Tunaongoza kwa kuwa na Amani Afrika

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige amewahakikishia wageni walioko nchini na wanaojiandaa kuitembelea kuwa Tanzania bado inaendelea kuongoza katika Bara la Afrika kwa kuwa na amani. Aidha, amesema Tanzania imeongeza udhibiti wa hali ya usalama ili kuhakikisha kuwa wageni na wananchi wanakuwa salama. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Maige alisema anaamini kuwa matukio yaliyotokea mbali kabisa na mipaka ya nchi, hayawezi kuwa sababu ya kuogopa na kukatisha safari za kuja Tanzania. Alisema Tanzania ni kisiwa cha amani na nchi imenuia kudumisha sifa hiyo nzuri, ingawa kumekuwapo na taarifa za kuwataka wasafiri wanaotembelea Mashariki mwa Afrika wachukue tahadhari. Tahadhari hiyo imetolewa kutokana na vitendo vya kuteka nyara watalii vilivyotokea upande wa Kaskazini, mbali na mipaka ya Tanzania na kushuhudia hofu inayoendelea kukua kuhusu usalama wa watalii wanaotembelea Mashariki mwa Afrika.

Jambo hilo na mengine yote yatakayojitokeza yatadhibitiwa kikamilifu ili kudumisha amani Tanzania ambayo ndio urithi pekee tulioachiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na urithi huu umesaidia nchi kwa kipindi chote tangu 1961 hadi sasa kuendelea kupokea wageni mbalimbali wanaoitembelea nchi kwa lengo la utalii, biashara na uwekezaji. Ni jukumu la kila raia wa Tanzania kuhakikisha kudhibiti na kutoa taarifa juu ya vitendo vyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani ili kudumisha amani ya nchi yetu.

Categories: