Kikongwe afa kwa kukatwa jembe kichwani

Na Stella Ibengwe, Shinyanga


MKAZI wa Kijiji cha Ushirika wilayani Bukombe, Mkoa wa Shinyanga, Paschal Matonange (75), ameuawa kikatili baada ya kukatwa jembe kichwani na mtu anayehisiwa kuwa ni mgonjwa wa akili.
  Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 2 asubuhi nyumbani kwa Constantine Bundala na kwamba chanzo cha mauaji hayo  hakikuweza kujulikana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athuman, alithibitisha kutokea kifo hicho akisema kuwa kikongwe huyo  alikatwa panga kichwani na kijana mmoja anayesadikiwa kuwa na ugonjwa wa akili, William Bundala, maarufu kama “Ngoma” (45) mkazi wa Kijiji hicho na kufariki dunia papo hapo.
Kutokana na tukio hilo, Polisi inafanya utaratibu wa kumpeleka mtuhumiwa kwa wataalamu kuweza kuthibitisha kama kweli ana tatizo la ugonjwa wa akili na baada ya uchunguzi huo atafikishwa mahakamani kujibu shitaka la mauaji.
 Katika tukio jingine, Polisi imefanikiwa kuyategua mabomu mawili ya kivita yaliyokuwa yamezikwa ardhini, yaliyogunduliwa na bibi kizee mmoja wa miaka 80, aliyekuwa akilima shambani kwake na kubaini vitu asivyovifahamu vikiwa vimezikwa ardhini, hivyo kutoa taarifa.
 Kamanda huyo alisema kuwa mabomu hayo yaligunduliwa na kikongwe huyo, Christina Sizya, katika Kijiji cha Kanembwa, Wilaya ya Bukombe, mkoani hapa.
Alisema  Jeshi la Polisi kwa  kushirikiana na wataalamu wa kutegua mabomu wanafanya jitihada za kuyaharibu  mabomu hayo ili yasilete madhara katika jamii na kutoa mwito kwa wananchi kutoa taarifa ikiwa wataona kitu chochote chenye asili ya chuma ambacho wanakitilia shaka.

Categories: