Rostam Aziz (picha kutoka maktba)
Na Moses Mabula, Tabora
WAKATI vumbi la aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Igunga, Bw. Rostam Azizi (CCM) halijatua, makundi yamezidi kukitafuna Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa
baada ya wananchama takribani 800 wa chama hicho kudaiwa kukihama chama hicho na kutimkia upinzani, Majira limeelezwa.
Wanachama hao wanadaiwa kuhama ikiwa ni wiki moja tangu mabalozi 19 wa chama hicho kujitoa wakilalamikia mgao wa fedha zilizotolewa kwa ajili ya uchaguzi wa Jimbo la Igunga.
Taarifa zilizolifikia Majira jana, zilisema wengi wa wanachama hao wanatoka vijijini husasuni Kata za Ufuluma, Ibiri na Usagali, huku ikielezwa kwamba vijana wengi waliokata tamaa ya maisha kutoka UVCCM mjini Tabora ni miongoni mwa wanachama wapya.
Baadhi ya vijana mjini hapa walionekana wakisaka ofisi za CHADEMA ili wajiunge na chama hicho, sababu inayoelezwa wazi ni kucheleweshewa malipo yao ya tumbaku kwa takribani miezi 5 sasa, huku habari za ndani zikisema kuna watu wanaosadikiwa kumuunga mkono Bw. Aziz ndio wanaoshawishi na kuratibu mpango huo.
Akizumngumza na majira mjini hapa mpashaji wa habari hizi
ambauye ni mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Uyui na mjumbe wa Baraza la Vijana UVCCM wilaya hiyo aliyekataa jina lake kuandikwa
gazetini kwa kuhofia usalama wake, alisema hatua hiyo imetokana na
kuibuka upya kwa makundi ndani ya chama hicho.
Alisema, "tangu uchaguzi mdogo wa Igunga umalizike, chama chetu naona kinarudia hali yake ile ya makundi ndani ya chama."
Alisema hali hiyo inasababishwa na viongozi wao wa mkoa na wilaya kuendekeza kupigana vijembe vya kijinga hadharani.
“Mimi naunga mkono kauli ya Mwenyekiti wetu (wa UV-CCM), Bw. Beno Malisa aliyoitoa Arusha kwamba ni wakati umefika kwa Vijana wa CCM tupewe fursa ya kutoa maamuzi katika vikao vya juu ndani chama na hata serikali.
Alieleza kuwa “matokeo ya kura ilizopata CCM Igunga hazifanani na nguvu za CCM kama ninavyoifahamu, na hapa natoa onyo iwapo viongozi wataendelea kutoa hotuba za taarabu majukwaani na kuacha kutoa
za msingi, wanachama wengi zaidi watatuhama," alisema.
“Angalia tu mwenyewe, juzi tu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Bw. Hassan Wakasuvi pale sanamu la Mwalimu Nyerere, hotuba yake ilitawaliwa na vijembe, badala ya kuwaeleza wananchi ni jinsi gani tunatatua matatizo yaliyopo kwa sasa katika taifa letu,” alisema.
“Mimi nilitegemea chairman (mwenyekiti) wangu atawaeleza wananchi na
kuwapoza kuhusu makali ya mgao wa umeme na kuwaeleza pia mikakati
inayochukuliwa na seriakali, ili kutatua kero hiyo, lakini mambo yakaenda kinyume kabisa, hotuba itakaliwa na taarabu, mafumbo yasiyokuwa na tija ndani ya chama chetu,” kilieleza chanzo chetu cha habari.
Mpasha habari huyo alibainisha kuwa, “kwa sasa mchakato mkali unaandaliwa kuhakikisha Bw. Wakasuvi hachaguliwi tena kushika wadhifa wa Mwenyekiti mkoa wa Tabora katika uchaguzi wa viongozi ndani ya CCM ambao unatarajiwa kufanyika mwakani nchi nzima.
“Hapa kuna makundi mawili ukae unajua hilo, kunakundi la Bw. Wakasuvi na lingine la aliyekuwa Mwenyekiti mkoa Mzee Nkumba, sasa wengi wa wanachama wameona ni bora ya Mzee Nkumba yeye hana makundi ndani ya chama kuliko huyu wasasa,” alisema mpasha habari.
Hivi karibuni Bw. Wakasuvi alikaririwa na gazeti hili akiwashambulia hadharani kwa vijembe na mafumbo wanachama wenzake wanaosadikiwa kutoka kundi la aliyekuwa mbunge wa Igunga, Bw. Rostam Aziz akisema walitaka CCM ishindwe Igunga ili waheshimiane.
Categories: