IGP, JWTZ wadaiwa sugu NHC


Mkurugenzi Mtendaji wa NHC, Nehemiah Mchechu




Waandishi Wetu
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limetangaza orodha ya taasisi 17 za Serikali na idara zake ambazo ni wadaiwa sugu huku Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ikiongoza kwa kudaiwa Sh586 milioni.Wadaiwa wanaofuatia katika orodha hiyo ya NHC ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambalo linadaiwa malimbikizo yanayofikia Sh247.4 milioni na Mkuu wa Jeshi la Polisi Sh42.8 milioni.

Mkurugenzi Mtendaji wa NHC, Nehemiah Mchechu aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwamba shirika lake linaidai Serikali na taasisi hizo 17 jumla ya Sh2.1bilioni na kutoa muda wa siku 60 deni hilo liwe limeshalipwa.

“Tumeamua kutoa siku 60 kwa hawa wadaiwa sugu kwani nina haki ya kuwaita wadaiwa sugu baada ya kukaa na madeni kwa muda mrefu bila kukumbuka kulipa,” alisema Mchechu na kuongeza kwamba NHC haigombani na Serikali, bali wateja wakorofi wasiolipa kodi za nyumba huku akielezea kushangazwa kwake na jinsi wadaiwa hao wanavyomudu majukumu mengine ya kiofisi kama warsha, safari na vitu vingine, lakini wakishindwa kulipia nyumba.

“Kila kitu kinafanyika katika ofisi zao na bajeti imetolewa, kwa nini wanashindwa kulipa kodi? Kila mtu anatakiwa kutimiza wajibu wake.”

Alisisitiza kuwa operesheni hiyo ya kuwataja na kuwaondoa katika nyumba zake ni endelevu. Hata hivyo, alisema shirika lake halitaendelea kutoa nje vyombo vya wapangaji, bali litazifunga ofisi za wadaiwa na kuweka walinzi kulinda majengo yake.

“Hatutachukua nyaraka zozote za Serikali katika ofisi hizo kwani ni kinyume na taratibu, ila kama wadaiwa wataendelea kukaa kimya baada ya kufungiwa ofisi hizo vyombo vitatolewa na vitapigwa mnada ili kulipia deni wanalodaiwa.”

Mchechu alisema shirika lake linapaswa kukusanya fedha hizo ili ziweze kuendeleza ujenzi wa nyumba nyingine mpya.

Wadaiwa sugu wengine
Katika orodha hiyo, Mchechu aliitaja Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, ambayo alisema inadaiwa Sh266.1 milioni. Nyingine ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii yenye deni la Sh325.3milioni, Wizara ya Fedha na Uchumi, Sh32.4 milioni wakati Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi inadaiwa Sh67.1 milioni.

Mchechu alisema Wizara ya Ujenzi ina deni la Sh23.8 milioni huku Wakala wa Majengo (TBA) wakidaiwa kiasi cha Sh67.4 milioni. Bodi ya Usajili wa Wahandisi inadaiwa Sh16.7milioni, Ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu (Tanga) inadaiwa Sh8.1 milioni Ofisi ya Rais Sh900,482.

Wengine ni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambayo inadaiwa malimbikizo ya Sh46.4milioni na Tume ya Utumishi wa Umma Sh23.3milioni.

Mkurugenzi huyo wa NHC alisema ukusanyaji huo wa madeni hautaishia serikalini pekee, bali hata watu binafsi, mashirika, taasisi za umma kwa kuzingatia taratibu zote za sheria.

Wizara ya Habari huru
Kuhusu Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo ambayo samani za Idara zake ikiwamo ile ya Habari (Maelezo) zilitolewa nje wiki iliyopita, Mchechu alisema imerudishiwa na kuendelea na kazi huku ikibakia na deni la Sh391,434,270.

Mchechu alisema Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), ndilo pekee ambalo halidaiwi kabisa kama ilivyo kwa wapangaji wengine wa NHC walioko chini ya wizara hiyo.

Polisi, JWTZ wanena
Akizungumzia deni hilo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema: “Ninachojua ni kwamba nyumba ya IGP imelipiwa hadi Juni mwakani.”

Senso alisema taarifa hizo za NHC si za kweli kwani mkuu huyo hana deni lolote... “Nyumba imelipiwa hadi mwakani, leo ni Oktoba. Waseme vizuri hizo taarifa zao zimetoka wapi? Kawaulize.”

Naye msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema jeshi halijapata taarifa rasmi za deni hilo lakini akaahidi kuwasiliana na uongozi wa juu ili kuhakikisha kwamba deni hilo lipo linalipwa.

Kanali Mgawe alisema JWTZ ina vitengo vingi vikiwamo vya ujenzi, hivyo siyo rahisi kufahamu mara moja kipi hasa kinachodaiwa.

Categories: