CAG alemewa kashfa ya UDA

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh (picha kutoka  Maktba).


Na Raymond Kaminyoge


MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh ameamua kukabidhi uchunguzi wa kashfa ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa Kampuni ya Kimataifa ya KPMG kutokana na ofisi yake kuwa na majukumu mengi.

Uamuzi huo wa CAG umekuja miezi mitatu tangu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika, kumtaka afanye kazi hiyo haraka.Mkuchika alimwandikia CAG barua hiyo Agosti 13, mwaka huu akimpa kipindi cha mwezi mmoja kufanya kazi hiyo.

Lakini, jana CAG aliliambia gazeti hili kwamba ameamua kukabidhi jukumu hilo kwa KPMG kutokana na ofisi yake kutingwa na mambo mengi na kuongeza kwamba, kampuni hiyo binafsi ilianza kazi hiyo tangu Ijumaa iliyopita na imepewa mwezi mmoja kuikamilisha.“Hiki ni kipindi cha ukaguzi, hivyo hatutakuwa na uwezo kufanya ukaguzi maalumu wa UDA na kuacha majukumu mengine,” alisema Utouh na kuongeza:

“Tukisema tuifanye kazi hiyo wenyewe, tutaichelewesha, ndiyo maana, tumeamua tuipe kampuni ya KPMG iifanye.” 

Utouh alisema kampuni hiyo imepewa hadidu za rejea za kufanya ukaguzi huo na kuongeza kwamba, ilishaandikiwa barua za utambulisho za kufanya ukaguzi UDA.

Bungeni   

Sakata la UDA liliibuka katika Mkutano wa Nne wa Bunge uliomalizika Agosti, mwaka huu baada ya wabunge kupinga kubinafsishwa kwa shirika hilo kwenda kwa Kampuni ya Simon Group.Baadhi ya wabunge waliwataja baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika na kutaka wawajibishwe kwa mujibu wa sheria, akiwamo waziri wa zamani, Iddi Simba.

Sakata hilo pia ndilo liliibua mvutano kati ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi na baadhi ya wabunge wa mkoa huo akidaiwa kuwashambulia kwa maneno makali. 



CHANZO:MWANANCHI