Askofu Dkt.Thomas Laizer (picha kutoka maktaba).
********
*Ataka iache kudhoofisha upinzani, kulinda amani iliyopo
*Asema CHADEMA inaongoza kwa umaarufu nchini
*Adai kutoridhishwa na matokeo yanayotangazwa na NEC
Na Gladness Mboma, Moshi
ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dkt.Thomas Laizer, amesema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete isifanye kazi ya
kudhoofisha nguvu ya vyama vya upinzani hasa wakati wa kupiga kura na kama hali hiyo itaendelea, wananchi watashindwa kuvumilia hivyo kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu uliopo nchini.
Alisema Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), kina umaarufu mkubwa kuliko vyama vingine vya siasa nchini hivyo umefika wakati wa Serikali kuviheshimu na kuvipa nafasi vyama vya upinzani ili viweze kufanya shughuli zao bila vikwazo hasa katika chaguzi mbalimbali.
Askofu Laizer aliyasema hayo juzi katika harambee ya kuchangia ukarabati na upanuzi wa kanisa la KKKT Nshara, lililopo Machame, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Bw. Reginald Mengi.
Katika harambee hiyo ambayo ilikwenda sambamba na Jubilee ya miaka 50 ya kuzaliwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa na Mbunge wa Hai, Bw.Freeman Mbowe, zaidi ya sh.milioni 200 zilichangwa.
“Kuna watu wanashindwa kutamka wazi kuwa CHADEMA ni chama maarufu hapa nchini, rushwa za kununuliana kanga wakati wa uchaguzi haziwezi kuwafikisha Watanzania popote, miaka 50 ya Uhuru itakuwa na maana kwetu kama tutaondoa chuki kandamizi.
“Kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza matokeo na kukubaliwa hata kama hayana ukweli binafsi sikubaliani nacho, naomba tujirekebishe katika kipindi kingine cha miaka 50, tusipofanya hivyo amani tuliyonayo itatoweka,” alisema.
Aliwasihi Watanzania kudumisha amani na utulivu uliopo sio katika mambo yanayohusu siasa pekee bali hata katika madhehebu ya dini kwa kuhakikisha jambo lolote ambalo litaonekana kufanywa kinyume, litatuliwe kwa mazungumzo.
Alisema Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa, “Mficha maradhi kilio kitamuumbua” hivyo amani iliyopo nchini itadumu kama haki itatendeka.
Askofu Laizer aliongeza kuwa ni jambo la kumshukuru Mungu kwa Tanzania kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru bila ya mapigano wala umwagaji damu na kusisitiza kuwa, kila Mtanzania awajibike kumuomba Mungu ili aendelee kusimamia amani miaka 50 ijayo.
Alisema maandamano yoyote yanayofanywa na wananchi au vyama vya upinzani kupinga mambo mbalimbali, lazima Serikali ikae chini, ijiulize na kutafuta ufumbuzi wa tatizo badala ya kutumia nguvu nyingi kuyazima na kusababisha madhara.
“Naipongeza Serikali kwa kujenga barabara ambazo awali hazikupitika kirahisi, naomba uboreshaji wa miundombinu uendelee katika kipindi cha miaka 50 mingine ili kuharakisha maendeleo ya sekta mbalimbali,” alisema Askofu Laizer.
Mbunge wa Siha, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bw. Agrey Mwanri, ambaye alikuwepo katika harambee hiyo, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru.
“Ni jambo la kumshukuru Mungu kutufikisha hapa tulipo, nchi yetu inashirikiana vizuri na mataifa mbalimbali duniani, raia wa nchi hizo wamekimbilia nchini kwa sababu ya amani tuliyonayo,” alisema.
Kwa upande wake, Bw.Mbowe alisema ujasiri wa kweli ni ule wa kukaa chini na kusikiliza wenzako kile wanachosema ili matatizo yaliyopo nchini yaweze kushughulikiwa.
Categories: