Mgombea wa CCM agonga mwamba kortini

Ramadhani Madabida


Mwanja Ibadi, Kilwa

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, imetupilia mbali kesi iliyokuwa imefunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti cha ubunge wa Jimbo la Kilwa Kusini kupitia tiketi ya CCM, Ramadhani Madabida ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi, Selemani Bungara Bwege wa CUF.Uamuzi huo umekuja baada ya mahakama kutoridhishwa na madai ya mlalamikaji katika kesi hiyo kuwa uchaguzi haukuwa wa haki na kwamba ulitawaliwa na vitendo vya wizi wa kura.

Madabida alidai kuwa wizi huo ulichangiwa na kukatika kwa umeme katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.Madabida pia alidai kuwa baadhi ya wapigakura wake halali, walizuiwa kupiga kura na kwamba katika kampeni zake, Bungara alidai kuwa yeye (Madabida) si mzawa wa jimbo hilo na kwa hiyo hastahili kuchagulia kuwa mbunge.

Akitoa hukumu ya kesi hiyo katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, Jaji Fatuma Massengi, alisema baada ya kupitia ushahidi, amejiridhisha kuwa madai ya Madabida hayana msingi.

Alisema kwa msingi huo, mahakama imetupilia mbali kesi hiyo na kumtambua Bungara kuwa mbunge halali wa Jimbo la Kilwa Kusini.Jaji huyo pia alimwamuru mlalamikaji kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo.

Hata hivyo alisema mlalamikaji yuko huru kukataa rufaa katika mahakama ya juu, kama atahisi kuwa hakutendewa haki.Baada ya hukumu hiyo, wanachama, washabiki na wapenzi wa CUF,) walioonyesha vituko vilivyoambatana na maandamano huku wakiwa kutembeza jeneza la kuzikia walilodai kuwa ni kifo cha CCM, katika jimbo hilo.

Kwa upande wae, Bunga alitokwa na machozi ya furaha baada ya kutangazwa kuwa ni mbunge halali wa Kilwa Kusini.Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Septemba 19 na kumalizika Oktoba 13 mwaka huu, ilikuwa na mashahidi 39.

Mashahidi 20 kati hao walikuwa wa upande mlalamikaji na 19 wengine walikuwa wa upande wa mlalamikiwa,

Categories: ,