Imeandikwa na John Mhala
MAPIGANO yanayoendelea wilayani Ngorongoro mkoani Arusha baina ya makabila mawili ya Wasonjo na Wamasai yamechukua sura mpya na kulichanganya jeshi la polisi na serikali.
Hali ina kuwa si shwari hasa baada ya makabila hayo mawili kutuhumiana kuingiza wenzao
kutoka nchi jirani ya Kenya kuja kuwasaidia wenzao wa Tanzania.
Kwa mujibu wa wenyeji wa maeneo yanakoendelea mapigano hayo wamelieleza gazeti hili kuwa vita hiyo inakua ngumu kwa kuwa kila siku mpya kunakuwepo na sura mpya za watu wa makabila hayo wanaofika kutoa msaada kwa wenzao.
Meilodi Sikunuo, mmoja wa wakazi wa maeneo hayo alisema kuwa kuna wasiwasi mkubwa
juu ya madai hayo kutokana na ukweli kuwa wengi wa wakazi wa makabila hayo wanafahamika
lakini kwa sasa kumekuwa na wimbi la wageni siku hadi siku.
Aidha, alisema pamoja na juhudi za jeshi la polisi pamoja na serikali ya wilaya hiyo kutaka
kuwapatanisha zimekuwa zikishindikana kutokana na somo wanalolitoa kwa makabila hayo
mawili kutoeleweka kwa kuwa wageni hao wamekuwa hawahudhurii vikao hivyo kwa kuhofia kugundulika.
Sikunuo aliongeza kuwa kinachopaswa kwa sasa kwa vyombo hivyo vya dola pamoja na
serikali ni kudhibiti katika maeneo ya mipakani ili kuzuia uingiaji wa watu wageni kutoka
Kenya kwa kuwa kushindikana kudhibiti hilo kutaendelea kuruhusu mapigano hayo kuendelea.
Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Japhet Loitoki alishauri serikali pamoja na jeshi la polisi njia sahihi ya kumaliza mapigano hayo ya kugombea eneo hilo kuwa ni kujenga
mradi wowote katika eneo hilo ili lisiwe linatumiwa na pande yoyote.
Alisema katika eneo hilo kuna uhaba wa huduma mbalimbali ikiwemo ya shule pamoja na zahanati hivyo ingekuwa busara kama ungefanyika mradi mmojawapo baina ya hiyo ambayo
pia ingefurahiwa na wananchi wote na kusahau suala la mapigano yanayosababisha mauaji na ulemavu.
CHANZO: HABARI LEO
Categories:
Loliondo