Magari 1,413 yabainika kuwa mabovu Dar

Na Nasra Abdallah



MAGARI 1,413 kati ya 23,489 yaliyokaguliwa jijini Dar es Salaam yamegundulika kuwa ni mabovu wakati wa ukaguzi uliofanyika katika maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani kuanzia Septemba 26 mwaka huu.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Jordan Rugimbana, katika risala yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Bernad Marcelline, wakati wa kufunga maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani yaliyofikia kilele chake kwenye viwanja vya Mashujaa jijini hapa.
Rugimbana alisema kati ya magari hayo yaliyokaguliwa 22,076 ndiyo yaliyoonekana kuwa mazima na yalipewa stika, huku wale wenye magari mabovu wakitakiwa kuyatengeneza na kuyarudisha kwa ukaguzi kabla ya kuruhusiwa kuendeshwa barabarani.
Halikadhalika katika kipindi cha maadhimisho hayo, magari 7,413 yalikaguliwa na kati yake magari 7,114 yalionekana mazima huku 299 yakibainika kuwa mabovu.
Kutokana na takwimu hizo, Rugimbana alisema iko kazi kubwa ya kuhakikisha magari yanakaguliwa kwa idadi ya kutosha na iwe kazi endelevu ukizingatia kwamba Mkoa wa Dar es Salaam pekee unakadiriwa kuwa na takriban magari 600,000.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani Mkoa wa Dar es Salaam, Jerome Ringo, alisema ajali za barabrani zitaweza kupungua kwa kiasi kikubwa kama kila mmoja atakuwa makini atumiapo barabara.
Hata hivyo, Ringo alizitaja baadhi ya changamoto ambazo Jiji la Dar es Salaam limekuwa likikabiliana nalo katika sekta ya usafiri kuwa ni pamoja na tabia za madereva kukatisha ruti na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria na wanafunzi na mara nyingine kulazimika kulipa nauli zaidi ya iliyowekwa kisheria.

Categories: