![]() |
Kaimu Mwenyekiti wa POAC, Murtaza Mangungu |
Raymond Kaminyoge na Mohamed Mohamed
KAMATI ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imegoma kupitisha hesabu za Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (Veta), baada ya kubaini matumizi mabaya ya fedha.
Kufuatia hali hiyo, kamati ilisema haitapitisha hesabu hizo hadi mamlaka hiyo itakapokutana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Hazina, ili kupitia upya hesabu hizo.
Kaimu Mwenyekiti wa POAC, Murtaza Mangungu, alisema hayo mbele ya viongozi wa Veta waliofika mbele ya kamati hiyo.Mangungu alisema msimamo wa kamati umetokana baada ya kubaini matumizi makubwa ya fedha, huku kukiwapo changamoto nyingi zinazoikabili mamlaka hiyo.
Pia, kamati imeitaka Veta kuwasilisha kibali cha maombi ya posho ambazo zimekuwa zikilipwa kwa wafanyakazi kutoka Hazina.“Posho mbalimbali zimekuwa zikilipwa na Veta kwa wafanyakazi wake bila kibali kutoka Hazina, hivyo tumewaagiza waombe kibali kwanza kabla ya kulipana posho,” alisema Mangungu.
Pia, kamati hiyo imeiagiza Veta kufanya utaratibu wa wafanyakazi kutumia huduma za bima ya afya badala ya kutumia hospitali binafsi.“ Utaratibu huu utawasaidia wafanyakazi wa Veta nchi nzima kutibiwa na bima ya afya, badala ya hospitali binafsi ambazo hutumia gharama kubwa,” alisema Mangungu.
Vilevile kamati iliagiza bodi ya Veta kuajiri wataalamu wa masuala ya uhasibu kutoka Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi (NBAA) ili kufanya kazi kwa kufuata maadili ya kazi za uhasibu.“Ni lazima tufahamu kuwa Veta ni muhimili wa taifa kutengeneza nguvu kazi, hivyo iwapo itashindwa kufanya kazi vizuri itadidimiza maendeleo,” alisema
Mwenyekiti wa bodi hiyo, Profesa Idrisa Mshoro, alisema bodi yake itahakikisha maagizo ya bodi yanatekelezwa.
Chanzo: MWANANCHI
Categories:
KAMATI ya Hesabu za Mashirika ya Umma