na Danson Kaijage, Dodoma
MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) kanda ya kati imekamata tani moja ya dawa za binadamu zenye thamani ya sh milioni 28.4 zilizoisha muda wa matumizi.
Akiongea na Tanzania Daima ofisini kwake, Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Kati, Florent Kyombo, alisema dawa hizo zilikamatwa kutokana na msako wa maduka yanayouza dawa za binadamu zilizoisha muda wake.
Alisema katika msako huo katika Manispaa ya Dodoma, maduka saba yalibainika kuuza dawa zilizopitwa na wakati.
Alisema maduka 17 yalikaguliwa na kubaini kuwa dawa mbalimbali zenye uzito wa tani moja zenye thamani ya sh milioni 28.4 zilikuwa zimeisha muda wa matumizi na zitateketezwa hivi karibuni.
Mbali na hilo, Kyombo alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa maduka yanayouza dawa zilizoisha muda wake, mamlaka hiyo imepanga kufanya msako mwingine mzito zaidi.
Kwa upande wa dawa zinazouzwa na Wachina alisema kuwa imebainika kuwa maduka mengi ya dawa zinazouzwa na Wachina hazina ubora wowote na dawa nyingi siyo za asili kama wanavyokuwa wakieleza.
“Kwanza nataka kusema kuwa Wachina hawana kibali cha kuuza dawa za binadamu bali wana kibali cha kufanya utafiti wa dawa za miti shamba lakini wamekuwa wakijipenyeza kwa ajili ya kufanya biashara ya madawa ya binadamu.
“Hata hivyo dawa wanazozitumia siyo kweli kuwa zote ni za kienyeji bali wanachukua dawa hizi zetu wanazitoa katika vifungashio vya awali na wanaziweka katika vifungashio vya kwao na kuanza kudai kuwa ni za Kichina,” alisema Kyombo.
Kutokana na kuwepo kwa uuzwaji dawa feki katika maduka ya dawa za binadamu, Kyombo amewataka wananchi wa Manispaa ya Dodoma kuhakikisha wananunua dawa katika maduka ya dawa yaliyosajiliwa pamoja na kununua dawa hizo katika vituo vya afya na zahanati.
Categories: