*RC atoa tamko rasmi, huduma za umeme, maji kukatwa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam akiongea na waandishi. (Picha kutoka maktaba).
Na Anneth Kagenda
WAKATI Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), ikitoa tahadhari kwa wananchi katika mikoa mbalimbali kuchukua tahadhari juu ya mvua zinazoendelea kunyesha na
kuleta maafa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw.Meck Sadick, jana ametoa tamko la kuwataka wananchi waishio mabondeni kuhama maeneo hayo haraka.
Bw.Sadick alitoa tamko hilo Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, wananchi ambao watashindwa kuhama maeneo hayo, sheria itachukua mkondo wake.
Alisema wananchi waliojenga mabondeni ni wavamizi ambapo dhamira ya Serikali ni kusitisha huduma muhimu katika maeneo hayo hususan umeme na maji mara baada ya kukamilika mchakato wa ugawaji viwanja kwa wakazi hao katika eneo la Mabwepande wilayani Kinondoni.
Alisema usitishwaji wa huduma hizo pia utawahusu wakazi wa Jangwani na Bonde la Msimbazi ambapo wananchi waliopewa hifadhi katika shule mbalimbali, wataondolewa siku nne kabla ya shule kufunguliwa Januari 9, 2012.
“Hivi sasa Serikali inaangalia eneo lingine ambalo tunaweza kuwahifadhi wakati upimaji wa viwanja ukiendelea ili shule zifunguliwe na wanafunzi waingie madarasani.
“Wakati mchakato wa upimaji viwanja ukiendelea, wakazi waishio mabondeni wanapaswa kuezua mabati yao pamoja na kubomoa matofari, hakuna mtu anayeweza kusema ana hati ya kumiliki kiwanja katika maeneo ya mabondeni na kama anayo, aende kwa mtu aliyempa hati iwe Manispaa au kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ili mmalizane, mkishindwana nendeni mahakamani,” alisema.
“Tunachotaka wakazi waishio mabondeni waondoke kwa hiari yao kabla sheria haijachukua mkondo wake, pamoja na kwamba tuliwahi kuwapa viwanja huko Yombo Buza na Wazo Hill, wengine waliviuza lakini kwa huruma ya Serikali tumewatafutia viwanja vingine,” alisema Bw.Sadick.
Aliongeza kuwa, Serikali haiwezi kuendelea kunyamaza wakati watu wanakufa kwa ajili ya kukaa maeneo hatarishi na kukaidi kuondoka maeneo hayo huku wengine wakidai maeneo hayo wamekaa miaka mingi.
“Nimepata taarifa kwamba licha ya Serikali kutoa matamko, kuna watu wanarudi lakini kwa sababu tumetoa tamko, baada ya kukamilika mchakato wa kugawa viwanja, tutatoa muda kidogo wa kuondoka mabondeni, yule ambaye atakaidi atakuwa anashindana na Serikali,” alisema.
Alipoulizwa kwanini Serikali ilikaa kimya muda wote hadi kutokea kwa mafuriko hayo na kusababisha maafa kwa wakazi wa mabondeni, Bw.Sadick alisema sheria ilikuwa inaendelea kufanyia kazi suala hilo baada ya watu kutakiwa kuondoka lakini wakapeleka pingamizi la kupewa muda ili waondoke.
“Safari hii wataondoka tu kwa sababu maafa yanayotokea hata taifa linaathirika kwa namna moja au nyingine, watu tunaowahudumia ni wengi kwa kuwapa vyakula na malazi,” alisema.
Akizungumzia utaratibu utakaotumika kuwatambua wamiliki halali wa nyumba zilizoathirika na mafuriko alisema, kazi hiyo inafanywa na Shirika la Msalaba Mwekundu ambao wako makini kuhakikisha kazi yao ili kuondoa ubabaishaji unaoweza kujitokeza.
“Wapangaji waliopo katika nyumba zilizopo mabondeni, wawaeleze wamiliki wa nyumba hizo ili warudishiwe kodi walizolipa, kama watashindwana waende mahakamani,” alisema.
Alisema waathirika waliopewa hifadhi, kila mmoja amepewa chakula chake ili apike mwenyewe ambapo mpango huo, umeanza jana jioni ili kuondoa usumbufu unaojitokeza.
Bw.Sadick alisema wananchi ambao bado wapo katika maeneo hatarishi, Serikali inawachukulia kama wahalifu kwani hakuna sababu yoyote ya kukaa maeneo hayo wakati kuna mahema ya kutosha.
Desemba 20, mwaka huu, mvua kubwa iliyonyesha jijini Dar es Salaam, ilisababisha mafuriko ambapo hadi kufikia juzi, watu 40 waliripotiwa kufariki dunia.
Mvua hiyo pia ilisababisha upotevu wa mali na kuharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja.Sheria ya ardhi ya mwaka 1979, inazuia watu kukaa katika maeneo hatarishi wakati sura ya 113 kifungu cha saba, kinasema kama eneo husika ni hatarishi, mtu yoyote hapaswi kujenga makazi na kuishi.
Categories: