Yanga yaingia hofu

Na Zahoro Mlanzi

UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umefuta mechi za kirafiki kwa sasa kutokana na kuhofia wachezaji wake kuumizwa hususani, kipindi hiki ambacho wapo katika mkakati wa
kuhakikisha inashinda mechi zilizobaki za mzunguko wa kwanza Ligi Kuu Bara .

Kauli hiyo imekuja baada ya timu ya Ruvu Shooting ya Pwani wiki iliyopita, kutangaza jana ingecheza na Yanga mchezo wa kirafiki uliotarajiwa kupigwa Uwanja wa Mabatini Mlandizi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo Louis Sendeu, alisema kwa sasa hawana mpango wa kucheza mechi zozote za kirafiki kwa kuhofia wachezaji wake kupata majeraha.

"Tumeanza vibaya ligi kutokana na wachezaji wetu wengi kuwa majeruhi, lakini walipopona tukaanza kukaa vizuri katika msimamo wa ligi hiyo, hivyo tangu tuanze kupata matokeo mazuri tumekuwa makini na wachezaji wetu wasiumie tena," alisema Sendeu.

Alisema na ndiyo maana walikataa kucheza na Ruvu kwa kuhofia hilo, lakini wanashangaa kuona wakitangazwa kucheza nao, wakati walishakaa tangu zamani.

Aliviomba vyomba vya habari kuwa makini na taarifa zinazotolewa na ikiwezekana vithibitishe kwa wahusika, kwani hiyo inasababisha usumbufu kwa wapenzi na wanachama wao kuulizia kila wakati.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Kager Sugar, utakaopigwa Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam alisema wanaendelea vizuri na kwamba hawana majeruhi zaidi ya nahodha, Shadrack Nsajigwa.

Hata hivyo alisema hali ya nahodha huyo inaendelea vizuri na wakati wowote ataanza kujifua na wenzake.
Yanga katika msimamo wa ligi hiyo ipo katika nafasi ya tano, ikiwa na pointi 15, nyuma ya timu za Mtibwa, Azam, Simba na vinara wapya wa ligi, JKT Oljoro ambayo ina pointi 19.

Categories: