Yanga yatimua vumbi




OLIVER ALBERT

YANGA inapiga hesabu ya mechi tano zilizobaki mzunguko wa kwanza, lakini Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Fred Felix Minziro amesema wanazipigia rada mechi tatu kwani ndio ngumu na wameziandalia silaha kali za maangamizi kabla ya kuzitimulia vumbi.

Vigogo hao walioanza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kusuasua, wamebakiza mechi tano za mzunguko wa kwanza dhidi ya Kagera Sugar, Toto African, JKT Oljoro, Simba na Polisi Dodoma.

Minziro alisema mikakati yao ni kushinda mechi tano ili kuendelea na harakati zao za kutetea ubingwa wa Tanzania Bara ingawa amedai mechi tatu ndio zinazowaumiza kichwa.

Beki huyo wa kushoto wa zamani, ambaye pia huitwa kwa jina la utani la `Majeshi' alijigamba kuwa wamepania kuwaliza wapinzani wao wa jadi, Simba, JKT Oljoro inayoongoza ligi na Kagera Sugar.

�Hakuna timu rahisi kwenye ligi lakini rada zetu tumezielekeza kwa Simba, JKT Oljoro na Kagera kwani ndio wagumu zaidi.

�Kagera Sugar mara nyingi huwa wanatusumbua tukikutana ingawa msimu uliopita tuliwafunga mara zote, hivyo si timu ya kubeza, hawa Oljoro wanaongoza ligi sasa bila kusahau watani zetu Simba, ambao tukikutana nao vumbi hutimka.

�Mkazo wetu uko kwa wachezaji kuhakikisha wanajituma na kujitolea ili lengo letu litimie la kupanda kileleni, naamini wachezaji wetu tumewaandaa vizuri na hawatatuangusha, � alisema Minziro, ambaye alifichua katika siku za karibuni wamekuwa wakishughulikia zaidi suala la ufungaji.

Minziro alisema wanataka si kushinda tu bali kuhakikisha pia wanapata mabao mengi huku wakiiombea Simba ipoteze mechi zake.

Alisema wametumia wakati huu wa mechi ya Stars kuwafua washambuliaji wa timu hiyo na ameridhika na kiwango chao.
Alidai kuwa wamewapa mbinu za kutosha washambuliaji wao ili kuhakikisha timu haikabiliwi na ukame wa mabao.

Minziro alisema kwa sasa anaamini kikosi kiko vizuri na watu wategemee mambo makubwa kwenye mechi zao zinazofuata kama vile ilivyokuwa kwa Coastal Union walipoibuka na ushindi wa 5-1.

Ikiwa Simba itashinda mechi tano itafikisha pointi 33 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi kwani hata kama Yanga itashinda mechi zote tano itaambulia pointi 27.

Simba wamebakiwa na mechi tano ambazo ni dhidi ya African Lyon itakayokutana nayo Jumapili, Ruvu Shooting, JKT Ruvu , Yanga na Moro United.

Katika mechi hizo zote, Simba ina kazi nzito zaidi kwani timu zote itakazokutana nazo zinacheza soka la uhakika tangu kuanza kwa ligi hiyo hivyo itabidi ifanye kazi ya ziada kuhakikisha inaibuka na ushindi kama inataka kurudi kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Categories: