TAARIFA:Chama Cha Mapinduzi(CCM)Kimepokea Kwa Masikitiko Makubwa Taarifa Za Kifo Cha Mmoja Wa Mawakala Wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA)

Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mmoja wa mawakala wa CHADEMA Mbwana Masoud kilichotokea baada ya upigaji kura katika uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Igunga mkoani Tabora.
Kifo hicho kinasikitisha, hasa ukizingatia mazingira ya kutokea kwake kutatanisha na kuacha maswali mengi kwa umma, kutokana na chanzo cha uhakika cha kifo cha kijana huyo kutojulikana mpaka sasa.
CCM inaungana na watanzania kuomboleza msiba huo, na kutoa pole kwa familia ya marehemu Mbwana Masoud, Ndugu Jamaa na Marafiki wa familia yake na kwa kuwa kijana huyo alikuwa Wakala wa Chadema, pia CCM inapenda kutoa pole kwa Viongozi na wanachama wa Chadema kufuatia msiba wa kijana huyo.
Pamoja na masikitiko hayo, CCM inakanusha vikali uvumi uliotolewa na baadhi ya watu na kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba Chama Cha Mapinduzi kinahusika na kifo cha kijana huyo.
Taarifa hizo si za kweli kabisa, na kwamba zimejaa uongo na uzushi, huku zikibeba dhamira ya kuipaka matope CCM mbele ya umma.
Lazima itambulike kuwa CCM ni chama Cha siasa ambacho kutokana na historia yake, hata siku moja hakijawahi na hakitakuja kuendesha hila chafu kama hizo zinazoweza sababisha mauaji ya mwananchi yeyote, kwa sababu hiyo si sehemu ya kazi ya siasa kinayoifanya.
CCM inavitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka ili kuwabaini na kuwakamata wote watakaobainika kuhusika na unyama huo ili ukweli dhidi ya mauaji hayo uweze kujulikana mbele ya umma.

Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano na Umma
Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM
Dar es Salaam
Oktoba 16,2011

Categories: , ,