JK aagiza chakula cha ziada kiingizwe sokoni


Rais Jakaya Kikwete, amezielekeza taasisi zinazohusiana na chakula nchini kutumia wingi wa ziada ya chakula ulioko nchini kwa sasa kukiingiza katika masoko ya mijini ili kupunguza bei ya chakula na pia kuunga mkono jitihada za maskini wa mijini kupata chakula kwa bei nafuu.

Aidha, Rais Kikwete, amezitaka taasisi hizo kuongeza kasi ya ununuzi wa chakula, na hasa mahindi kutoka kwa wakulima ili kuwawezesha kuwa na nafasi ya kuweka mazao mapya yanayoanza kuvunwa sasa.

Kadhalika, amezielekeza taasisi hizo kuweka mfumo rasmi wa kuwaruhusu wafanyabiashara nchini kuuza chakula cha ziada katika nchi jirani bila kuathiri upatikanaji wa chakula ama kusababisha upungufu nchini.

Alitoa maagizo hayo juzi jioni, alipokutana na mawaziri na watendaji wa serikali ambao taasisi zao zinahusika na upatikanaji, uuzaji na usambazaji wa chakula nchini.

Miongoni mwa walioshiriki katika kikao hicho kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Wengine ni Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo pamoja na maofisa wa Mamlaka ya Taifa ya Chakula cha Akiba (NFRA).

Kuhusu ununuzi zaidi wa chakula, Rais Kikwete alisema: “Bado kiko chakula kingi mikononi mwa wakulima....Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa zinachukuliwa hatua za haraka kukinunua na kukihifadhi katika maghala ya SGR.” Kuhusu uuzaji wa chakula kwa nchi jirani na hata kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), alisema ufanywe utaratibu wa kuwawezesha wafanyabiashara nchini kuruhusiwa kukiuza cha ziada kwa nchi jirani kwa utararibu maalum na ulio wazi.

Categories: