![]() |
Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya |
Na Mussa Juma, Arusha
WAZIRI wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, anatarajia kurejea nchini Novemba 8, mwaka huu baada ya hali ya afya yake kuimarika nchini India anakopatiwa matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa kimataifa wa wadau wa Rabobank's mjini hapa jana, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Samuel Sitta, alisema aliwasiliana na Profesa Mwandosya juzi na kumweleza kuwa, afya yake inaimarika tofauti na uvumi ambao unaendelea.
"Kuna maneno mengi kuhusiana na Profesa Mwandosya na Dk Mwakyembe kutokana na kupata maradhi, lakini kikubwa hapa afya zao zimeimarika na nimewasiliana na Profesa Mwandosya atarejea Novemba 8, kabla ya kurejea tena kwenye matibabu Januari mwakani," alisema Sitta.
Sitta alikuwa akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari kuhusiana na kuonekana kuanza kupungua nguvu kundi la wanachama wa CCM ambao wanapiga vita ufisadi.
Hata hivyo, Waziri Sitta alisema hivi sasa vita dhidi ya ufisadi haipiganwi na viongozi wachache pekee, bali kuna wananchi wengi wakiwamo wanaoishi vijijini.
"Vita hii ya ufisadi hatupigani peke yetu, wapo wengi. Tunawasiliana na ingekuwa tupo wachache tusingefika hapa," alisema Waziri Sitta.
Alisema haiwezekani nchi kuachwa mikononi mwa watu wachache waendelee kubomoa urithi wa taifa kutokana na kutaka kuhodhi utajiri na mamlaka.
Waziri Sitta alisema kama ambavyo amekuwa akunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari, vita dhidi ya ufisadi ni endelevu na itakoma pale watuhumiwa watakapowajibika kwa makosa yao.
Categories:
ccm,
prof mwandosya