HABARI NA CHARLES NGEREZA
Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Arusha, umethibitisha kuendesha zoezi la bomoa bomoa katika nyumba zilizojengwa kando kando ya barabara ya Namanga-Arusha na kusema kuwa wamiliki wa nyumba hizo walipewa taarifa kabla ya zoezi hilo.
Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Arusha, Albert Kent alisema kuwa nyumba zilizobomolewa hazifiki 100 kama inavyodaiwa na wanaolalamika.
“Nyumba zilizobomolewa ni kama hamsini tu, zingine zimeguswa kidogo tu na zingine ni vibanda, kuta za nyumba na mageti,” alisema Kent.
Alisema kuwa walitoa matangazo wiki iliyopita kuwatakan wananchi kutii mamlaka kuvunja nyumba zao wenyewe, lakini baadhi waliitikia vizuri na kuzivunja wenyewe.
Alieleza kuwa zoezi hilo limefanywa kwa umakini na kwamba nyumba zilizovunjwa ni zile zilizoingilia katika eneo la barabara.
“Kila nyumba iliyovunjwa tulipima na kuhakiki kama imeingilia eno letu ambalo ni mita ishirini na mbili na nusu na baada ya kujiridhisha tulivunja, hakuna haki ya mtu tuliyoihujumu,” alisema Kent.
Aliongeza kuwa nyumba zingine zilibomolewa na wananchi wenyewe ambao walikubali wito halalali wa kubomoa nyumba zao ambazo zilijengwa kimakosa ndani ya eneo la barabara.
Kent alikanusha vikali madai ya baadhi ya walalamikaji ambao wanadai kuwa baadhi yao walipewa barua za kuonyesha kuwa nyumba zao ziliwekewa alama hizo kimakosa.
“Napenda niweke rekodi sawa sawa hapa, kila nyumba tuliyovunja tulianza kupima pale pale kwenye eneo la tukio kabla ya kuvunja,” alisema Kent.
Wakati mamlaka hiyo ikitoa msimamo huo, wananchi waliobolea nyumba zao wanasema kuwa watatafuta haki yao bila kukoma.
Wananchi hao wamedai kuwa mali nyingi za watu ziliharibiwa na zingine ziliporwa na lawama zote wanazitupa kwa Tanroads.
“Ndugu mwandishi nawashangaa Tanroads kusema nyumba zetu ni vibanda, hizo ni nyumba za kwetu hapaswi kuviita viambaza,” alisema mmoja wa waathirika aliyejitambulisha kwa jina moja la Meitarano.
Zoezi hilo la bomoa bomoa lilifanyika juzi chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi.
CHANZO: NIPASHE
Categories: