KLABU ya soka ya Simba imesikitishwa na habari iliyotoka katika gazeti moja la kila siku toleo la leo, Januari 31, 2012, inayodai kuwa klabu inakabiliwa na matatizo makubwa ya ukata yaliyosababisha, pamoja na mambo mengine, timu kushindwa kukaa kambini.
Habari hizo hazina ukweli wowote na inasikitisha kwamba imetoka katika gazeti linaloheshimika kama hilo
Simba SC inapenda kusema mapema kwamba timu imeingia kambini katika hoteli ya Lamada jijini Dar es Salaam tangu jana na hata mwandishi wa gazeti hilo aliambiwa na uongozi wa Simba alipouliza kuhusu hilo.
Hata hivyo, na hili pia gazeti waliambiwa jana, Simba imeamua kufanya maamuzi ya kuweka kambini timu kwa siku chache kabla ya mechi. Maamuzi haya yametokana na maombi ya wachezaji na benchi la ufundi kwa uongozi.
Benchi la ufundi na wachezaji wa Simba walishauri kuwa kwa kuwa wengi wa wachezaji wana familia zao, wakati mwingine hupata matatizo ya kisaikolojia yanayotokana na kukaa mbali na familia zao kwa muda mrefu wakiwa kambini.
Kwamba ni vizuri pia kwa wachezaji kwenda mazoezini wakitokea kwenye familia zao ukizingatia kuwa wao ni watu wazima wanaojua wajibu wao.
Wachezaji wa Simba wameuhakikishia uongozi kuwa watafanya vizuri kwenye michuano mbalimbali wanayoshiriki msimu huu kwa utaratibu huo.
Uongozi wa Simba ulikubaliana na mapendekezo hayo ya wachezaji na benchi la ufundi. Na ifahamike kuwa wanachoomba wachezaji wetu si kitu kigeni. Katika nchi zilizoendelea kisoka, wachezaji hukaa kambini mara moja tu wakati wa maandalizi ya kuanza kwa msimu. Baada ya hapo timu huwa haikai kambini.
Kwa hiyo walichokiomba wachezaji si kitu kibaya au kipya katika medani ya soka.
Uongozi wa Simba umewaambia wachezaji kuwa wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanafanya vizuri ili utaratibu huo uwe wa kudumu kwa lengo la kukuza soka la Tanzania na kuamini kuwa wachezaji wa Tanzania wanaweza kuishi maisha ya kiweledi wakipewa fursa.
Hicho ndicho kilichotokea na hakuna suala la ukata. Pendekezo hili limetoka kwa wachezaji na benchi la ufundi na si kwa uongozi.
Yote haya mwandishi wa gazeti aliambiwa lakini bado akaendelea na stori yake hiyo kwa sababu ambazo ni vigumu kuzifahamu.
SIMBA SC inatoa wito kwa wana habari kuwa makini kwenye kuripoti matukio. Ile dhana kwamba habari mbaya ndiyo inauza haina maana kwamba mwandishi hatakiwi kutenda haki.
Simba haitaraji upendeleo wa aina au namna yoyote kutoka kwenye vyombo vya habari bali inachohitaji ni kutendewa haki tu.
Wenu katika kazi
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
Categories: