujio wa mtoto wa mfalme utakuwa ni kielelezo kizuri sana cha kupeleka ujumbe kimataifa.
“Mikutano ya siku saba ni maamuzi magumu sana ambayo chama ilifikiria kuchukua, bado ujio wa mtoto wa mfalme kwetu tunauona kuwa ni mzuri wa kupeleka ujumbe, pengine itakuwa ni wakati muafaka kwa dunia kujua yanayotokea Arusha na Tanzania kwa ujumla,” alisema.
MKUTANO WA MNYIKA WAINGIA DOSARI, OPOLISI WAVAMIA
Jeshi la Polisi mkoa wa Kinondoni limewakamata watu waliokusanyika kwa ajili ya kumsubiri Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika, kuwahutubia kwa madai ya kuhofia Al Shaabab.
Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na Diwani wa Sarange, Ephahim Kinyafu, Katibu Mwenezi wa jimbo, Ali Makwiro, mfanyakazi Ofisi ya Mbunge, Julius Mgaya na dereva wa gari ambalo lilikuwa limewekwa kipaza sauti, Jafari Mbaga.
NIPASHE Jumapili jana jioni ilishuhudia purukushani kati ya jeshi la polisi na wafuasi hao ambao walikusanyika eneo la Ubungo karibu na baa ijulikanayo kama Corner baa, kwa lengo la kumsubiri Mbunge wa jimbo hilo.
Wakati wakiendelea kumsubiri, ghafla majira saa 10:27 jioni zaidi ya polisi wanane wakiwa na magari na vitendea kazi mbali mbali walifika eneo hilo na kuanza kuwakamata viongozi hao pamoja na wananchi waliokuwa wamevalia sare za chama hicho.
Hata hivyo, kamata kamata hiyo ambayo ilidumu takriban dakika tano, ilisababisha wafuasi waliokuwepo eneo hilo kuduwaa na kushindwa kufanya chochote dhidi ya polisi hao.
Baada ya askari hao kuwakamata watu hao pamoja na gari lililokuwa limebeba spika, waliondoka eneo hilo na ndipo Mnyika alipowasili eneo hilo na kulazimika kutumia gari lake kama jukwaa kuwahutubia wananchi waliobaki.
Mnyika, aliwaeleza wananchi kuwa, polisi hawajafuata utaratibu.
“Polisi hawajafuata taratibu kwani wanawakamata viongozi waliochaguliwa na wananchi na wanawakataza kuongea na nyinyi kwa kisingizio kuwa kuna Al Shaabab, je swali la kujiuliza hawa Al Shaabab wanafuata nini hapa, nilitegemea wangenikamata mimi,” alisema na kuongeza:
“Ningependa hili la tishio la Al Shaabab ambalo linatumika kama kisingizio Rais atoe tamko, atueleze kuwa nchi ipo kwenye hatari, nakumbuka Jumamosi iliyopita jeshi la polisi hili hili lilizuia maandamano ya wanaharakati waliokuwa wakipinga Dowans na siku hiyo kulikuwa na mpira wa Simba na Yanga na mimi nilikuwa na mkutano Mbezi Msigani na ulifanyika vizuri mbona kisingizio hichi hakikutajwa,” alisema.
Aidha, alisema baada ya mkutano huo ataelekea polisi ili kujua hatma ya waliokamatwa kwa sababu polisi walitakiwa waandike barua kama alivyofanya yeye wakati wa kuomba kufanyika mkutano huo.
Akizungumzia kuhusu lengo la kuitisha mkutano huo, Mnyika alisema lililenga kueleza mafanikio ya jimbo, kukusanya maoni ya katiba ili ayapeleke bungeni.
Pia alisema lengo lingine lilikuwa ni kugawa nyaraka kwa wananchi zilizoelezea suala katiba ambazo hata hivyo mbunge huyo alieleza zimechukuliwa na polisi hao.
Kufuatia tukio hilo, Mnyika aliwaeleza wananchi kuwa, polisi watalazimika kulipa gharama zote ambazo zimetumika kufanikisha mkutano huo.
Katika maoni ya wananchi yaliyotolewa kwenye mkutano huo yalieleza kitendo cha serikali kutowashirikisha kwenye mchakato wa katiba mpya, upanda kwa gharama za maisha na kukataa kulipwa kwa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema wamelazimika kuuvunja mkutano huo kutokana na barua waliyoipokea kutoka kwa mbunge huyo kutojitosheleza baadhi ya mambo pamoja na kuhofia matukio ya kigaidi ambayo yamekuwa tishio nchi mbalimbali duniani.
Kenyela alisema alipokea barua hiyo jana (juzi) huku ndani yake ikionyesha imeandikwa kutoka Alhamis ya wiki hii (Novemba 3).
"Barua hii ya Mnyika iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho,'Maombi ya kushiriki ziara jimbo la Ubungo' ilikuwa na mapungufu kwanza haikutaja tarehe wala siku ya ziara hiyo, zaidi ilibainisha maeneo ya ziara kuwa ni Kibo na Usewe na muda ambao ni kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 12:00 jioni," alisema.
Kenyela alisema kutokana na tatizo hilo kujitokeza kwenye barua hiyo, jana (juzi) alilazimika kumwandikia barua mbunge huyo kumweleza upungufu huo kwenye barua yake.
Alisema barua aliyoiandika kwa Mnyika pamoja na sababu ya kutokuwa na tarehe na muda wa ziara iliyopangwa, pia alimweleza kuwa haikueleza ni ofisi/taasisi zipi ambazo atazizindua na majina ya wahusika wake.
"Hofu yetu sasa hivi ni haya matukio ya ugaidi yanayoendelea duniani, tulifikiri mbunge huyu angetujibu barua tuliyomwandikia badala yake, ameamua kufanya mkutano," alisema.
Hata hivyo, Kenyela hakubainisha idadi ya watu wanaowashikilia kutokana na tukio hilo.
CHANZO: NIPASHE
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

MH. GODBLESS LEMA AOMBA KUWALIPIA FAINI WAFUNGWA



Na Musa Juma, 

 MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amemuomba Mkuu wa Gereza kuu la Arusha, kumruhusu kuwalipia faini wafungwa 22 wanaotumikia vifungo vya makosa mbalimbali katika gereza hilo kutokana na kushindwa kulipa faini zao. Katika barua yake jana yenye orodha ya wafungwa hao kwa mkuu huyo wa gereza, Lema alieleza kuwa ofisi yake ya jimbo inataka kuwalipia faini wafungwa hao ambao wengi wamefungwa kwa makosa madogo na kushindwa kulipa faini. "Wafungwa hawa licha ya kusababisha msongamano, vifungo vyao vinatokana na ukweli kuwa Watanzania hao walishindwa kulipa faini na sio kwa ridhaa yao bali kutokana na hali duni ya maisha yao," ilisomeka sehemu ya barua hiyo. Lema ambaye bado yupo rumande katika gereza hilo, baada ya kugoma kuwekewa dhamana katika kesi ya kufanya maandamano na mkusanyiko bila kibali, alisema ofisi yake, inaomba kupatiwa majina yote ya wafungwa waliokosa faini walizotakiwa kulipa ili afanye utaratibu wa kuwatoa kwa kuwalipia faini hizo katika chombo husika.

"Nitafurahi utekelezaji huu kufanyika haraka ili kupunguza msongamano katika gereza hili na wafungwa hao kujumuika na wananchi wengine katika shughuli mbalimbali za maendeleo," alisema Mbunge Lema katika barua hiyo. Hadi jana tayari majina ya wafungwa 22 ambao wanatumikia kifungo baada ya kushindwa kulipa faini kati ya Sh 10Milioni na Sh200,000 yalikuwa yamepatikana.Wafungwa hao ni Rasul Hemed mwenye namba 262/2011,Hamis Jafari455/2011, Gabriel Martin105/2011, Simon Peter503/2011 na Emanuel Ndelekwa namba 400/2011. Wengine namba zao kwenye mabano ni Juma Seleman (60/2011)Bakari Ramadhani (354/2011) Ally Ramadhani (300/2011), Sakidi Athuman 305/2011) na Charles Mkama (555/2010). Wafungwa wengine ni Emanuel Bundala (457/2011) Mdoo Saruni (337.2011), Rajab Ally(450/2011), Lameck Abdiel (362/2011) Abdul Ismail (439/2011), Anold Philipo mwenye namba315/2011. Wengine ni Julius Ngadayo (377/2011),Ombeni Stephano (475/2011), Ney Sabas(111/2011), Bura Thomas(59/2011) na Emanuel Samweli (714/2007). Mwenyekiti wa mfuko wa Maendeleo wa Jimbo la Arusha (ARDF), Elifuraha Mtowe, alisema jana kuwa baadhi ya wananchi wameanza kutoa michango ili kufanikisha mpango wa kutoa gerezani wafungwa hao. Mgomo wa mabasi wasitishwa Hatimaye mgomo wa mabasi yanayotoa huduma ya usafiri jijini Arusha, maarufu kama ‘vifodi’, ulisitishwa jana na kuanza kutoa huduma kama kawaida. Mwandishi wa habari hizi alishuhudia jana katika kituo cha mabasi na vituo vidogo magari hayo yakiwa yanaendelea na kazi ya kubeba abiria.Baadhi ya madereva waliozungumza na Mwananchi walieleza kuwa, licha ya baadhi yao kumuunga mkono Lema kutokana na kupinga vitendo vya polisi na viongozi wengine wa usalama kutisha raia na kuwafungulia kesi kwa malengo ya kisiasa, wengine walisitisha huduma kwa kuogopa magari yao kuvunjwa vioo."Isingewezekana jana kutoa huduma magari yalikuwa yakitishiwa kuvunjwa vioo na vijana wanaodaiwa kuwa wa Chadema, sasa tuliona badala ya kupata hasara ya vioo bora tusitishe huduma," alisema Bakari Msangi. Waliohamasisha mgomo kusakwa. Jeshi la Polisi mkoani hapa, linaendelea kuwasaka vijana wanaotuhumiwa kuchochea mgomo wa mabasi uliotokea juzi na kusababisha adha kubwa kwa abiria wakiwemo wanafunzi. Hadi juzi jioni zaidi ya vijana 30 walikamatwa kuhusiana na vurugu hizo.Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Akili Mpwapwa, alisema jeshi hilo haliwezi kuachia watu wakiendelea kuchochea vurugu jijini Arusha. "Tunaendelea na uchunguzi na kuwasaka wote waliochochea mgomo na kufanya vurugu. Ingawa tayari tumewakamata baadhi yao, uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani," alisema Mpwapwa.Mbunge Lema alipelekwa mahabusu mapema wiki hii baada ya kukataa kuwekewa dhamana katika kesi inayomkabili ya kuandamana bila kibali na kuwafanya wafuasi wake wakiwemo madereva wa vifodi kusitisha shughuli zao juzi na kwenda kumtembelea gerezani.

[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

Lema awataka wafuasi wa Chadema gerezani


Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),Godbless Lema.





Habari na Peter Saramba na Mussa Juma, Arusha.

MBUNGE wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ambaye yuko mahabusu, amewataka wafuasi wa chama hicho kumtembelea gerezani kwa wingi leo ambayo ni siku ya kawaida ya kuona mahabusu, akiwataka wasiwe na hofu yoyote kufanya hivyo.

Lema alituma ujumbe maalumu kwa wanachama wa chama hicho akiwataka kuwa watulivu na kumwunga mkono katika harakati zake alizoziita za kupigania haki, usawa na demokrasia ya kweli nchini bila kujali vitisho vya dola.

Katika ujumbe wake huo uliotolewa na Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo Arusha (ARDF), Elifuraha Mtowe aliyemtembelea gerezani jana, Lema alisema ameamua kuchukua dhamana ya kukubali kwenda magereza ili kufikisha ujumbe kwa dola na wote wenye kujaribu kuwatisha wenye nia na kiu ya kupigania haki na usawa na kwamba yuko tayari kulipia gharama yoyote kukamilisha ndoto yake.

Aliwataka wananchi kuchanga fedha kwa ajili ya watu aliowakuta Magereza wakitumikia vifungo baada kushindwa kulipa faini walizohukumiwa kwa kutiwa hatiani kwa makosa madogo na alisema tayari ameomba kwa uongozi wa Magereza, orodha ya waliofungwa walioshindwa kulipa faini.

Kwa mujibu wa Mtowe, Lema amewakaribisha wananchi kumtembelea gerezani katika utaratibu wa kawaida wa wafungwa na mahabusu kutembelewa siku za Jumatano, Jumamosi na Jumapili.

Alisema uongozi wa Chadema Mkoa wa Arusha utaratibu ziara hizo kuhakikisha sheria, taratibu na kanuni za Magereza zinazingatiwa kwa wenye nia hiyo.

Lema gerezaniOfisa mmoja mwandamizi wa Gereza la Arusha ambaye alikataa kutaja jina lake, alisema mbunge huyo alifikishwa gerezani hapo juzi saa 10:00 jioni akiongozana na watu wengine 12 waliomsindikiza ambao licha ya kutokuwa watuhumiwa wala wafungwa, walikuwa tayari kuingia naye mahabusu.

Alisema ili kumhakikishia usalama, mbunge huyo ametengewa chumba maalumu na haruhusiwi kukutana na wafungwa au mahabusu wengine.

“Mheshimiwa Lema tumempokea vyema, tumempangia chumba chake maalumu na tumemweleza kuwa haruhusiwi kukutana na wafungwa au mahabusu wengine ingawa yeye alipendelea kuchanganywa kwenye seli ya kawaida ili achanganyike na mahabusu wengine.
Hana shida yoyote na jana alitembelewa na mkewe (Neema Lema), watu wasiwe na hofu yoyote kwani anatendewa haki sawa na wengine,” alisema ofisa huyo kwa simu jana.”

Alikanusha habari zilizozagaa mjini Arusha kuwa baada ya Lema kufikishwa gerezani, kulitokea mtafaruku wa wafungwa na mahabusu kupiga kelele kupinga uonevu wa vyombo vya dola, dhidi ya mbunge huyo kijana.

Ilidaiwa kelele na vurugu hizo za wafungwa na mahabusu zilitokana na redio moja ya mjini hapa kurusha hewani waraka maalumu wa Lema, akitangaza hiari yake ya kwenda mahabusu.

Hata hivyo, Kaimu Mkuu Magereza Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Marcel Lorry hakutaka kuzungumza lolote kuhusu suala hilo akisema anayeweza kufanya hivyo ni mkuu wa gereza alipo Lema jambo ambalo pia halikuwezekana.

Bavicha wachukizwa
Nalo Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) Mkoa wa Arusha, limemtaka Mkuu wa Polisi (IGP), Said Mwema kumng'oa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Zuberi Mwombeji kutokana na kile wanachodai kuwa ni kuwaonea viongozi na wafuasi wa chama hicho.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana,  Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Arusha, Ephata Nanyaro alisema wamechoka kunyanyaswa, kukamatwa ovyo, kupigwa na
kudhalilishwa na OCD huyo.

Mwenyekiti huyo wa Bavicha alitoa mfano wa jeshi la polisi kushindwa kuwachukulia hatua vijana wa CCM (UVCCM), walioongozwa na Kaimu Mwenyekiti wao wa Taifa, Benno Malisa kufungua matawi mjini hapa, kuandamana na kufanya mkutano wa hadhara bila kibali cha jeshi hilo licha ya shughuli hiyo kupigwa marufuku na OCD huyo aliongoza ulinzi katika shughuli hiyo haramu.

“Kaimu RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) alikiri kwamba vijana hao wa CCM walikaidi amri halali ya polisi. Badala ya kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, alitoa onyo. Maana yake ni kwamba utekelezaji na utendaji wa polisi Arusha unazingatia nani mhusika katika kosa na ana itikadi gani,” alidai Nanyaro.

Awali, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa alisoma taarifa ya kurasa tatu ambayo pamoja na mambo mengine, alitaja mambo mawili ya msingi yanayopaswa kushughulikiwa sasa na kwa haraka kurejesha amani, utulivu na maendeleo ya Arusha kuwa ni pamoja na vyombo vya dola kukomesha uonevu wenye lengo la kujenga hofu kwa wananchi, wanachama wa Chadema, viongozi wao.

Golugwa alisema msingi wa maendeleo ya jamii yoyote ni haki na usawa kwa wote na kutaka jeshi la polisi kuzingatia misingi ya sheria katika kutekeleza wajibu na dhamana waliyokabidhiwa na umma.

Chanzo: MWANANCHI
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

CHADEMA NGAZI YA MKOA WA DAR ES SALAAM YATOA TAMKO KALI KUHUSIANA NA SUALA LA MBUNGE WA ARUSHA MJINI.

Kulia ni Katibu wa Mkuu wa CHADEMA Kanda Maalum Bw. Henry Kilewo 
akisoma tamko la Chama cha CHADEMA Mkoa wa Kinondoni Kanda 
Maalum ya Dar es Salaam kuhusiana na suala la Mbunge wa 
ARUSHA Mjini Mh. Godbless Lema kukamatwa na kupelekwa 
magereza. Kushoto ni Katibu wa Vijana CHADEMA Mkoa wa 
Dar es Salaam Bw. Renatus Mlashami.






MKOA WA KINONDONI KANDA MAALUM YA DAR ES SALAAM


Tamko la katibu wa mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum ya Dar es salaam


Ndugu zangu wanahabari


Nimewaita hapa leo kwa lengo la kuwapa watanzania msimamamo wangu na wa chama ngazi ya mkoa kuhusu tukio la kukamatwa na kupelekwa magereza kwa Mhe. Godbless Lema Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini.


Imekuwa ikizoeleka kwa muda mrefu sasa kwamba waheshimiwa wabunge wa CHADEMA na wale wanaaotokana na vyama vya upinzani wamekuwa wakinyanyaswa sana kwa lengo la kuwafanya wajute kuingia katika siasa za upinzani Tanzania.


Hii kwa CHADEMA haitokei tu kwa waheshimiwa wabunge bali hata kwa viongozi wa ngazi zote. Inaonekana kuwa sasa serikali ya Chama Cha Mapinduzi imeamua kutekeleza kwa vitendo mkakati wa kuwatesa kwa siri na kwa wazi wale wote wanaoipinga siasa kandamizi na zisizowalazimisha watawala kuwajibika kwa wananchi.


Mkakati huu umetungwa na CCM, unasimamiwa na usalama wa taifa na unatekelezwa na jeshi la polisi. Kwa hakika hatuhoji tena kwamba jeshi la polisi ni kitengo cha kusimamia maamuzi na maelekezo ya CCM badala ya kulinda raia na mali zao.


Mheshimiwa Godbless kama mbunge wa wananchi wa jimbo la Arusha Mjini amekuwa akifuatwafuatwa na jeshi la polisi kila mara na kufanyiwa vitendo vingi vya udhalilishaji na unyanyasaji hasa kwa kupitia OCD wa Arusha Mjini Zuberi.

Mathalani wiki iliyopita siku ya ijumaa tarehe 28/10/2011 Mhe. Godbless lema akitoka mahakamani alisindikizwa na wananchi wake kutoka mahakamani hadi ofisini kwake. Wafuasi wake walipomfikisha ofisini waliondoka na kurejea makwao. Huko ofisini aliwakuta wananchi wakimsubiri ili awahudumie kama mbunge wajimbo lao. Wakati akiongea na wananchi ghafla polisi walifika na kuwakamata wananchi wote waliokuja kuomba usikivu wa mbunge na kuwapeleka kituo kikuu cha polisi.


Mbunge Lema alipokwenda kituo cha polisi kwa lengo la kuwawekea dhamana naye aliwekwa chini ya ulinzi kwamba eti amefanya maandamano bila kibali.


Tunahoji: Ni maandamano yapi hayo ambayo Lema aliyafanya na wananchi wake akiwa angali ofisini kwake? Je maandamano wanayoyazungumzia ni kuondoka na wananchi mahakamani hadi ofisini kwake? Je kama kuondoka kwake na wafuasi wake mahakamani ni kosa kisheria; Je kwa Mhe Ole Sendeka alipokuwa akitoka mahakamani, alikuwa akiondoka na kundi kubwa la wafuasi wake na kusindikizwa na OCD huyu huyu? Vile vile Mwenyekiti wa UV-CCM mkoa wa Arusha amekuwa akienda kituo kikuu cha polisi akisidikizwa na kundi kubwa la wafuasi wake wa CCM. Polisi hawakuwahi kuwakamata wala kuwaonya. Sasa haya yote yalikuwa maandamano ama matembezi ya hisani? Maana Arusha kuna msiba mkubwa wa CCM kukataliwa na wananchi.


Kwa hakika tukio la kukamatwa kwa Mhe Lema, kupelekwa mahakamani na hatima ye kupelekwa gerezani ni ushahidi wa kutosha kwamba jeshi la polisi sasa linakamilisha sehemu kubwa wa wajibu wake wa kuibaka demokrasia.


Hata hivyo tunalitaka jeshi la polisi na serikali ya CCM wajue kwamba kitendo cha kumpeleka Lema magereza ni ushindi tosha katika harakati za ukombozi wa taifa hili. Maana hakuna silaha yoyote duniani ama jeshi la polisi popote pale duniani ambavyo viliweza kushinda vita dhidi ya ukweli, haki na uwazi.

Ndugu zangu watanzania

Tunawaunga mkono wana Arusha kwa kumpata mbunge ambaye anayatetea maslahi yao kwa mzigo hata pale inapobidi kwenda gerezani kwa ajili ya watu wake na hata ikibidi kifo anaweza kusimamia hilo. Alisema Martin Luther King Jr. 1963 “A man who wont die for something is not fit to live” na akaendelea kusisitiza “Nobody can give you freedom, nobody can give you justice or right or anything. You take it!” (STAND UP; STAND UP 4, UR RIGHT) Hayo yalikuwa maono ya bob marley ambayo aliyaona mwaka wa 1973,baada ya kuwa amekaa katika mto mmoja huko jamaica akaona samaki wanapita katika maji lakini samaki wakubwa wakawa wanawaonea samaki wadogo,hivyo akaona hata hapa duniani hata wa2 walio juu wanawaonea watu wa hali ya chini.


Kwa watu wanaopinga ama kukejeli maamuzi ya Godbless lema kukataa dhamana, Wathubutu kufanya ziara huko Mahospitalini wavae sura za uhasilia wa kibinadamu wakaone watu waliokuwa kama wao jinsi wanavyotaabika kwa kukosa matibabu ile hali ni walipa kodi wa taifa hili. Kwanini Godbless asiende jela wakati anasimamia mambo ya msingi na hayatekelezwi, tukiandamana tunaonekana tunavunja sheria ni afadhali kwenda sehemu wanayodhani tunaogopa kuliko kukaa kimya kumbe hatuogopi. Mungu yupo upande wetu na tunaelekea kushinda unyanyaswaji huu.


Kama ambavyo alivyowahi kusema Martin Luther king jr, ndivyo tunavyo wahakikishia wana wa Arusha, we will work together; we will stand up together, we will go to jail together, until justice runs down like water. maana mateso tunayoyapata ni makubwa kuliko huko jehanam tusipopajua.


Kwa kuonyesha tuko pamoja katika harakati hizi za kudai demokrasia ya kweli tunampogeza Godbless lema mbunge wa Arusha mjini kwa kupeleka ujumbe kwa watawala wanaodhani wanaweza kutumia magereza kama sehemu ya vitisho kurudisha harakati zozote zile nyuma.


Ujumbe huu uwafikie watawala yakuwa jela sisehemu ya kumtishia mtu yeyote Yule mwenye akili timamu, mpenda haki bali ni sehemu ya kawaida ambapo binadamu yeyote Yule anaweza kwenda.


ASANTENI ASANTENI NA MUNGU AWABARIKI WATANZANIA WENZANGU!


Henry J Kilewo

KATIBU (M) Kanda Maalum

01/11/2011
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

Mbunge atimua mbio kuwakimbia polisi



Moses Mashalla na Peter Saramba, Arusha

MBUNGE wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema jana alilazimika kutimua mbio kujinusuru kukamatwa na polisi baada ya kutoka mahakamani kusikiliza kesi ya kupinga ubunge wake.Lema alilazimika kukimbia baada ya polisi kuwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa katika ofisi za mbunge huyo, wakisikiliza hotuba yake muda mfupi baada ya kuwasili kutoka mahakamani.

Baadhi ya wafuasi hao ambao walitoka katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwa maandamano hadi kwenye ofisi za Lema, walikamatwa na polisi katika patashika iliyodumu kwa dakika kadhaa.

Wafuasi hao walitoka katika mahakama hiyo kwa maandamano huku wakiimba nyimbo za hamasa na walipofika eneo la Barabara ya Boma walikutana na polisi ambao waliwataka kutoendelea na maandamano yao lakini wakakaidi amri hiyo.

Zaidi ya magari matano yaliyosheheni askari zaidi ya 50 wakiwa na silaha walijaribu kuwazuia wafuasi hao ambao pia walikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali bila mafanikio hadi walipowasili katika ofisi za mbunge.

Mara baada ya kufika hapo, Lema alianza kuwahutubia wafuasi hao akiwataka kamwe wasiwaogope polisi kwa kuwa wao wamewekwa kuhakikisha ulinzi wa raia ambao ndiyo ni wao.

“Msiwaogope polisi. Hawa wamewekwa kwa ajili ya kuwalinda nyie hivyo teteeni haki yenu bila woga,” alisema Lema.

Wakati akiendelea kuhutubia ghafla gari la polisi likiwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD), Zuberi Mwombeji lilifika eneo hilo la mkutano, kisha polisi kadhaa  kushuka na kuanza kuwatawanya wafuasi hao.

Baadhi ya wafuasi hao walipigwa virungu na kushambuliwa kwa mateke huku wengine wakikamatwa na kusekwa ndani ya magari ya polisi. Kuona hivyo, Lema alitimua mbio.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya magari yaliyokuwa yakipita Barabara ya Makongoro kuelekea Barabara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na ile ya Boma kushindwa kufanya safari zake kama kawaida.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa hakuwa tayari kutoa taarifa za tukio hilo kwa maelezo kwamba zilikuwa bado hazijamfikia.

Kwa upande wake, Lema alilaani hatua hiyo ya polisi huku akieleza kushangazwa na hatua ya askari hao kuwatawanya wafuasi wake na kuwashikilia baadhi yao.

Alidai kwamba polisi walivamia ofisi yake kwa nguvu na kutaka kuvunja mlango kwa lengo la kumkamata pamoja na wafuasi wake bila mafanikio.

Mahakamani

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imetoa hati ya kuitwa mahakamani hapo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na Mhariri wa Gazeti la Nipashe kwa maelezo kwamba waliingilia mwenendo wa kesi ya Lema.

Nape na mhariri huyo wanapaswa kufika mahakamani hapo, Novemba 16 mwaka huu.

Wito huo unatokana na hoja ya Wakili wa Lema, Method Kimomogoro aliyesema kwamba upande wa utetezi hauna imani na Jaji anayesikiliza shauri hilo, Aloyce Mujulizi kutokana  na matamshi  yaliyotolewa na Nape na kunukuliwa na Gazeti la Nipashe.

Wakili huyo alisema matamshi ya kiongozi huyo wa CCM yanaashiria kuwapo kwa njama za walalamikaji kushinda kesi hiyo isivyo halali.

Akiahirisha kesi hiyo jana, Jaji Mujulizi alikubaliana na hoja za Kimomogoro za kuitwa mahakamani hapo watu hao wawili na kwamba Nape anatakiwa aieleze mahakama hiyo juu ya matamshi yake yaliyonukuliwa na Nipashe toleo la Oktoba 9, mwaka huu.

Alisema mhariri wa gazeti hilo anapaswa kufika mahakamani ili kutoa uthibitisho juu ya matamshi aliyotoa Nape kupitia gazeti lake.

Mapema Kimomogoro aliieleza mahakama hiyo ya kuwa kitendo cha Nape kutoa matamshi yanayoashiria kuharibu mwenendo wa kesi hiyo ni kosa na kwamba kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa mahakama.

Wakili huyo alisema sehemu ya habari hiyo ilisema: “Nnauye alisema kwa sasa wako katika mchakato wa kwenda kupiga kambi katika Mkoa wa Arusha ili waweze kulichukua jimbo hilo. Alisema wana uhakika wa kushinda kesi yao dhidi ya Lema na kulichukua jimbo hilo uchaguzi utakapofanyika.”

Kimomgoro alisema matamshi hayo hayajawahi kukanushwa hadharani na kusisitiza ya kuwa mteja wake ambaye ni Lema, Chadema pamoja na wafuasi wa chama hicho wana shaka na kauli hiyo.

Hata hivyo, maelezo hayo yalipingwa na wakili wa walalamikaji, Alute Mughai ambaye alisema hizo zilikuwa mbinu za kuchelewesha kesi.

Kuhusu hoja ya kauli iliyotolewa na Nape, Wakili Mughai alisema mahakama hiyo haiwezi kusikiliza mambo yote yanayoandikwa kwenye magazeti hapa nchini huku akitoa onyo ya kuwa endapo mahakama hiyo itakuwa ikisikiliza mambo ya magazetini, basi huenda ikakwamisha shughuli zake.


CHANZO: MWANANCHI
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

KESI YA LEMA YAAHIRISHWA TENA



Na Woinde Shizza,Arusha

KESI ya kupinga matokeo ya ubunge wa Godbless Lema wa Jimbo la Arusha Mjini,imeahirishwa hadi Jumatatu ijayo baada ya mahakama hiyo kushindwa kuwasilisha nyaraka muhimu.

Akiahirisha kesi hiyo leo, Jaji Aloyce Mjulizi, alisema wakili wa walalamikiwa Method Kimomogoro,aliomba kupewa nakala ya uamuzi mdogo uliotupilia mbali pingamizi lililowekwa dhidi ya kesi hiyo.

Pia aliomba kupewa nakala ya mwenendo wa shauri hilo lakini hadi kesi hiyo inatajwa leo asubuhi upande wa walalamikiwa haukuwa umepata nakala hizo.

“Nathibitisha drafti na nakala ya mwenendo wa shauri la pingamizi ipo kwenye faili nilikabidhiwa leo,” alisema Jaji Mjulizi.

Katika uamuzi wake wa kuahirisha kesi, Jaji Mjulizi alimwagiza msajili wa mahakama kutoa nakala hizo kwa wadaiwa na wadai kabla ya kuanza kusilikiza kesi hiyo wiki ijayo.

Pia alimwagiza msajili wa wilaya kutoa taarifa ya shauri hilo kwa mujibu wa sheria na kubandika kwenye ubao wa matangazo mahakamani hapo na kuomba ukumbi mkubwa wa kusikilizia kesi hiyo kutokana na idadi kubwa ya watu wanaopenda kwenda kusikiliza.

Maagizo mengine aliyotoa ni kumtaka msajili kuweka utaratibu wa mwenendo wa shauri hilo kusikilizwa kwa vipaza sauti ili kuruhusu watu wengine watakaoshindwa kuingia ndani ya ukumbi waweze kusikiliza.

Jaji Mjulizi alitoa amri hizo baada ya wakili wa wadai Alute Mughwai,kuikumbushia mahakama hiyo kuhusu muda uliopangwa kusikiliza kesi hiyo hadi Desemba kuwa ni mdogo.

Kutokana na hali hiyo aliomba mahakama hiyo iandae utaratibu wa kuomba muda wa nyongeza, kutoa taarifa ya siku ya kesi kwenye ubao wa matangazo, na kesi hiyo isikilizwe kwenye ukumbi mkubwa zaidi.

“Hiki chumba hakifai kwa usikilizaji wa kesi hii, tumejazana na hewa haitoshi, inatakiwa ipande toka chini hadi kichwani,” alisema na kuongeza,“tunahitaji uwanja mpana wa kufanya kazi yetu.”

Pia Wakili Mughwai alilalamikia suala la usalama mahakamani hapo lakini wakati akitoa ombi hilo, sauti za kumsonya zilisikika kutoka kwa watu waliokuwa wamekaa nyuma yake.

“Mheshimiwa Jaji, unasikia jinsi ninavyosonywa, hii inaonyesha wanataka nisiseme na huu sio utaratibu wa kuendesha kesi mahakamani,” alisema.

Hata hivyo, Jaji Mjulizi alisema, “hawakusonyi wewe ila wanaisonya mahakama,” na baada ya kusema hivyo watu hao walisikika wakipiga makofi,lakini baadaye Jaji alionya kwamba anayesonya anaidharau mahakama.
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»