Jessca Nangawe
KIVUMBI cha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kinaendelea leo katika viwanja vitatu tofauti huku timu ngeni ya JKT Oljoro iksaka kukaa kileleni mwa ligi hiyo kwa mara ya kwanza msimu huu,
Kwenye Uwanja wa Chamazi uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, African Lyon watawakaribisha Kagera Sugar huku Coastal Union wakiwa wenyeji wa Villa Squad mjini Tanga.
Lakini, kivutio kitakuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha ambako maafande wa JKT Oljoro watakuwa na kibarua kikali dhidi ya Moro United, ambayo pia imepanda daraja msimu huu.
Ligi hiyo hata hivyo imesimama kwa muda kwa timu za Simba,Yanga na Azam ili kupisha timu ya taifa 'Taifa Stars' iliyopo Morocco ambako kesho itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya wenyeji wao kuwania tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za Mataifa Mataifa ya Afrika mwakani.
Mechi za leo kwa kila timu zina umuhimu na zenye ushindani mkubwa kufuatia kila moja kutaka pointi tatu muhimu za kuendelea kujitengenezea mazingira mazuri katika msimamo wa ligi kuu.
Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, JKT Oljoro wenye pointi 16 wakiwa nyuma ya vinara wa ligi hiyo, Simba kwa pointi mbili wanasaka kupanda kileleni.
Oljoro kwa sasa wanaonekana kucheza soka la ushindani mkubwa huku wakikamata nafasi ya pili, leo wanasaka nafasi ya kuishusha Simba kileleni kwa kuhakikisha wanatumia vyema uwanja wao wa nyumbani kwa kuiondoa Moro United.
Kwa upande wa kocha mkuu wa timu hiyo, Ally Mohamed 'Chidi' aliiambia Mwananchi jana kwa simu kutoka Arusha kuwa matokeo mazuri katika mchezo wao wa leo yataendelea kuwaweka vizuri katika nafasi ya kupanda juu na kuahidi kutumia vyema uwanja wao wa myumbani kwa kuwafunga wapinzani wao.
"Hatudharau mchezo hata mmoja kwani kila mmoja amejiandaa na anajitafutia nafasi ya kusonga mbele zaidi,tunafahamu ligi ni ngumu na yenye ushindani mkubwa, lakini napenda kuwaambia wapinzani wetu (Moro United) kwamba wategemee kichapo toka kwetu kwani tumejipanga kuhakikisha tunashinda,"alisema Chidi.
Kwa upande wake, Hassan Banyai ambaye ni kocha wa Moro united yenye pointi10 kibindoni mpaka sasa alisema licha ya timu yake kuwa ugenini wamejipanga kufanya vizuri katika mchezo huo na kuahidi kutoka na ushindi.
Naye kocha mkuu wa African Lyon yenye pointi tisa, Jumanne Chale ambaye timu yake itakabiliana na Kagera Sugar wenye pointi nane, makocha wa timu zote mbili kila mmoja amemtambia mwenzake na kudai kuwa ushindi ni wake na kueleza kuwa wamejipanga vyema na kuhakikisha wanafanya vizuri.
"Tutakuwa ugenini, lakini si sababu ya kufungwa kwa wachezaji wangu licha ya wengine kuwa mejeruhi, lakini ni imani yetu maandalizi tuliyofanya yanatupa imani kubwa ya ushindi,"alisema Mrage Kabange ambaye ni kocha msaizidi wa Kagera Sugar.
Nako kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, vibonde wa ligi hiyo Coastal Union wenye pointi nne nao watakutana na vibonde wenzao, Villa wenye pointi sita katika kuwania pointi tatu muhimu.
Huo utakuwa mtihani wa kwanza wa kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio' ambaye amekabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo ambayo mwenendo wake hauridhishi katika ligi hiyo.
CHANZO: MWANANCHI
Categories: