Imeandikwa na Arnold Swai, Moshi
WATU wawili wamekufa mkoani Kilimanjaro katika matukio mawili tofauti, likiwemo la kijana mmoja aliyetambulika kwa jina la Yunis Diana (24), kukutwa chumbani kwake akiwa amejichinja shingoni hadi kufa.
Akizungumzia matukio hayo jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Yusuph Ilembo alisema kijana huyo alikutwa amejichinja Oktoba 24 saa saba mchana katika eneo la Njoro Sokoni katika Manispaa ya Moshi.
Alisema kuwa tukio hilo liligundulika baada ya mama mzazi wa kijana huyo, Sion Parasala (54) kurejea nyumbani akitokea katika shughuli zake, na kukuta mlango wa chumba cha binti yake ukiwa umefungwa.
Kamanda Ilembo alisema mama mzazi huyo alimwita binti yake bila mafanikio ndipo alipowaeleza majirani na kuuvunja mlango, ambapo walimkuta Yunis amekufa baada ya kujichinja na kisu kwenye koo huku damu nyingi zikiwa zimetapakaa ndani.
Kwa mujibu wa maelezo ya Sion kwa Polisi, Yunis alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili tangu mwaka 2006.
Kaimu Kamanda Ilembo alisema kuwa katika tukio lingine mtoto mchanga aliyetambulika kwa jina la Hadija Ngwangwa wa mwaka mmoja na nusu, alikufa baada ya chumba alichokuwa amelala kuungua kwa moto.
Alisema kuwa ajali hiyo ilitokea saa tano mchana katika eneo la Majengo Kwamtei Manispaa ya Moshi, wakati kichanga huyo akiwa amelala, baada ya kuachwa ndani na bibi yake, Maimuna Abdi (55).
Kamanda Ilembo alisema Maimuna anayeishi na kichanga huyo alikuwa ameenda dukani kupata mahitaji yake ya nyumbani na aliporejea alikuta chumba alichokuwa amelala mjukuu wake kikiwaka moto.
Kutokana na moto huo, Kamanda Ilembo alisema juhudi za kumuokoa akiwa mzima zilifanyika lakini zilishindikana baada ya kuzidiwa nguvu.
Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana kutokana na nyumba hiyo kutokuwa na umeme na Polisi inamshikilia Maimuna kwa ajili ya kumchunguza kama alihusika na tukio hilo.