Tanga yakumbwa na mafuriko

Imeandikwa na Anna Makange, Tanga


BAADHI ya wakazi wanaoishi kwenye maeneo ya mabondeni hususan katika mitaa ya Kata ya Mabawa katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, wamekumbwa na mafuriko kutokana na mvua iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo mwishoni mwa wiki.

Mvua hiyo iliyofululiza kwa zaidi ya saa 40 usiku na mchana, ilileta hofu si tu kwa wakazi hao wa maeneo ya mabondeni, bali hata katika maeneo ya katikati ya Jiji na kusababisha barabara kadhaa kutopitika kwa muda baada ya maji kujaa kutokana na mifereji kuzidiwa nguvu huku mingine ikiwa imezibwa na taka ngumu.

Wakazi wa kata hiyo, Mariam Adam na Sofia Waziri ambao wanaishi Magaoni, walisema mvua hiyo imesababisha usiku wakeshe kwa shaka ya kuingiliwa na maji nyumbani mwao.

Sofia alisema walilazimika kuvunja shughuli za uzalishaji badala yake walibaki nyumbani ili kujaribu kuchota maji hayo bila mafanikio huku wengine wakijitahidi kuweka vizuizi katika maeneo kadhaa ili kupunguza kasi ya mafuriko kuelekea kwenye makazi yao.

“Mafuriko hutokea kila mwaka zinaponyesha mvua maji mengi huingia kwenye mitaa yetu huku na hali hii tumebaini inasababishwa na uzembe wa baadhi ya watendaji katika Halmashauri hasa wanaohusika kushughulikia miundombinu ya mifereji midogo na mikubwa inayotiririsha maji taka na maji ya mvua kuelekea baharini kwa sababu imeziba kutokana na kujaa mchanga na taka ngumu,” alisema.

Kwa upande wake, mkazi mwingine, Saidi Ally alidai kuwa tatizo kubwa linatokana na viongozi kutowashirikisha wananchi wa maeneo hayo hasa vijana ambao hawana ajira rasmi kwenye kazi za kusafisha mifereji midogo inayoelekeza maji kwenye mifereji mikubwa kuelekea baharini, hatua inayowafanya wajione kwamba hawahusiki kwa kuwa wapo vibarua walioajiriwa kwa shughuli hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwembeni ‘B,’ Ernest Mussa alisema uzoefu unaonesha kuwa nyakati za kiangazi hakuna mtendaji anayejihusisha na usafi wa mifereji hadi maafa yanapotokea ndipo watendaji wa ngazi tofauti katika Halmashauri ya Jiji hujitokeza na vifaa hafifu ambavyo havina uwezo wa kukabiliana na mafuriko ambayo sasa yamekuwa kero kwao kila inaponyesha mvua.

Alisema ni vema mkakati endelevu wa kusafisha mifereji ya maji taka na ya mvua hasa ile mikubwa na midogo ikaendelea kuimarishwa wakati wote ili kusaidia kupunguza hofu ya madhara na kero zisizo za lazima zinazoendelea kusababisha mafuriko kwa wakazi wa Magaoni na Mwembeni.

Chanzo: Habaarai leo

Categories: ,