Mussa Juma,Samunge
MCHUNGAJI Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Ambilikile Masapila(76) ambaye, amekuwa akitoa tiba ya kikombe katika kijiji cha Samunge, amesema wateja wamepungua kwenda kwake kwa kuwa amefanyiwa hujuma.
Msongamano wa magari Samunge sasa umekwisha, kati ya mwezi Januari hadi Juni mwaka huu, magari zaidi ya 500 yalifika Samunge kwa siku na maelfu ya wagonjwa, lakini sasa chini ya magari 15 yanakwenda kwa babu kwa siku. Magari mengi yanatoka nje ya nchi.
Tofauti na miezi kadhaa, unapofika Samunge sasa idadi ya watu imepungua sana, wafanyabiashara wengi wameondoka, bei za vyakula zimerejea hali ya kawaida na kumuona Mchungaji Masapila hakuna urasimu.
Akizungumza katika mahojiano maalum jana, huku akiwa bado anaendelea kulindwa na Ofisa Usalama wa Taifa, Mchungaji Masapila alisema kupungua kwa idadi ya Watanzania wanaofika Samunge kumetokana pia na desturi ya watanzania kuoneana wivu na kuchafuana tofauti na nchi jirani.
Mchungaji Masapila licha ya kukiri kupokea taarifa za baadhi ya watu kutopona baada ya kunywa kikombe cha tiba, alisema kuna kundi la watu lilijipanga kudhoofisha huduma yake.
"Ni kweli kuna watu walikunywa kikombe hawajapona, lakini hii ni tiba ya kiimani zaidi, wengi walikiri hawakufuata masharti,"alisema Masapila.
Mchungaji Masapila alisema licha ya kufanyiwa hujuma kuna sababu kadhaa ambazo zinachangia Watanzania wengi kutofurika Samunge kwa sasa.Anasema miongoni mwa sababu hizo ni kuwa watanzania wengi wenye uwezo wakiwamo viongozi wa Serikali wamekunywa kikombe tayari na hivyo wamebaki watu masikini ambao hawawezi kugharamia safari ya kufika Samunge.
Mchungaji Masapila pia alisema baadhi ya magazeti yalipotosha tiba yake na kusababisha watu wengi kutokwenda Samunge.Awali gharama za usafiri kutoka Arusha mpaka Samunge zilikuwa kati ya Sh150,000 na 100,000 na sasa zimerejea hadi kati ya Sh50,000 na Sh20,000 pia gharama ya mahema Samunge ilikuwa kati ya Sh50,000 mpaka Sh10,000 na sasa imebaki kati ya Sh10,000 na Sh 5,000.
Uwezo wa tiba yake
Mchungaji Masapila bado alisisitiza tiba ya kikombe cha dawa inayotokana na mizizi ya mti wa Mugariga inatibu magonjwa sugu kwani Mungu hawezi kumwotesha tiba isiyo sahihi."Mimi naamini hii ni tiba kwani kuna ambao wamepona na wengine hawajapona na hii inatokana tu na kufuata masharti au imani yao,"alisema Masapila.
Kikombe bado ni kimoja hakuna kurudia
Mchungaji Masapila alisema watu ambao hawajapona, wamekuwa wakimpigia simu kutaka kurejea kupata kikombe kingine, lakini amewaeleza kuwa wanapaswa kunywa kikombe kimoja tu na ambao hawajapona wanafanyiwa maombi.
"Kikombe nimeelezwa ni kimoja tu, sasa siwezi kusema vinginevyo labda nipate maelekezo mengine kutoka kwa Mungu, ila ambao wananipigia simu naomba majina yao nay a wagonjwa ili niwaombee,"alisema Masapila.
Licha ya watu wachache kufika Samunge kwa sasa, mchungaji Masapila bado anaendelea na mpango wa ujenzi wa kituo kipya cha tiba ambacho alieleza kuoteshwa ahamie.
Masapila alisema tayari amenunua vifaa vya kupeleka maji katika eneo lipya vyenye thamani ya Sh7 milioni.
Atabiri kufurika tena watu Samunge
Mchungaji Masapila alisema bado anaoneshwa kuna watu watafurika tena Samunge kama ilivyokuwa awali.
"Hata mwanzo nilikuwa nawaeleza watu hapa kuwa wataona magari na mamia ya watu Samunge hawakuamini na wakaona pia wataona tena,"alisema Masapila.Hata hivyo, hakufafanua ni lini watu hao watafurika Samunge na watakwenda kutibiwa magonjwa gani.
Anunua magari ya kusaidia tiba akamilisha ujenzi wa nyumba yake.Katika kuhakikisha tiba ambayo inatoa inaendelea kuwa endelevu, Mchungaji Masapila amenunua gari aina ya Isuzu na Toyota Landcrusser kwa ajili ya kufuata dawa porini."Ni kweli nimenunua magari mawili ili yatoe huduma kwa kuwa siku hizi dawa zinapatikana mbali,"alisema Masapila.
Mchungaji Masapila ameishukuru Serikali kwa kuendelea kumuunga mkono na kumpa ulinzi jambo ambalo linaendelea kumpa moyo."Naishukuru sana serikali wakati wote wamenipa ushirikiano mkubwa na bado wanaendelea,"alisema Masapila.
Posted by newstz.blogspot.com
0
comments»