SAKATA la kusafirisha sukari nje ya nchi kwa njia ya magendo limechukua sura mpya baada ya serikali kuyafutia leseni makampuni matatu yanayonunua sukari katika kiwanda cha sukari cha TPC na kutangaza kutaifisha magari yatakayokamatwa na sukari ya magendo. Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Moshi, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, alisema uamuzi wa kufuta leseni za makampuni hayo (majina yamehifadhiwa kwa sasa) umetokana na hatua ya wasambazaji hao kukaidi agizo la serikali na kuendelea kuuza bidhaa hiyo nje ya nchi. Profesa Maghembe alisema pamoja na serikali kukutana na wadau wa sukari mwezi uliopita na kukubaliana bei ya sukari iuzwe kwa sh 1,800 hadi 1,900, bado wamekiuka agizo hilo na bei ya sukari imepanda kufikia sh 2,500 katika maeneo mengi ya nchi. Waziri huyo alionya kuwa kuanzia sasa ni marufuku sukari kusafrishwa usiku na usafirishaji utafanywa kuanzia saa 12 alfajiri hadi saa 12 jioni huku akitangaza kuongeza ulinzi katika maeneo ya mipakani. Aidha aliagiza viwanda vyote kutoa ushirikiano katika kudhibiti uuzaji kwa njia ya magendo pamoja na orodha ya magari yote yanayochukua bidhaa hiyo kutoka viwandani, namba zake na kiasi kilichobebwa. Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, kila kiwanda cha kuzalisha sukari kitatoa taarifa ya kiasi cha uzalishaji kila siku kabla ya saa 12 jioni kwa Wizara ya Kilimo, Bodi ya Sukari na mkoa kilipo kiwanda husika. Aidha serikali imewaagiza makatibu tawala wa mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Manyara kuteua mawakala waaminifu ambao serikali itawapa leseni za kusambaza sukari mikoani mwao. Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi katika maeneo ya Rongai, Kamwanga, Tarakea na Holili kwa upande wa wilaya ya Rombo, umebaini kuwa licha ya kuwapo askari wengi wa doria waliotanda katika barabara kuu, bado sukari inapita mbele yao. Baadhi ya askari hao wanadaiwa kuwa na ukwasi wa kutisha unaotokana na fedha wanazochukua kutoka kwa wafanyabiashara wa sukari wanaovusha kwenda nchi jirani ya Kenya wakitumia pikipiki maarufu kama bodaboda. Pikipiki hizo zimekuwa zikipishana katika Barabara ya Tarakea Rongai zikiwa zimebeba mifuko ya sukari yenye nembo ya kiwanda cha sukari cha TPC ikiwa katika ujazo wa kilo 50 kila mmoja. Kinachofanywa na wafanyabiashara hao ni kuisafirisha sukari hadi Tarakea wakitumia magari aina ya Fuso na wanapofika huko huwapa polisi rushwa inayojulikana kama ‘safisha njia’ na kuipeleka porini ambako hukodi pikipiki zinazopenya kirahisi kwenye njia za panya. Chanzo: Tanzania Daima