WALIMU WATANGAZA KUGOMA NCHI NZIMA


Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana , kuhusu mgomo wa walimu nchi nzima utakaoanza mwezi Januari kama Serikali haitatimiza makubaliano yaliyofikiwa ya kuwalipa madai yao. Picha na Venance Nestory

Na Raymond Kaminyoge


CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT), kimetangaza mgomo wa walimu nchi nzima kuanzia Januari mwakani ikiwa ni hatua ya kuishinikiza Serikali iwalipe walimu deni la malimbikizo ya stahili zao mbalimbali, linalofikia Sh49.6 bilioni.

Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kushindwa kutimiza ahadi yake ya kuanza kuwalipa walimu fedha hizo tangu Novemba mwaka huu. Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na wandishi wa habari kuwa Serikali iliahidi kuwalipa walimu Novemba hadi Desemba mwaka huu ili kumaliza deni hilo.

“Natangaza kuwa shule zitakapofunguliwa mwezi Januari 2012, sisi walimu tutaendelea kuwa likizo mpaka kero zetu zitakapotatuliwa,” alisema Mukoba. Alisema tangu Juni mwaka huu, CWT na Serikali wamekuwa na vikao kadhaa kuhusu madai hayo na ikafikia uamuzi wa kuwalipa walimu katika kipindi cha miezi miwili ambayo ni Novemba na Desemba mwaka huu.

“Kumbe Serikali haikuwa na nia ya kweli kutaka kutulipa, waliona tunaweza kugoma katika kipindi cha mitihani ya taifa wakatudanganya,” alisema. Alisema kwa kuwa Serikali haina nia ya dhati katika kulipa madai hayo, wameamua kufikia uamuzi wa kutoendelea kufundisha.

Mukoba alisema wakati mishahara na posho za wabunge zikizidi kuongezeka, walimu wanashindwa kulipwa madai yao ya msingi. “Tunawaomba wazazi watuunge mkono katika mgomo huu ili watoto wenu wapate elimu sahihi,” alisema Mukoba. Kwa mujibu wa Mukoba, madai hayo yanayowahusu zaidi ya walimu 3,000 ni ya kuanzia mwaka 2008.

Alisema kero nyingine inayowafanya walimu wagome ni waraka kandamizi uliotolewa na Serikali mwaka 2007 unaowashusha vyeo walimu wanaojiendeleza kielimu. “Serikali ilikubali kuufuta waraka huo baada ya kuridhika kwamba ulikuwa unawakandamiza walimu, lakini hadi sasa unaendelea kutumika, haujafutwa,” alisema. Mukoba alisema waraka huo umelenga kuwakatisha tamaa walimu ili wasijiendeleze kielimu.

Aidha, Mukoba alisema walimu wanakaa kwa muda mrefu bila kupandishwa vyeo ingawa wanastahili kulingana na sifa zao. “Walimu tumekosa nini, kwa nini kilio chetu hakisikiki na Serikali? Iweje tunadanganywa kila siku? Sasa ni lazima tuchukue hatua,” alisema Mukoba. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawamba hakupatikana jana kuzungumzia tishio hilo la mgomo baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana kabisa.

Categories: