Geofrey Nyang’oro
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitaka Serikali kutolipa deni la Sh111 bilioni Kampuni ya kufua Umeme ya Dowans na kuonya kuwa endapo itaendelea na mkakati huo kitapinga kwa maandamano ya nchi nzima. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mnyika, alisema hawakubaliani na malipo hayo kwa sababu mikataba yote iliyoliingiza taifa kwenye deni hilo ni ya kifisadi.
Chama hicho kimetoa mwezi mmoja kwa serikali kuwachukulia hatua watu waliohusika kuingia mikataba mibovu ikiwa ni pamoja na kuwafilisi mali zao.Alisema pamoja na kutoa muda huo, bado chama hicho kitakuwa tayari kuchukua hatua wakati wowote kikipata taarifa za Serikali kuanza mchakato wa kulipa deni hilo.
Kauli ya Chadema imekuja siku moja baada ya wanaharakati wa masuala ya sheria na utawala bora kutoa tamko na kuanza kuhamasisha wananchi kuandamana kuishinikiza Serikali kuwachukuliwa hatua watu wote waliosababisha nchi kuingia kwenye mkataba na Richmond ambayo baadaye ilirithiwa na Dowans. Mnyika alisema kuwa, kama Serikali inataka kulipa deni hilo itaifishe mali za watu waliohusika kuingia mkataba huo badala ya fedha za walipa kodi.
“Kama Serikali inadhamira ya kulipa deni hilo, iwachukulie hatua watu wote waliohusika kujadili mikataba mibovu ya Kampuni ya Richmond na Dowans, itaifishe mali zao na fedha hizo zitumike kulipa deni hilo,” alisema Mnyika.
“Tumewaita ili umma ujue msimamo wa chama (Chadema) juu ya malipo ya Dowans, hatupo tayari kuona fedha za Watanzania zinatumika kulipa Dowans iliyorithi mkataba wa kifisadi, tumefikia hatua hiyo sababu Serikali wakati wote imeshindwa kuchukua hatua thabiti dhidi ya ufisadi,” alisema Mnyika.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema kama Serikali ina huruma dhidi ya Dowans na kuona umuhimu wa kulipa deni hilo, inapaswa kuchukua hatua za kuwafilisi watu walioshiriki kuingia mikataba mibovu na fedha zao zitumike kulipa deni hilo.
Msimamo wa Chadema umekuja kufuatia uamuzi uliotolewa hivi karibuni na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kuridhia malipo ya fidia ya Sh111 bilioni kwa Dowans baada ya kusajili tuzo iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya Kibiashara (ICC).
Alisema wahusika katika sakata hilo la mikataba mibovu wanajulikana na kwamba kitendo cha Serikali kushindwa kuwachukulia hatua ni ishara kuwa Serikali inakumbatia ufisadi.
“Zipo kesi za uhujumu uchumi zinazohusu majengo pacha ya (BOT), lakini tunashangaa hadi leo wahusika walioingia mikataba mibovu ya kampuni za Richmond, Dowans bado wapo mitaani licha ya kuingizia taifa hasara ya mabilioni ya fedha,” alisema Mnyika na kuongeza;
“Tunaitaka Serikali kuchukua hatua kama haitachukua hatua dhidi yao na kuendelea na mpango wao wa kuilipa Dowans, Chadema tutaunganisha nguvu ya umma ili Watanzania wahusike katika kupinga malipo hayo ya kifisadi.”
Mnyika alihoji sababu za Serikali kuona umuhimu wa kulipa deni hilo wakati wapo wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliyovunjika mwaka 1977 wakihangaika bila mafanikio kwa miaka mingi sasa. “Madai ya walimu pekee ni Sh29 bilioni, wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki hadi leo wanahaha kufuatilia madeni yao, kupanda kwa gharama za maisha, bei ya mafuta, Serikali inayosema haina hela leo inailipa Dowans mabilioni ya fedha, tutaunganisha nguvu ya umma kupinga hilo hadi kieleweke,” alisisitiza Mnyika.
Alimtaka Rais Jakaya Kikwete kusoma alama za nyakati na kutumia nafasi yake kama kiongozi wa taifa kufanya uamuzi sahihi juu ya sakata hilo, alilodai kuwa linaweza kuifikisha Serikali ya CCM katika wakati mgumu.
Alisema katika hilo ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia inaingia katika tuhuma hizo kwa kuishauri Serikali vibaya juu ya mikataba hiyo ambayo alisema imeweka masharti magumu dhidi ya wananchi wa Tanzania.
“Mkataba wa Richmond umewekwa kipengele kinachosema kama mmoja atakiuka kesi yake itasikilizwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Migogoro ya Kibiashara ya (ICC) na hukumu ikitolewa hakuna kukataa rufaa popote,” alisema Mnyika na kuongeza:
“Ikiwa viongozi wetu wanaoingia mikataba kama hii tunajiuliza wanalitakia taifa letu mema? Hawa ndio tuliowapa dhamana ya kutuongoza kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya nane?” alihoji Mnyika.
Alisema kutokana na hali hiyo, Chadema itatumia nguvu ya umma kukataa mikataba hiyo na kuueleza umma wa kimataifa kuwa wale tuliowapa dhamana ya kutuongoza wanashirikiana na wezi kutuibia. Sakata la Dowans limekuwa mzimu unaowatafuna wanasiasa tangu lilipoibuka mwaka 2008 wakati huo ikijulikana kama Richmond.
Bunge liliunda Kamati Teule iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela Dk Harrison kuchunguza uhalali wa kampuni hiyo ya kufua umeme na kubainika kuwa ni yakitapeli.
Categories: