NAFASI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI KATIKA MIKATABA YA NCHI IPEWE UZITO - CHEYO



Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Bw George Masaju (katikati) Mkurugenzi wa Mipango (Kushoto) na Mkurugenzi wa Rasilimali watu wakitoka kwenye kikao hicho.
Baadhi ya Wajumbe kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwa katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali.


********


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Mh.John Momose Cheyo ametoa wito kwa Wizara,Idara,Taasisi na Mashirika ya umma kufuata na kutekeleza Sheria ya Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali {The Office of the Attorney General(Discharge of Duties)Act} Namba 4 ya mwaka 2005 ili kuhakikisha kuwa Serikali inadhibiti hasara kubwa inayotokana na kuingia Mikataba mibovu.

Wito huo umetolewa wakati wa Kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kilichofanyika tarehe 26 Octoba 2011 katiba Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam ambapo utekelezaji wa Bajeti na Mpango wa mwaka wa fedha 2008/2009 wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ulijadiliwa.

Aidha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imetakiwa kuchukua hatua madhubuti juu ya usimamizi na utekelezaji wa Sheria hiyo ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha makatibu Wakuu wote wa Idara za Serikali kuzingatia maelekezo ya Sheria hiyo ili kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali kutokana na kuingia mikataba ambayo haina manufaa kwa walipa kodi.

Akifafanua suala hilo Mh.Cheyo amesema Kuwa Serikali haihitaji kuwa na Sheria nyingine ili kudhibiti uingiaji wa Mikataba mibovu kwa kuwa Sheria inaelekeza kuwa endapo Idara au Taasisi yoyote ya Serikali itakiuka ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mikataba wachkuliwe hatua ikiwa ni pamoja na kufunguliwa Mashtaka ili waweze kujibu namna amabvyo wametumia vibaya fedha na rasilimali za Watanzania.

Akitoa maelezo katika hatua ambazo Serikali imechukua ili kudhibiti mikataba mibovu, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Mcheche Masaju,ameileza kamati hiyo kuwa tatizo kubwa lipo katika utaalamu ambapo suala la Mafunzo ya mikataba limekuwa halipewi kipaumbele kwa muda mrefu na hivyo kuathiri utendaji kazi wa Mawakili wanaoshughulika na utekelezaji wa jukumu hilo. 

Ili kushughulika suala hili Ofisi imekuwa ikiwakengea uwezo Mawakili wa Serikali kwa kuwapatiwa mafunzo ili katika kuhakiki mikataba ya aina mbalimbali kwa ufanisi. Pamoja na hatua hizo,Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliieleza kamati hiyo kuwa

Ofisi imeanzisha Divisheni mpya kuanzia Juni,2011 ambayo itakuwa ikishughulika na masuala ya Mikataba pekee ili kuhakikisha kuwa mikataba inaandikwa katika kiwango kinachotakiwa.

Kwa upande mwingine,Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imepewa changamoto katika kuongeza kasi ya kufungua na kuendesha Mashauri ya watu wenye ulemavu wa ngozi ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa haraka zaidi.

Akifunga kikao hicho cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ,Mh Cheyo ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwa na hati safi na kusisitiza kuwa itekeleze Majukumu yake kwa ufasaha na ufanisi zaidi ili kuhakikisha kuwa walipa kodi wanapata huduma kulingana na thamani ya kodi zao.

Categories: ,