Mwema: Uhalifu sasa umepungua


MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Said Mwema, amesema kufanyika kwa maboresho ambayo pia yanaendelea ndani ya Jeshi la Polisi pamoja na mpango wa Polisi Shirikishi na Jamii, vimewezesha kwa kiasi kikubwa kupungua kwa vitendo vya uhalifu ukiwemo ujambazi na biashara ya dawa za kulevya nchini.

IGP Mwema alisema hayo, katika hotuba yake fupi mbele ya Rais Jakaya Kikwete, aliyekuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa mafunzo ya upelelezi kwa maofisa 50 wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambayo yalifanyika hivi karibuni katika Chuo cha Maofisa wa Polisi, Kidatu, Mkoani Morogoro.

“Uharifu umepungua ukiwemo ujambazi pamoja na dawa za kulevya …siwezi kusema sana kuhusu ujambazi, lakini vitendo hivyo vimepungua ikiwemo na biashara ya dawa za kulevya,” alisema IGP Mwema.

Hata hivyo aliongeza kusema “mnashuhudia jinsi tunavyopambana na majambazi pamoja na wasafirishaji wa dawa za kulevya …tumekuwa tukiwakamata watu hawa , sambamba na majambazi.

“Mafanikio haya yanatokana na dhana ya Polisi Jamii na Shirikishi inayowashirikisha wananchi kutoa taarifa za viashiria vya uharifu ili kuzuia na kupambana na uharifu nchini,” alisisitiza IGP Mwema.

Hata hivyo alisema, jeshi hilo limeanza kushirikiana na Idara ya Wanyamapori kwa kuwafundisha askari wake mbinu mbalimbali za kupambana na majangili wanaoua wanyama na kutorosha nyara na rasilimali za Taifa .

“Katika kupambana na uhalifu wa ujangili kwenye hifadhi za wanyama pori, Polisi pia inashirikiana na askari wa wanyamapori kuwapatia mbinu za kukabiliana na majangili na
kushiriki kikamilifu katika baadhi ya oparesheni. “Tunashirikiana pia na askari wa Halmashauri za Majiji na Manispaa katika kukabiliana na uharifu kwenye miji,” alisema.

Pamoja na jeshi hilo kujikita kwenye maboresho yaliyoanzishwa ndani ya Jeshi la Polisi ya kubadili utamaduni wa kufanya kazi kwa polisi na maofisa wake, moja ya majukumu yaliyowekewa mkazo ni kusimamia dhana ya kuaminiana baina ya polisi na wananchi.
Chanzo: HabariLeo

Categories: