Wanaojiunga vyuo vikuu wazidi kuilalamikia HELSB

Na Godfrey Moshi


Malalamiko ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kuhoji utaratibu unaotumiwa na Bodi ya Mikopo nchini (HELSB) katika utoaji wa mikopo hiyo, yanaendelea kuitesa bodi hiyo, baada ya wafanyakazi wanaojiunga na vyuo hivyo kudai kuwa wanabaguliwa.
Wanafunzi waliojiunga na Chuo Kikuu cha Tumaini-Iringa, wakitokea kazini, wanadai kwamba serikali pamoja na HELSB, haijaweka wazi haki ya kada hiyo kupata mikopo.
Hayo yalielezwa jana na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini-Iringa (IUCo) walipokuwa wakizungumza na Uongozi wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho. Mmoja wa wanafunzi hao, Elizabeth Kabanga, alisema kuwa hawaoni kwa nini HELSB haiwajumuishi wafanyakazi wanaojiunga na vyuo hivyo wakitokea kazini ilihali imeundwa kwa ajili ya kutoa udhamini wa masomo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.
“Ifike mahali wafanyakazi wanaojiunga na vyuo vya elimu ya juu na sisi tupewe mikopo, hakuna mantiki ni kwa nini tusipewe mkopo wakati bodi imeundwa kwa ajili hiyo…Kwa hili ni kama tunabaguliwa,” alisema. Emanuel Gervas, alisema kinachotakiwa kwa sasa ni kuishauri serikali kuiboresha zaidi bodi hiyo ili kuondoa malalamiko ya aina hiyo.
Rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho (TUSO-IUCo), Method Kagoma, aliwataka wanafunzi wapya wa chuo hicho kuwa watulivu kwa kuwa kila mmoja atapata haki yake. “Huu utaratibu uliowekwa na Serikali kuhusu mikopo ni mzuri sana na mimi naamini kwamba kila anayestahili kupata haki yake ataipata, niwaombe muwe watulivu,” alisema.
Kuhusu utovu wa nidhamu na mmomonyoko wa maadili kwa wanafunzi,Rais huyo aliwaeleza wanachuo hao kwamba hata kuwa tayari yeye na serikali yake hawatavumilia utovu wa nidhamu na badala yake atachukua hatua kwa yeyote atakayevunja sheria za chuo hicho.
CHANZO: NIPASHE

Categories: