Na Jackson Kimambo
Walimu wa Wilaya ya Moshi Vijijini wametishia kugoma kufundisha na kufanya maandamano makubwa hadi kwa Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro kumwelezea kilio chao cha kutolipwa mshahara.
Walimu hao wamedai kuwa mpaka kufikia jana walikuwa hawajalipwa mshahara wa mwezi uliopita kutokana na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini kukosa fedha.
Baadhi ya walimu waliozungumza na NIPASHE na kuomba majina yao kuhifadhiwa, walidai kuwa licha ya kutolipwa mshahara mpaka sasa, lakini pia uongozi wa Halmashauri haujawaeleza chochote.
Walisema watagoma kufanya kazi na kuandamana hadi kwa Mkuu wa Mkoa ili kufikisha kilio chao hicho.
Walidai kuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo mara kwa mara amekuwa hawatendei haki kutokana na kuwacheleweshea mishahara yao.
“Kila siku tunakwenda benki kuangalia mshahara lakini hakuna kitu. Tunatumia nauli za kwenda na kurudi mjini kula na kulala...hii ni hasara kubwa kwetu,” alisema mmoja wa walimu hao.
Alisema hali hiyo imewafanya wapoteze vipindi madarasani kwa takriban wiki mbili wakifuatilia mshahara wao.
Akijibu malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, Annah Mwahalende, alisema ni kweli walimu na watumishi wengine bado hawajalipwa mishahara yao kutokana na kuchelewa kufika kutoka wizarani.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alisema taratibu zote zimekamilika na wameshapeleka hundi benki ili walimu na watumishi wengine wa halmashauri hiyo walipwe mishahara yao kama kawaida.
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ina jumla ya walimu 4,037.
CHANZO: NIPASHE
Categories: