Dk Mwakyembe aanza matibabu

Na Patricia Kimelemeta

SAA chache baada ya kufikishwa hospitali ya Appolo nchini India, Naibu waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe tayari amechukuliwa vipimo vya awali, kubaini matatizo yanayomkabili.Dk Mwakyembe aliondoka nchini juzi saa 6:00 mchana na ndege ya Qatar Airways baada ya hali yake kiafya kuzidi kuzorota.

Naibu waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Kyela, amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya kuvimba mwili pamoja na muwasho na hali hiyo ilifikia katika hatua ya juu zaidi mwishoni mwa wiki ndipo juzi, wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, iliamua kumpeleka hospitali ya Appolo kwa matibabu zaidi.Lakini jana, akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam Msemaji wa familia ambaye pia ni Mbunge wa Lupa,Victor Mwambalaswa alisema Dk Mwakyembe anaendelea vizuri kwani tangu jana alipowasilini hospitalini hapo alianza kupatiwa vipimo.

“Nimewasiliana naye asubuhi ya leo (jana), yeye na mkewe na kwamba wameniambia tayari ameanza kupatiwa vipimo vya awali juu ya ugonjwa wake ili aweze kuendelea na matibabu,” alifafanua Mwambalaswa.

Aliongeza kwamba, kutokana na hali hiyo Dk Mwakyembe hawezi kurudi nchini mpaka atakapopona au kupewa ruksa na madaktari.Mwambalaswa aliwataka wananchi waendelee kumuombea ili aweze kupata matibabu na kurudi nchini, ili aweze kuendeleza shughuli zake za ujenzi wa taifa.

“Dk Mwakyembe ni mchapakazi mzuri, ninaamini atakaporudi ataweza kuendelea na shughuli zake kama kawaida kwani sasa hivi tayari ameanza kupatiwa matibabu, hivyo basi tuendelee kumuombea,” alifafanua Mwambalaswa.

Taarifa mchanganyiko
Dk Mwakyembe alikimbizwa India kwa matibabu zaidi baada ya hali yake ya afya kuzidi kuzorota, hiyo ni kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya ngozi yaliyosababisha kuharibika kwa ngozi yake.

Taarifa za kuumwa kwa Dk Mwakyembe zilisambaa zaidi mwishoni mwa wiki, baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya na Jumamosi mwishoni, Rais Jakaya Kikwete, alimtembelea nyumbani kwake Kunduchi Beach, jijini Dar es Salaam.Hata hivyo, juzi Jumapili, baada ya hali ya naibu waziri huyo kuzidi kuwa mbaya,Serikali ililazimika kumkimbiza nchini humo ili aweze kupata matibabu zaidi.

Kauli yake kabla kuondoka
Kabla ya kuondoka, Dk Mwakyembe aliliambia gazeti la hili kwamba alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya mwili kuvimba.Hata hivyo, mkewe Dk Mwakyembe, Linah alisema kwamba mumewe alianza kusumbuliwa na ugonjwa huo miezi mitatu iliyopita.

“Alianza kuugua muda mrefu kidogo kama miezi mitatu iliyopita, hali hiyo ilikuwa inatokea na kupotea hadi sasa ambapo hali imekuwa mbaya,” alisema.

Washirika wake wa karibu
Hata hivyo, wakati taarifa za baadhi ya madaktari zikionyesha Dk Mwakyembe anasumbuliwa na kisukari, baadhi ya watu wake wa karibu wanaamini maradhi hayo ni sumu.Kwa mujibu wa washirika hao wa karibu wa Dk Mwakyembe, uthibitisho wa sumu ulitolewa na mmoja wa madaktari maarufu nchini ambaye alimweleza bayana kwamba alikuwa na sumu mwilini.

Vyanzo hivyo vilisema kwamba, Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alikuwa akipata matibabu, alielezwa kusumbuliwa na sukari."Mtu akishika ngozi inapepetuka na kutoa unga, akishika nywele zina nyonyoka, sasa hii ni hatari," alifafanua mmoja ya watu walio karibu naye.

Alianza kuumwa taratibu
Vyanzo vya habari vinasema kuwa Dk Mwakyembe alikuwa akiumwa taratibu na wakati mwingine alilazimika kumeza vidonge hali hiyo inapomjia.

"Alikuwa anaumwa taratibu, sasa wakati mwingine hali hii inapomjia alikuwa akilazimika kumeza vidoge ili kutuliza," vyanzo hivyo vilidokeza.Aliongeza kwamba, awali, hali hiyo ilipokuwa ikimjia mwili wake ulikuwa ukikakamaa na baada ya kunywa vidonge hutulia.

Chanzo: Mwananchi

Categories: