Kikwete ahimiza maadili vyama vya siasa


RAIS Jakaya Kikwete, amewataka viongozi wa vyama vya siasa, wakiwemo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mstari wa mbele wa kusimamia maadili ndani ya vyama vyao kwa kukosoa na kukemea vitendo vya rushwa.

“Sheria hii ya sekretarieti pekee si mwarobaini, bali watumishi wakubali kuzingatia maadili kupitia taasisi za dini, viongozi wa vyama vya siasa na asasi nyingine kuwa kila moja kutimiza wajibu wake,” alisema Rais Kikwete.

Aliyasema hayo kwenye hotuba ya kufunga mafunzo ya upelelezi kwa maofisa 50 wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, yaliyofanyika hivi karibuni Chuo cha Maofisa wa Polisi, Kidatu, mkoani Morogoro.

“Ni siku muhimu na ya kihistoria, tangu kuanzishwa kwa Sekretarieti hii ya Maadili imeweza kuwapatia mafunzo maofisa wake mafunzo ya Upelelezi na Uchunguzi. Huu ni mwanzo mzuri wa kusimamia jukumu hili.

“Ni wajibu kwa viongozi wa vyama vyote vya siasa ikiwemo CCM nao wawajibike kusimamia maadili kwani viongozi wanatoka kwenye vyama vya siasa,” alisisitiza Rais Kikwete.

Alisema ili kujenga viongozi na watumishi wenye kuzingatia maadili mema, Sekretarieti ya Maadili inapaswa kubuni njia nyingine ya kuwapiga msasa watumishi wapya wanaoajiriwa serikalini na kwenye taasisi za umma kwa kuwapatia maadili mema.

Categories: