Matokeo Igunga: Chadema wanatembea kifua mbele


Dr Benson Bana

*Nguvu za CCM hazifanani na kura zake
*IGP Mwema naye azungumzia yaliyojiri

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, amesema idadi ya kura kilizopata Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga.
Mkoani Tabora, Jumapili iliyopita inaashiria kwamba, kinazidi kukubalika na hivyo uwezekano kwa chama hicho kuunda serikali katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015, ni mkubwa.
Dk. Bana, ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, alisema hayo jana alipozungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum akitoa tathmini kuhusu uchaguzi huo uliofanyika Jumapili wiki iliyopita.
Katika uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Dallaly Kafumu aliibuka mshindi.
Dk. Kafumu alishinda uchaguzi huo, baada ya kujizolea kura 26,484 sawa na asilimia 50.56.
Aliyekuwa mgombea kupitia Chadema, Joseph Kashindye, alipata kura 23,260 sawa na asilimia 44.32, huku aliyekuwa mgombea wa CUF, Leopard Mahona, akiambulia kura 2,104 sawa na asilimia 4.01.
Hata hivyo, Kashindye alikataa kusaini fomu ya matokeo hayo baada ya kuona idadi ya kura alizopata.
Wagombea wengine walikuwa ni Stephen Mahui wa Chama cha AFP (kura 235), Hassan Lutegeza wa Chausta (183), Said Cheni wa DP (kura 76), John Maguma wa Sau (kura 83) na Hemed Dedu wa UPDP (kura 63).
“Chadema wanatembea kifua mbele kwa sababu kura walizopata (katika uchaguzi huo) hazikutarajiwa,” alisema Dk. Bana, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Mpango wa Utafiti wa Elimu ya Demokrasia (Redet).
Aliongeza: “Hiyo ni ishara kwamba, Chadema inaendelea kukubaliwa zaidi na CCM inazidi kushuka. Hivyo, Chadema katika uchaguzi ujao uwezekano wa kuunda serikali ijayo ni mkubwa.”
Alisema kutokana na matokeo hayo, Chadema kinastahili kutembea kifua mbele kutokana na kura kilizozipata ambazo hazikutarajiwa.
Alisema uchaguzi huo ulikuwa mzuri na uliendeshwa kwa mujibu wa sheria japokuwa rabsha za hapa na pale zilijitokeza.
Hata hivyo, alisema matokeo ya uchaguzi huo yanapaswa kutafakariwa kwa kina, hasa nguvu kubwa na rasilimali nyingi zilizotumiwa na CCM kutowiana na kura walizovuna.
Alisema iwapo CCM wangeshindwa katika uchaguzi huo, kiu ya sekretarieti ya chama hicho chini ya Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama, ya kuona chama hicho kinajivua gamba, ingekuwa hatarini.
“Hivyo, kwa ushindi huo, sasa sekretarieti wanaweza kutembea kifua mbele,” alisema Dk. Bana.
Alisema jambo lingine la kutafakari katika uchaguzi huo, ni watu wachache kujitokeza kupiga kura.
Wapigakura walioandikishwa katika Jimbo la Igunga ni 171,019, lakini waliojitokeza kupiga kura ni 53,692 sawa na asilimia 31.3. Dk. Bana alisema hali hiyo ni mbaya na ni changamoto kwa wanademokrasia wote kwa siku za baadaye.
Alisema jambo lingine ni kampeni zilizoambatana na fujo, ambazo ziliutia dosari uchaguzi huo.
Kutokana na hilo, aliwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kuwaheshimu viongozi akisema kuwa uchaguzi wa Igunga umemuacha Mkuu wa Wilaya hiyo akiwa amevunjiwa heshima.
“Kiongozi wa serikali alichofanyiwa kwa kweli si kitu kizuri. Viongozi wetu yafaa tuwaheshimu. DC Igunga hakuheshimiwa,” alisema Dk. Bana.
Aliongeza: “Chadema baada ya uchaguzi kwisha wangeenda kumuomba radhi DC huyo. Jambo hilo lilitokea kisiasa, hatuwezi kuliacha.”
IGP MWEMA: TOFAUTI ZA ITIKADI ZISITUGAWE
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, amewataka wananchi kuendeleza amani nchini na kwamba changamoto ambazo zimetokea katika kipindi cha uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga, zimesababishwa na tofauti za kiitikadi.
IGP Mwema alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema licha ya kuwepo kwa changamoto hizo, uchaguzi ulifanyika kwa amani.
Mwema alisema tofauti za kiitikadi zisiwe ni chanzo cha kupoteza amani na kwamba kama kutakuwa kuna tatizo lolote wanachotakiwa kukifanya ni kufuata sheria na sio vinginevyo.
“Kama kuna tatizo wanachotakiwa ni kufuata sheria kwani tofauti za kiitikadi isiwe ni chanzo za kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani,” alisema Mwema.
Hata hivyo, alisema uvumilivu pamoja na subira katika kipindi cha kampeni na uchaguzi, vimeonyesha kuwa kuna ukomavu wa kidemokrasia nchini.
Alisema uchaguzi umeisha na kinachotakiwa ni kufuata utaratibu na sheria kwani hakuna haki isiyokuwa na wajibu wala uhuru usio na mpaka.
Aidha, IGP Mwema alisema kama wananchi watatii sheria bila kushurutishwa, watakomaza demokrasia nchini na vijana wanatakiwa kujiepusha na vitendo vyenye dalili ya uvunjifu wa amani.
Mwema alilipongeza Jeshi la Polisi na wananchi kwa kumaliza zoezi la uchaguzi kwa amani bila kuwapo kwa vurugu.
CHANZO: NIPASHE

Categories: