WABUNGE CCM WAGOMA KUKUTANA NA RAIS KIKWETE

WAJIPANGA KUKWAMISHA MUSWADA MABADILIKO YA KATIBA


Habari na Midraji Ibrahim, Dodoma


SASA ni dhahiri kuwa wigo wa mpasuko kati ya wabunge wa CCM na Serikali unazidi kupanuka, baada ya wabunge hao kugoma kukutana na Rais Jakaya Kikwete mjini Dodoma.Katika kikao chao kilichofanyika Ijumaa usiku ukumbi wa Pius Msekwa mjini hapa, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwaomba wabunge hao kukutana na Rais Kikwete ili kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya Serikali badala ya kuendelea kuikwamisha bungeni.Wabunge hao wanadaiwa kukataa rai hiyo huku wakimweleza waziwazi Pinda kwamba, itakuwa ni kumkosea heshima na adabu Rais, iwapo watakutana naye halafu wakwamishe marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayotarajiwa kufikishwa bungeni wiki ijayo.

“Itakuwa siyo heshima kukutana na Rais halafu tukwamishe muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kwa sababu tumejipanga kuhakikisha kwamba haupiti,” vilieleza vyanzo vyetu vya uhakika kutoka ndani ya kikao hicho.

Badala yake, wabunge hao walikubali kuteua miongoni mwao watu watano ambao wataonana na Rais Kikwete leo atakapowasili mjini hapa akitokea Mwanza kwenye Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 34 ya CCM.

Wazungumzaji wakuu kwenye kikao hicho wanadaiwa walikuwa pamoja na, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na Mbunge wa Shinyanga, Steven Masele.

Marekebisho hayo yalitarajiwa kuwasilishwa kesho, lakini walikataa hadi Ijumaa kwa kile walichodai kuwa, wengi wao watakuwa hawajarejea kutoka Mwanza kwenye sherehe za maadhimisho ya CCM.

Inadaiwa na wabunge hao wa CCM kuwa, marekebisho hayo yanalenga kukimaliza chama hicho na kukiweka madarakani Chadema baada ya kuondolewa kwa wakuu wa wilaya, kushiriki mchakato wa katiba na kazi hiyo kukabidhiwa wakurugenzi wa halmashauri.

“Hii ni dhahiri kuwa marekebisho haya yanaiumiza CCM na kuisimika Chadema madarakani. Kuwaondoa Ma-DC kwenye mchakato wa katiba na kuweka wakurugenzi wa wilaya ambao wote ni Chadema, hatuwezi kukubali kamwe,” kilieleza chanzo chetu.
Pia, inadaiwa na wabunge hao kuwa marekebisho waliyopewa Dar es Salaam kwenye kamati, ni tofauti na yale yaliyowasilishwa bungeni, huku kukiwa na ongezeko la kurasa nne.

Hata hivyo, inadaiwa baada ya wabunge hao kugoma kukutana na Rais Kikwete, alisimama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Stephen Wasira, akiwataka kupitisha marekebisho hayo kwa sababu ni agizo la Rais, hali iliyosababisha azomewe huku akitupiwa maneno ya kashfa.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge hao ambao hawakupenda kutajwa majina yao, walisema athari wanayoiona mbele kwa kutopitishwa kwa marekebisho hayo, Chadema watapeleka mashtaka kwa umma kwamba sheria ile ilipitishwa kulinda CCM, hivyo haina manufaa kwa umma.

“Lakini CCM hatujajipanga, kila siku anayesimama jukwaani anazungumzia kujivua gamba, kwa hali hii tusubiri mashambulizi mazito siyo tu kutoka kwa Chadema hata nchi za nje,” kilieleza chanzo chetu.

Pia, wabunge hao wa CCM wanadai kuwa miongoni mwa sababu za kukwamisha marekebisho hayo, ni kile walichodai Rais Kikwete kuwadharau kutokana na wao kupitisha muswada wa sheria hiyo, halafu yeye (Kikwete) anakutana na Chadema dakika chache na kukubaliana na hoja zao.

“Sisi tumekaa hapa (bungeni) kwa zaidi siku mbili na akili zetu timamu, tukapitisha muswada ule, anakutana (Kikwete) na Chadema dakika chache anatuletea marekebisho! Hiyo ni dharau na hatuwezi kukubali,” alilalamika mbunge mmoja.

Kura ya kukosa imani na Rais
Katika kikao cha wabunge hao kilichofanyika Alhamisi wiki hii, baadhi yao walihoji sababu zinazokwamisha masuala mbalimbali serikalini kutopatiwa ufumbuzi, huku Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, akipendekeza kwamba kama tatizo ni Rais Kikwete, watumie utaratibu wa kumpigia kura ya kutokuwa na imani.

Shelukindo anadaiwa alitaka kujua sababu za masuala mbalimbali kukwama na kutopatiwa ufumbuzi wa haraka na kwamba, iwapo tatizo ni Rais Kikwete, wapo tayari kufuata utaratibu wa kumpigia kura ya kutokuwa na imani.

Hata hivyo, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Olle Sendeka, alisimama na kumtaka mbunge huyo kufuta kauli yake, suala ambalo Shelukindo alikubali.

Pia, katika kikao hicho kiliwataka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda, Naibu wake, Dk Lucy Nkya na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni, kujiuzulu kutokana na kuwa chanzo cha mgomo wa madaktari.

Katika kile kinachoonyesha mpasuko huo kuchukua sura mpya, wabunge hao wamekuwa wakikwamisha miswada ya Serikali, suala ambalo siku zilizopita walikuwa wakiipitisha hata pale yanapokuwepo malalamiko kutokana kwa wananchi, kwa kile kilichokuwa kikielezwa kuwa ni ‘msimamo wa chama.’

CHANZO: MWANANCHI

Categories: