Mbunge atimua mbio kuwakimbia polisi



Moses Mashalla na Peter Saramba, Arusha

MBUNGE wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema jana alilazimika kutimua mbio kujinusuru kukamatwa na polisi baada ya kutoka mahakamani kusikiliza kesi ya kupinga ubunge wake.Lema alilazimika kukimbia baada ya polisi kuwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa katika ofisi za mbunge huyo, wakisikiliza hotuba yake muda mfupi baada ya kuwasili kutoka mahakamani.

Baadhi ya wafuasi hao ambao walitoka katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwa maandamano hadi kwenye ofisi za Lema, walikamatwa na polisi katika patashika iliyodumu kwa dakika kadhaa.

Wafuasi hao walitoka katika mahakama hiyo kwa maandamano huku wakiimba nyimbo za hamasa na walipofika eneo la Barabara ya Boma walikutana na polisi ambao waliwataka kutoendelea na maandamano yao lakini wakakaidi amri hiyo.

Zaidi ya magari matano yaliyosheheni askari zaidi ya 50 wakiwa na silaha walijaribu kuwazuia wafuasi hao ambao pia walikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali bila mafanikio hadi walipowasili katika ofisi za mbunge.

Mara baada ya kufika hapo, Lema alianza kuwahutubia wafuasi hao akiwataka kamwe wasiwaogope polisi kwa kuwa wao wamewekwa kuhakikisha ulinzi wa raia ambao ndiyo ni wao.

“Msiwaogope polisi. Hawa wamewekwa kwa ajili ya kuwalinda nyie hivyo teteeni haki yenu bila woga,” alisema Lema.

Wakati akiendelea kuhutubia ghafla gari la polisi likiwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD), Zuberi Mwombeji lilifika eneo hilo la mkutano, kisha polisi kadhaa  kushuka na kuanza kuwatawanya wafuasi hao.

Baadhi ya wafuasi hao walipigwa virungu na kushambuliwa kwa mateke huku wengine wakikamatwa na kusekwa ndani ya magari ya polisi. Kuona hivyo, Lema alitimua mbio.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya magari yaliyokuwa yakipita Barabara ya Makongoro kuelekea Barabara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na ile ya Boma kushindwa kufanya safari zake kama kawaida.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa hakuwa tayari kutoa taarifa za tukio hilo kwa maelezo kwamba zilikuwa bado hazijamfikia.

Kwa upande wake, Lema alilaani hatua hiyo ya polisi huku akieleza kushangazwa na hatua ya askari hao kuwatawanya wafuasi wake na kuwashikilia baadhi yao.

Alidai kwamba polisi walivamia ofisi yake kwa nguvu na kutaka kuvunja mlango kwa lengo la kumkamata pamoja na wafuasi wake bila mafanikio.

Mahakamani

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imetoa hati ya kuitwa mahakamani hapo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na Mhariri wa Gazeti la Nipashe kwa maelezo kwamba waliingilia mwenendo wa kesi ya Lema.

Nape na mhariri huyo wanapaswa kufika mahakamani hapo, Novemba 16 mwaka huu.

Wito huo unatokana na hoja ya Wakili wa Lema, Method Kimomogoro aliyesema kwamba upande wa utetezi hauna imani na Jaji anayesikiliza shauri hilo, Aloyce Mujulizi kutokana  na matamshi  yaliyotolewa na Nape na kunukuliwa na Gazeti la Nipashe.

Wakili huyo alisema matamshi ya kiongozi huyo wa CCM yanaashiria kuwapo kwa njama za walalamikaji kushinda kesi hiyo isivyo halali.

Akiahirisha kesi hiyo jana, Jaji Mujulizi alikubaliana na hoja za Kimomogoro za kuitwa mahakamani hapo watu hao wawili na kwamba Nape anatakiwa aieleze mahakama hiyo juu ya matamshi yake yaliyonukuliwa na Nipashe toleo la Oktoba 9, mwaka huu.

Alisema mhariri wa gazeti hilo anapaswa kufika mahakamani ili kutoa uthibitisho juu ya matamshi aliyotoa Nape kupitia gazeti lake.

Mapema Kimomogoro aliieleza mahakama hiyo ya kuwa kitendo cha Nape kutoa matamshi yanayoashiria kuharibu mwenendo wa kesi hiyo ni kosa na kwamba kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa mahakama.

Wakili huyo alisema sehemu ya habari hiyo ilisema: “Nnauye alisema kwa sasa wako katika mchakato wa kwenda kupiga kambi katika Mkoa wa Arusha ili waweze kulichukua jimbo hilo. Alisema wana uhakika wa kushinda kesi yao dhidi ya Lema na kulichukua jimbo hilo uchaguzi utakapofanyika.”

Kimomgoro alisema matamshi hayo hayajawahi kukanushwa hadharani na kusisitiza ya kuwa mteja wake ambaye ni Lema, Chadema pamoja na wafuasi wa chama hicho wana shaka na kauli hiyo.

Hata hivyo, maelezo hayo yalipingwa na wakili wa walalamikaji, Alute Mughai ambaye alisema hizo zilikuwa mbinu za kuchelewesha kesi.

Kuhusu hoja ya kauli iliyotolewa na Nape, Wakili Mughai alisema mahakama hiyo haiwezi kusikiliza mambo yote yanayoandikwa kwenye magazeti hapa nchini huku akitoa onyo ya kuwa endapo mahakama hiyo itakuwa ikisikiliza mambo ya magazetini, basi huenda ikakwamisha shughuli zake.


CHANZO: MWANANCHI

Categories: ,