Imeandikwa na Agnes Haule
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Omari Mrisho (25) baada ya kupatikana na hatia ya ubakaji, ulawiti na kumgeuza mtoto wa miaka tisa kuwa mkewe kwa kipindi cha miezi miwili.
Hukumu huyo ilitolewa juzi na Hakimu Nuruprudensia Nasari, ambaye alisema mahakama imeamua kutoa adhabu hiyo kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwake na vijana wengine wenye tabia kama ya mshitakiwa.
Hakimu Nasari alisema kutokana na ushahidi ulitolewa mahakamani hapo, hana pingamizi la kutoa adhabu hiyo ya miaka 30 kwa mshitakiwa kufuatia kitendo chake cha kinyama kwa mtoto huyo.
Akitoa ushahidi mahakamani hapo, mshitakiwa huyo alidai alikuwa akikaa na mtoto huyo kama mtoto wake akimlea, lakini alipohojiwa zaidi alishindwa kuthibitisha kuwa huyo ni mtoto wake kivipi.
Ushahidi uliotolewa alipohojiwa mtoto huyo, alidai kukaa na kijana huyo kwa muda huo kama mumewe baada ya yeye (mshitakiwa) kutoa mahari kwa dada wa mtoto huyo ambaye hakumtaja na kudai kuwa mshitakiwa alikuwa akimuingilia sehemu zote za maumbile na kumsababishia maumivu makali.
Awali akisoma maelezo ya mashitaka hayo, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Lameck Webi alidai mahakamani hapo kuwa Mrisho alitenda kosa hilo Juni 12, 2010 saa 12 asubuhi katika eneo la New- land katika Kata ya Mikese.
Alidai mshtakiwa huyo huku akijua kufanya hivyo ni kosa alimlawiti na kumbaka mtoto huyo na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.
Categories: