Na Richard Makore
Sakata la Dowans limegeuka baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kumeipa Serikali siku 30 kuanzia jana kusitisha mpango wake wa kutaka kuilipa kampuni ya Dowans Sh. bilioni 94.
Kimesema baada ya muda huo kupita bila hatua kuchukuliwa, kitaitisha maandamano makubwa yatakayotumia staili ambayo haijawahi kutumika hapa nchini na kushirikisha wananchi wote.
Kadhalika, chama hicho kimesema ikiwa Rais Jakaya Kikwete hatachukua hatua za kuzuia mpango huo wa Serikali wa kutaka kuilipa Dowans asije akakilaumu Chadema kutokana na maamuzi magumu kitakayoyafanya kwa kushirikiana na wananchi bila kujali itikadi za vyama vyao.
Chadema kimesema fedha hizo ni za Watanzania hivyo kitawaambia wananchi wasikubali kulipa deni lililotokana na uzembe na ufisadi wa watu wachache ambao wengi wao bado wapo katika Serikali ya Rais Kikwete.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika alitoa ujumbe huo jana alipokutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Kwa niaba ya Chadema nasema Rais Kikwete lazima achuke hatua za haraka kuzuia ulipaji wa fedha hizo vinginevyo sisi tutakwenda kwa wananchi kuishtaki serikali,” alisema Mnyika.
Alisema kama Serikali ina hamu na huruma ya kutaka kuilipa Dowans ikamate mali za mafisadi walioingia mkataba wa kifisadi na kuziuza lakini sio kutumia fedha za Watanzania.
Mnyika alisema walimu hapa nchini wanaidai Serikali sh. bilioni 29, wazee wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mpaka leo hawajalipwa, wanafunzi wa vyuo vikuu wapatao 14,000 wamekosa mikopo lakini anashangaa serikali kuonyesha uharaka na hamu ya kutaka kulipa deni hilo.
Aliweka wazi kuwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Dk. Idrisa Rashid wawe watu wa kwanza kukamatiwa mali zao na kuziuza kwa kuwa walihusika na kuingia mkataba mbovu wa Richmond ambao mwishoni ulizaa Dowans.
“Safari hii Chadema hakitakuwa na mzaha wala kuogopa badala yake tutawashawishi wananchi wote wa mijini na vijijini ili waamke na kukataa dhuluma inayotaka kufanywa na serikali hii,” alisema Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam kupitia Chadema.
Mwishoni mwa mwezi uliopita Mahakama Kuu ilisajili hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) iliyofunguliwa na kampuni ya kufua umeme ya Dowans (T) Ltd.
Mahakama hiyo Kanda ya Dar es Salaam ilikubali kusajili Tuzo ya ICC ya malipo ya fidia ya mabilioni ya fedha kwa kampuni ya Dowans.
Kwa mujibu wa uamuzi huo wa jana, Tanesco sasa italazimika kulipa sh bilioni 94 kwa Dowans.
Akisoma uamuzi huo uliochukua zaidi ya saa tatu, Jaji wa Mahakama hiyo, Emilian Mushi, alisema mbali na tuzo hiyo kusajiliwa, Tanesco italazimika kulipa pia gharama za usikilizwaji wa shauri hilo.
Katika uamuzi wake Jaji Mushi alisema Tanesco ilikuwa na sababu 12 ilizowasilisha mahakamani kuomba tuzo hiyo isisajiliwe, lakini alizipitia na kuona kuwa Mahakama yake haina uwezo wa kuingilia uamuzi wa ICC kwa sababu Tanesco ilijifunga yenyewe katika mkataba ilioingia na Dowans.
Alisema katika mkataba huo, walikubaliana kuwa msuluhishi wao wa mwisho atakuwa mahakama hiyo pekee na haitaingiliwa na chombo kingine chochote cha sheria katika kufanya makubaliano kati yao.
Aidha, alisema mkataba huo pia ulisema wazi kuwa hawatakata rufaa na mshindi atatakiwa kulipwa mara moja.
Jaji Mushi alisema kwa makubaliano hayo kwenye mkataba, Mahakama yake imefungwa mikono kuingilia uamuzi wa ICC.
Dowans iliwasilisha maombi Mahakama Kuu hiyo Dar es Salaam ikiomba tuzo yake ya malipo ya fidia ya sh bilioni 94 dhidi ya Tanesco iliyotolewa ICC isajiliwe .
Novemba 15, mwaka jana, ICC chini ya uenyekiti wa Gerald Aksen akisaidiwa na wasuluhishi, Swithin Munyantwali na Jonathan Parker, iliiamuru Tanesco iilipe Dowans fidia hiyo ya mabilioni ya fedha kwa kuvunja mkataba baina yake na kampuni hiyo kinyume cha sheria.
Hata hivyo, Dowans ilifungua maombi mengine ya utekelezaji wa hukumu hiyo ya ICC katika Mahakama Kuu ya Uingereza.
Uamuzi huo ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu na wananchi ambao wengi walipinga kulipwa kwa fedha hizo wakiamini kuwa wamiliki halali wa kampuni hiyo bado wana utata.
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema hukumu hiyo inaitaka Tanesco kuilipa Dowans Tanzania Limited dola za Marekani 65,812,630 (sh bilioni 94) zikiwa ni fidia ya kuvunjiwa mkataba wake.
Ngeleja alisema malipo ya fidia hiyo yangetekelezwa iwapo tu hukumu hiyo ingesajiliwa katika Mahakama ya Tanzania, hatua ambayo imeishafanyika.
Dowans Tanzania Limited ilirithi mkataba huo kutoka Dowans Holdings SA (Costa Rica), ambayo nayo iliachiwa na kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond Development LLC, Desemba 2006.
Awali, Richmond iliingia mkataba huo na Tanesco kwa ajili ya mauziano ya umeme Juni, 2006.
Hata hivyo, wakati utekelezaji wa mkataba ukiendelea, ilizuka hoja kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwamo wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba, haukuwa halali kisheria.
Mashirika 17 yasiyokuwa ya kiserikali yalijitokeza kufungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kuitaka ikatae kusajili hukumu ya ICC ili kuzuia malipo hayo kufanyika kwa Dowans. Hata hivyo, hali hiyo imekuja kinyume cha matakwa ya mashirika hayo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Categories: