Imeandikwa na Veronica Mheta, Arusha
POLISI mkoani Arusha wamekwenda wilayani Ngorongoro kufanya uchunguzi wa chanzo cha mapigano kati ya kabila la Wamasai na Wasonjo yaliyosababisha mauaji ya watu wawili.
Askari hao walioondoka jana wakiwa na magari mawili, wanatarajiwa kuonana na viongozi wa makabila hayo ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza awali.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Leonard Paul alisema mapigano hayo yalitokea juzi ambapo vijana wawili; Lifadi Gendiri (19) na Mletwi Ngeswai (15) wote wakazi wa Kijiji cha Mgongo Mageri walikufa na miili yao ikahifadhiwa Hospitali ya Misheni ya Wasso wilayani Ngorongoro.
Mapigano hayo yanadaiwa kusababishwa na baadhi ya vijana wa makabila hayo kwenda kulisha mifugo yao kwenye eneo ambalo makabila hayo yalikubaliana awali yasitumike kutokana na mgogoro wa ardhi.
Lakini Kamanda Paul alisema mapigano hayo yalianza juzi majira ya saa tano asubuhi baada ya vijana kadhaa wanaoaminika kuwa ni Wamasai wakiwa na bunduki inayohisiwa kuwa SMG, kuwavamia vijana wa Kisonjo katika eneo la Kisiansui linagombewa na jamii hizo kwa muda mrefu na kuwaua kwa risasi.
Kamanda Paul alisema mara baada ya taarifa za mauaji hayo kufika kwa Wasonjo, mamia ya vijana wa Kisonjo walitangaza vita na kuanza kwenda katika vijiji vya Wamasai ambako mpaka sasa hakuna taarifa zilizopatikana kutoka vijiji hivyo kutokana na ugumu wa mawasiliano.
Alisema mara baada ya mapigano hayo watu mbalimbali walikimbia kwenye nyumba zao kutokana na silaha za moto kutumika kwenye mauaji hayo na kuongeza kuwa tatizo lililosababisha mauaji hayo ni mgogoro wa ardhi baina ya makabila hayo.
Kutokana na mgogoro huo, polisi wamekwenda eneo hilo kufanya uchunguzi zaidi pamoja na kushauri uongozi wa vijiji na viongozi wa kimila kujadili suala hilo kwa kina na kutoa ufumbuzi ili vifo vingine visitokee.
Katika tukio lingine, mlinzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Arusha, Maombi Lusanda (48) anashikiliwa Polisi kwa tuhuma za kumuua Godlucky Chokoraa (29) eneo la Sanawari katika mgahawa wa Grocella.
Kwa mujibu wa tuhuma hizo, Lusanda alikuwa akinywa pombe katika mgahawa huo saa 7 za usiku na alipotoka kidogo kwenda msalani na kurudi alipokuwa akinywea pombe yake, alikuta watu wanazozana na alipoingilia ugomvi alijikuta akimpiga risasi Chokoraa.
Kamanda Paul alisema Lusanda alitumia bastola yenye namba za usajili T 394-09D0031 ambayo imekamatwa na mwili wa Chokoraa umehifadhiwa katika Hospitali ya Mount Meru.
CHANZO: HABARI LEO
Categories: