Showing posts with label mafuriko. Show all posts
Showing posts with label mafuriko. Show all posts

MVUA YA ZUA BALAA MBEYA NA KILIMANJARO

Lori lenye namba za usajili T190 AKW likiwa limetumbukia mtoni baada ya kusombwa na maji katika daraja la mto Loobuko kati ya Makuyuni na Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani Arusha kutokana na mvua kubwa zinazonyesha mkoani humo. (Picha na Prisca Libaga).


******

MVUA kubwa na upepo iliyonyesha usiku wa kuamkia jana katika mikoa ya Mbeya na Kilimanjaro, kwa zaidi ya saa tano imesababisha vifo na kuwaacha baadhi ya wakazi wake wakihaha kutafuta sehemu ya kujihifadhi baada ya nyumba zao kuezuliwa.

Kutokana na mvua hiyo, watu wawili wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa vibaya, huku familia 222 zikiachwa bila makazi.

Watu hao wawili walifariki dunia mkoani Kilimanjaro ambako mvua iliyokuwa imeambatana na upepo, ilinyesha katika kijiji cha Mamba kilichoko kwenye Kata ya Msangeni.

Mvua hiyo iliyonyesha kwa takribani saa 13, imesababisha kifusi cha mlima kuangukia nyumba ya Musa Mruma na kusababisha kifo cha Anna Keshi (20) ambaye ni mama mzazi wa mtoto Easter Ally ambao wote walipoteza maisha.

Diwani wa kata ya Msangeni, Fihirini Mvungi, alisema kuwa mvua hiyo ilinyesha usiku wa kumkia juzi na kusababisha kifusi hicho cha udongo ambacho kilifunika nyumba hiyo.

“Nyumba za huku ziko milimani, huku ukitaka kujenga nyumba unakata kipande cha mlima ndio uweze kujenga, sasa mvua ilivyonyesha ukuta wa mlima umeanguka na kufunika nyumba na kusababisha vifo,”alisema.

Diwani huyo alisema mbali na kusababisha vifo, mvua hiyo pia imesababisha nyufa kwenye nyumba nyingi kutokana na nyumba hizo kuangukiwa na udongo.

"Mvua hiyo pia imeharibu mashamba na miundombinu ya barabara hususan barabara ya Kikweni- Zahanati, imeharibika vibaya sana," alisema Diwani huyo.

Shemeji wa marehemu, Charema Mruma alisema siku ya tukio majira ya saa 8:00 usiku wakiwa wamelala huku mvua kubwa ikinyesha, gafla walisikia kitu kimeanguka. Walipotoka na kuangalia wakagundua kuwa nyumba aliyokua amelala shemeji yake, imeangukiwa na kifusi.

"Hatukuwa na chakufanya kutokana na mvua kuwa nyingi. Asubuhi mvua ilipungua na walitoa taarifa polisi ambao nao walifika na kusaidiana na wananchi kufukua na kufanikiwa kutoa miili hiyo," alisema.

Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Usangi ikisubiri kusafirishwa kwenda wilayani Same kata ya Kisiwani, kwa ajili ya mazishi.


Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Athuman Mdoe alithibitisha maafa hayo na kwamba alikuwa njiani kuelekea kwenye eneo la tukio hivyo taarifa zaidi atatoa taarifa baadaye.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma naye amethibitisha tukio hilo.

Wakati hayo yakiendelea wilayani Mwanga, mkoani Mbeya zaidi ya familia 88 zilizoko kwenye kata ya Galula Wilayani Chunya, hazina makazi kufuatia kimbunga na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha watoto watatu wa familia moja walijeruhiwa vibaya.

Waliojeruhiwa wamejulikana kwa majina ya Nkwimba Rozaria, Simba Rozalia na Sayi Rozalia. Wamelazwa katika Hospitali Teule ya Mwambani.

Mvua hiyo kubwa ambayo ilinyesha juzi ikiwa imeambatana na upepo mkali na kuezua mapaa na nyumba kubomoka, ilidumu kwa muda wa saa moja mfululizo.

Vitongoji vilivyokumbwa na maafa hayo ni Galula ‘B’, Galula ‘A’, Kasilo ‘A’, Kasilo ‘B’, Galula ‘C’, Muhimbili na Ilembo. Vitongoji hivyo vipo katika Kijiji cha Galula na kwamba kaya 37 zenye wakazi 222 hazina mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuanguka

Kufuatia maafa hayo, Mbunge wa Jimbo la Songwe, Philipo Mulugo ametoa msaada wa magunia 100 ya mahindi na zaidi ya Sh 1.3 milioni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi hao.

Habari hii imeandaliwa na Rehema Matowo na Fina Lyimo, Mwanga na Hawa Mathias, Mbeya (MWANANCHI)
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

Tanga yakumbwa na mafuriko

Imeandikwa na Anna Makange, Tanga


BAADHI ya wakazi wanaoishi kwenye maeneo ya mabondeni hususan katika mitaa ya Kata ya Mabawa katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, wamekumbwa na mafuriko kutokana na mvua iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo mwishoni mwa wiki.

Mvua hiyo iliyofululiza kwa zaidi ya saa 40 usiku na mchana, ilileta hofu si tu kwa wakazi hao wa maeneo ya mabondeni, bali hata katika maeneo ya katikati ya Jiji na kusababisha barabara kadhaa kutopitika kwa muda baada ya maji kujaa kutokana na mifereji kuzidiwa nguvu huku mingine ikiwa imezibwa na taka ngumu.

Wakazi wa kata hiyo, Mariam Adam na Sofia Waziri ambao wanaishi Magaoni, walisema mvua hiyo imesababisha usiku wakeshe kwa shaka ya kuingiliwa na maji nyumbani mwao.

Sofia alisema walilazimika kuvunja shughuli za uzalishaji badala yake walibaki nyumbani ili kujaribu kuchota maji hayo bila mafanikio huku wengine wakijitahidi kuweka vizuizi katika maeneo kadhaa ili kupunguza kasi ya mafuriko kuelekea kwenye makazi yao.

“Mafuriko hutokea kila mwaka zinaponyesha mvua maji mengi huingia kwenye mitaa yetu huku na hali hii tumebaini inasababishwa na uzembe wa baadhi ya watendaji katika Halmashauri hasa wanaohusika kushughulikia miundombinu ya mifereji midogo na mikubwa inayotiririsha maji taka na maji ya mvua kuelekea baharini kwa sababu imeziba kutokana na kujaa mchanga na taka ngumu,” alisema.

Kwa upande wake, mkazi mwingine, Saidi Ally alidai kuwa tatizo kubwa linatokana na viongozi kutowashirikisha wananchi wa maeneo hayo hasa vijana ambao hawana ajira rasmi kwenye kazi za kusafisha mifereji midogo inayoelekeza maji kwenye mifereji mikubwa kuelekea baharini, hatua inayowafanya wajione kwamba hawahusiki kwa kuwa wapo vibarua walioajiriwa kwa shughuli hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwembeni ‘B,’ Ernest Mussa alisema uzoefu unaonesha kuwa nyakati za kiangazi hakuna mtendaji anayejihusisha na usafi wa mifereji hadi maafa yanapotokea ndipo watendaji wa ngazi tofauti katika Halmashauri ya Jiji hujitokeza na vifaa hafifu ambavyo havina uwezo wa kukabiliana na mafuriko ambayo sasa yamekuwa kero kwao kila inaponyesha mvua.

Alisema ni vema mkakati endelevu wa kusafisha mifereji ya maji taka na ya mvua hasa ile mikubwa na midogo ikaendelea kuimarishwa wakati wote ili kusaidia kupunguza hofu ya madhara na kero zisizo za lazima zinazoendelea kusababisha mafuriko kwa wakazi wa Magaoni na Mwembeni.

Chanzo: Habaarai leo
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»