WAKATI Taifa Stars ikiondoka jana jioni kwenda Morocco kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Afrika mwakani, mabeki Juma Said 'Nyosso' na Nadir Haroub Cannavaro wamejumuishwa katika safari hiyo. Cannavaro ambaye ameziba nafasi ya Victor Costa aliyeachwa kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyonga, amekabidhiwa jukumu la unahodha badala ya Shadrack Nsajigwa aliyeumia.
Awali, Nyosso alikuwa katika hatihati ya kuikosa safari hiyo kutokana na kuugua malaria huku Cannavaro ambaye amekuwa majeruhi kwa muda mrefu akiitwa dakika za mwisho kuokoa jahazi.Stars itaikabili Morocco Jumapili, Oktoba 9 katika mchezo huo muhimu utakaochezwa kwenye mji wa Marakhech saa moja jioni. Mbali ya Costa, kocha Jan Poulsen pia amemwacha kiungo wa Tanzania anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada, Nizar Khalfan na mlinda mlango Shaaban Kado wa Yanga.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana,ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Boniface Wambura alisema kuwa licha ya Cannavaro kuziba pengo la Costa, pia atakuwa nahodha wa timu hiyo wakati wa mechi hiyo. "Kimsingi, Poulsen amemteua Cannavaro kuchukua nafasi ya Costa ambaye ni majeruhi ,pia ndiye atayekekuwa nahodha wa timu wakati wa mechi hiyo. Wambura alisema kikosi hicho kiliondoka na wachezaji 20. Aliwataja wachezaji kuwa ni pamoja na makipa Juma Kaseja na Shabani Dihile. Mabeki - Juma Jabu,Idrisa Rajab,Juma Nyosso,Aggrey Morris, Nassoro Said' Chollo', Erasto Nyoni na Cannavaro.
Viungo ni: Nurdin Bakari, Jabir Aziz,Ramadhan Chombo' Redondo',Henry Joseph, Shaaban Nditi na Hussein Javu na Abdi Kassim.
Washambuliaji: Mrisho Ngassa,Athuman Machuppa,Mbwana Samatta na Danny Mrwanda.
Ofisa habari huyo wa TFF alisema kuwa kikosi cha Taifa Stars kitarejea nchini Oktoba 11.
Categories: