Mawaziri ambao wizara zao zilibainika kuwa na vitendo vya ubadhirifu wa mali ya umma katika ripoti hiyo ya CAG na hivyo kushinikizwa kujiuzulu ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu; Waziri wa Fedha; Mustafa Mkulo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, George Mkuchika.
Wengine ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na Waziri wa Viwanda na Biashara; Dk Cyril Chami.
Nape alisema Kamati Kuu iliyokutana jana ilipokea taarifa mbili ikiwemo uamuzi huo wa Rais kulisuka upya baraza la mawaziri kutokana na ripoti ya CAG.
“Kamati Kuu imepokea taarifa kubwa mbili, taarifa ya Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM na Kamati ya Wabunge wa CCM kwa upande mmoja na taarifa ya Kamati ya Uongozi ya Wawakilishi wa CCM kwa Bara na Zanzibar,” alisema Nape.
Alisema pamoja na taarifa hizo, Kamati Kuu ilipokea taarifa ya jinsi Rais alivyopanga kuchukua hatua za kuwawajibisha mawaziri na watendaji serikalini na viongozi wa mashirika ya umma waliobainika kuhusika na ubadhirifu ulioainishwa na CAG, kamati za kudumu za Bunge na wabunge.
“Kamati Kuu inatambua na kuheshimu haki na wajibu wa wabunge kujadili utendaji wa Serikali yao. Inapongeza juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa ripoti ya CAG inajadiliwa kwa uwazi na hivyo kuibua upungufu uliojadiliwa,” alisema Nape.
Alisema kutokana na hilo, Kamati Kuu imeridhika na imebariki uamuzi wa Rais kulisuka upya baraza la mawaziri na taasisi nyingine zilizoainishwa katika ripoti hiyo ya CAG.
“Kamati Kuu imesisitiza utekelezaji wa uamuzi huo wa Rais ufanywe mapema iwezekanavyo," alisema na kuongeza kwamba Rais anaweza kuwabadilisha mawaziri na kuwawajibisha wale ambao kutokana na uzito wa tuhuma zilizopo kwenye ripoti ya CAG, wanapaswa kuwajibishwa.
"Taarifa ya CAG ndiyo ambayo ukiipitia inaonyesha nani atawajibishwa kutokana na uzito wa tuhuma,” alisema Nape.
Alipoulizwa lini Rais amepanga kulisuka baraza hilo la mawaziri, Nape alijibu: “Wakati wowote na haraka iwezekanavyo.”
Alisema kabla ya Rais kutoa uamuzi huo, alikutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda juzi ambaye alimpa ripoti nzima ya mambo yaliyojiri bungeni.
Alisema CCM hakijatikiswa na sakata la mawaziri hao na kwamba suala lililopo mbele yao ni kuwawajibisha... “Tunajivunia tumelifikisha suala hili hapa kutokana na mfumo."
Katika Mkutano wa Saba wa Bunge la 10 mawaziri hao walishinikizwa wajiuzulu kiasi cha wabunge kumkalia kooni Waziri Mkuu, Pinda baada ya ripoti hiyo ya CAG kubainisha ubadhirifu wa fedha za umma kama ilivyowasilishwa bungeni na wenyeviti wa kamati za tatu za Bunge.
Taarifa za ndani ambazo zilipatikana baada ya kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika Dodoma zilieleza kuwa wabunge wa chama hicho waliagiza mawaziri hao wajiuzulu kutokana na kushindwa kufanya kazi zao kikamilifu.
Baada ya kikao hicho Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamekubaliana kwamba uamuzi uliofikiwa katika kikao cha wabunge wa CCM ungetolewa baadaye na Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Vyanzo vya ndani ya kikao hicho vilimnukuu Pinda akiwataarifu wabunge kwamba mawaziri wanane walitakiwa kuandika barua za kuachia nafasi zao.
Chami ajikosha
Wakati akiwa amekalia kuti kavu, Dk Chami amesema amemwandikia barua Rais Kikwete akitaka amwajibishe Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege.
Hatua hiyo ya Dk Chami imekuja baada ya wabunge kuchachamaa bungeni wakitaka Waziri Chami ajiuzulu kwa kile kinachodaiwa kumkingia kifua mkurugenzi huyo.
Licha ya shinikizo hilo, Waziri Chami alikuwa akijitetea kuwa asingeweza kumchukulia hatua mkurugenzi huyo bila kuwa na tuhuma ambazo zingempa nguvu ya kumshauri Rais.
Dk Chami alikuwa akisema kuwa hadi bunge linamalizika mjini Dodoma wiki hii alikuwa hajaiona ripoti ya Kamati Ndogo ya Bunge iliyomchunguza Ekelege ambayo ingemsaidia kupata tuhuma zinazomkabili.
“Hata ripoti maalumu ya ukaguzi iliyofanywa na CAG mpaka wabunge wanapaza sauti pale bungeni sikuwa nimeiona na Ekelege ni mteule wa Rais nitamwambia Rais amefanya nini?”
Mkurugenzi huyo mkuu anatuhumiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh18 bilioni kutokana na utendaji mbovu katika kusimamia ukaguzi wa magari yanayoingia nchini uliokuwa ukifanywa na mawakala nje ya nchi.
Dk Chami alithibitisha jana kuwa baada ya kupokea taarifa ya CAG Aprili 18, mwaka huu siku iliyofuata alimwandikia barua Rais akimuomba amsimamishwe kazi Ekelege.
Alisema amemuomba Rais afanye mambo mawili, kumpa likizo ya malipo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili na pia airuhusu Bodi ya Wakurugenzi kuteua kaimu katibu wake.
LHRC nao washinikiza
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jana asubuhi kiliitisha mkutano na waandishi wa habari na kumtaka Rais Kikwete awawajibishe mawaziri wote na watendaji wa Serikali wanaohusika katika tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema baada ya uchunguzi wa CAG kubaini kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma, ni wakati wa Rais Kikwete kufanya uamuzi wa haraka ya kuwawajibisha wote waliohusika.
“Kwa sasa tunaona wazi kwamba deni la taifa limeongezeka kutoka Sh10.5 trilioni mwaka 2010/2011 na mpaka kufikia mwaka deni hilo limeongezeka mpaka Sh14.4 trilioni na kwamba bado kuna misamaha ya kodi kiasi cha Sh1.02 trilioni jambo ambalo ni la hatari kwa uchumi wa taifa,” alisema Bisimba na kuongeza:
“Kama fedha hizi zingepata usimamizi mzuri, zingeweza kujenga kilometa 1,000 za barabara bila kuomba misaada kutoka kwa wafadhili. Jambo jingine la kushangaza ni kuwepo kwa mishahara hewa iliyolipwa kwa walimu wa vyuo vikuu 17 ambapo Serikali imepoteza Sh1.9 bilioni ambazo zingeweza kutumika kuwakopesha wanafunzi zaidi ya 1,000.”
“Tunamuomba Rais Kikwete alitilie uzito suala hili kwani kuna mambo mengi yamejitokeza wazi na kuonyesha kwamba mawaziri wake siyo watendaji makini kwani imefikia wakati wao kwa wao wanatofautiana katika uamuzi jambo ambalo sisi kama Watanzania linatushangaza.”
“Tumeshangazwa sana kuona utovu uliokithiri wa nidhamu na kukosekana kwa uwajibikaji unaofanywa na mawaziri kwani wamekuwa wakitofautiana wao kwa wao jambo ambalo hata viongozi wa juu kama Waziri Mkuu wamelinyamazia bila kuchukua hatua zozote hali ambayo inazidi kutuchanganya.”
Bisimba alizipongeza Kamati za Bunge kwa kile alichoeleza kuwa zimefanya kazi yake vizuri na kusaidia kufichua baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yamejificha.
“Tukiwa watetezi wa haki za binadamu tunajiuliza kwamba mawaziri hawa walikuwa wapi kipindi chote hicho mpaka wabunge wasimame ndipo wawajibike?” alisema.
Aliwataka wabunge kutanguliza mbele maslahi ya wananchi waliowaweka madarakani na badala ya kujali maslahi ya vyama vyao au ya mtu binafsi.
Kamati Kuu Chadema
Kwa upande wake, Kamati Kuu ya Chadema nayo ilikutana Mbezi Beach, Dar es Salaam jana ambako pamoja na mambo mengine, ilijadili namna itakavyoendesha maandamano nchi nzima kumshinikiza Rais Kikwete awawajibishe mawaziri hao.
Baadhi ya vyama vya siasa na taasisi nyingine zimeshaweka bayana msimamo wake wa kuungana na Chadema katika maandamano hayo. Hizo ni pamoja na Chama Cha Wananchi (CUF), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na baadhi ya viongozi wa dini, wasomi na wanaharakati.
CHANZO: MWANANCHI
Categories: