MH STTA: SIOGOPI KUSHTAKIWA KUMTETEA MWAKYEMBE

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema haogopi kupelekwa mahakamani kutokana na kutamka kuwa Dk Harrison Mwakyembe amelishwa sumu, kwak sababu ana ushahidi wa kutosha.

Kauli hiyo ni mwendelezo wa mjadala mzito unaotikisa nchi kwa sasa baada ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, kusema polisi wameandaa jalada la kumpeleka mahakamani waziri huyo kutokana na madai hayo.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Wwaziri Sitta alisema kama Dk Mwakyembe amedai kuwa, ripoti ya daktari wake inaonyesha kuna kitu kwenye ndani ya mifupa kinachochea hali aliyonayo, yeye anapelekwa mahakamani kwa kosa lipi.

Tayari, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda, amemruka Manumba akisema hatambui ripoti ambayo aliitoa kwa waandishi, ambayo inaonyesha Dk Mwakyembe hakunyweshwa sumu.

Sitta akisisitizia kwamba Dk Mwakyembe kapewa sumu, alisema kutokana na hali hiyo yupo tayari kwa lolote katika hilo na kwamba, anasubiri jalada hilo lipelekwe mahakamani ambako ndiko kwenye uamuzi wa kisheria.
“Ukiwa mwanasheria huwezi kuogopa mahakama, mimi ni mwanasheria namba 384 wa Mahakama Kuu.Nimesajiliwa kisheria na natambulika kwenye vyama vya wanasheria. Niko tayari kwa lolote litakalotokea kuhusu hilo na siwezi kuogopa kwa kusema ukweli,”alisisitiza Sitta.

Aliongeza kuwa anachotakiwa kufanya DCI, ni kuwasiliana na viongozi wake wa juu akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ili aweze kuwapa taarifa hizo na kuwasilisha jalada hilo mahakamani.

Sitta alisema licha ya hilo, anashindwa kuelewa kosa linalompeleka mahakamani, ikiwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Mponda amemkana na Mkuu wake wa kazi ( IGP), Said Mwema.

Alisema Dk Mwakyembe mwenyewe ametoa ufafanuzi kuhusu suala hilo na kumwambia DCI alikopata mamlaka ya kutoa tamko kuhusu afya yake,hivyo basi anasubiri jalada hilo lipelekwe kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), ili afikishwe mahakamani.

Alisema anachotakiwa Manumba ni kutekeleza kile alichokusudia ili aweze kufanikiwa, kutokana na hali hiyo anasubiri uamuzi huo.

“Ni kichekesho bwana, we unafikiri mimi naogopa kupelekwa mahakamani kwa hili? Hata siku moja... niko kwa ajili ya kusema ukweli, nitasema ukweli daima na wala siogopi kwenda mahakamani, nashindwa kumwelewa huyu bwana, tena muulize Manumba ameshawasiliana na viongozi wangu wa juu maana sheria zinasema anapaswa kuwasiliana nao kabla ya kuwasilisha jalada lake mahakamani,”alisema.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Manumba alikanusha Dk Mwakyembe kulishwa sumu na kwamba, jeshi hilo linakamilisha uchunguzi ili kuwasilisha jalada la kumfikisha mahakamani Waziri Sitta kutokana na kusambaza habari hizo.

Alichokisema Dk Mwakyembe
Mwishoni mwa wiki iliyopita, akitoa tamko baada ya kukerwa na kauli ya polisi, Dk Mwakyembe alisema anapata taabu kuamini kama Manumba na wenzake walisoma taarifa halisi ya matibabu yake au walisoma taarifa ‘nyingine’ na kama waliisoma wenyewe au ‘walisomewa’

“Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa waandishi wa habari, hakifanani kabisa na picha iliyoko kwenye taarifa halisi ya Hospitali ya Apollo inayotamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow (uboho) kinachochochea hali niliyonayo,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza:

“Kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua, kukidhibiti au kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu: hakulishwa sumu.”

Pia, alitoa sababu kuu tatu za kupinga ripoti o ya DCI akisema:"Kwanza, kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake, unaoendelea katika Hospitali ya Apollo, nchini India, ambako bado sijahitimisha matibabu yangu, pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa “sikunyweshwa sumu” wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu.

Alisema sababu ya tatu ni kitendo cha Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima sasa, halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.

Habari hii imendaliwa na Patricia Kimelemeta, Anthony Mayunga, Serengeti, Joseph Zablon, Venance George, Morogoro

CHANZO: MWANANCH

Categories: