Robert Kakwesi,Tabora
WABUNGE wawili wa Chadema,Sylvester Kasulumbayi na Susan Kiwanga pamoja na mwenzao mmoja wamepewa onyo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora kuwa watafutiwa dhamana endapo hawataonekana mahakamni tarehe 24 mwezi huu.
Onyo hilo limetolewa na hakimu mkazi mfawidhi Tabora,Thomas Simba mara baada ya upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Musa Kwikima kudai kuwa washtakiwa hao watatu walikuwa na hudhuru maalum iliyowafanya wasifike mahakamani hapo
Wakili Kwikima alieleza mahakama kuwa wabunge hao wawili walikuwa katika vikao vya kamati za Bunge huku mshtakiwa wa tatu Anwar Kashaga kuwa amelazwa Hospitali ya Bugando ndiyo maana hawakuweza kuhudhuria mahakamani.Upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali Mugisha Mboneko ulidai kuwa hoja zilizotolewa na upande wa utetezi ni dhaifu na hazina nguvu kisheria.
Aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa anayedaiwa anaumwa na amelazwa Bugando, Anwar Kashaga hakuwakilisha vyeti vya Hopitali ya Bugando kuwa anaumwa na amelazwa huku wabunge wakiwa hawana barua kama wapo kwenye vikao na kuitaka mahakama kuwafutia dhamana washtakiwa na wakamatwe.
Hakimu Simba baada ya maelezo ya pande zote mbili aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 24 mwezi huu lakini alitoa onyo kuwa washtakiwa wasipofika mahakamani tarehe hiyo mahakama itawafutia dhamana.
Upande wa mashtaka ulimuongeza mshtakiwa mwingine aitwaye Robert William akikabiliwa na mashtaka matatu kama washtakiwa wa pili na wa tatu na kufanya jumla ya washtakiwa kufikia wanne.Mshtakiwa huyo alipelekwa rumande baada ya kushindwa masharti ya dhamana ambapo aliongezwa hadi tarehe 24 mwezi huu.
Washtakiwa wa pili hadi wa nne wanakabiliwa na mashtaka matatu la kwanza likiwa shambulio la kawaida,pili likiwa la kumuweka chini ya ulinzi pasipo halali Fatuma Kimario ambaye ni mkuu wa wilaya ya Igunga na la nne ni shambulio la maungoni ambapo wanadaiwa kuiba simu yenye thamani ya shilingi laki nne na wote walikana mashtaka na wapo nje kwa dhamana isipokuwa Robert William.
Categories: