Imeandikwa na Anna Makange, Tanga
IDARA ya Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, imewataka baadhi ya wafugaji na wananchi kwa ujumla kuacha kusambaza taarifa zisizo sahihi kwamba ugonjwa wa kimeta umeingia na kuua ng’ombe kadhaa.
Ofisa Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Kilindi, Fredrick Kiango alisema hayo kutokana na kuongezeka kwa hofu miongoni mwa wakazi wa maeneo tofauti ya Mkoa wa Tanga zilizotokana
na tetesi kwamba ugonjwa wa kimeta umeingia wilayani Kilindi na kuua ng’ombe zaidi ya 100 hivi karibuni.
Kiango alisema ameshangazwa na taarifa hizo ambazo hata baada ya wataalamu katika idara yake kuzifanyia kazi vijijini, imebaini hazina ukweli wowote isipokuwa ni uvumi ambao hadi sasa hawafahamu lengo lake, na hasa kwa wananchi ambao ndio watumiaji wakubwa wa mazao yatokanayo na ng’ombe.
Alibainisha kwamba hivi karibuni katika baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo ng’ombe 15 waliripotiwa kufa kutokana na ugonjwa wa chambavu na sio kimeta kama baadhi ya watu
wanavyosambaza uvumi na kudai kuwa tayari wametoa chanjo ya kudhibiti.
“Napenda ieleweke kwamba taarifa zinazoenezwa kuhusu kuingia kwa ugonjwa wa kimeta hapa Kilindi sio sahihi. Mwezi uliopita katika baadhi ya vijiji vyetu vinavyopakana na mikoa jirani,
ng’ombe 15 waliripotiwa kufa wakiwa na dalili kama za ugonjwa huo, lakini baada ya madaktari kukagua ile mizoga, walibaini ni ugonjwa wa chambavu ambao kimsingi baadhi
ya dalili zake zinafanana na za kimeta,” alisema.
Kiango alitaja vijiji hivyo kuwa ni Negero, Kimbe, Kilindi pamoja na Pagwi vilivyoko Tarafa ya Kimbe na kuongeza kuwa huenda baadhi ya watu hawakupata taarifa sahihi kuhusu matokeo ya kitaalamu ya uchunguzi wa vifo vya ng’ombe hao na hivyo kuamua kueneza hofu kwa
jamii na watumiaji wa mazao ya ng’ombe.
Aidha, alibainisha hatua zinazoendelea kuchukuliwa na idara yake hivi sasa ni kuendeleza utoaji wa elimu na chanjo kwa mifugo na kuwahimiza wafugaji kutoa taarifa mapema za
ng’ombe wagonjwa, kutogusa mizoga ya mifugo inayokufa kabla ya kumwita daktari ambaye akishabaini tatizo huwapa maelekezo sahihi.
Wakazi wengi wa Wilaya ya Kilindi wanajishughulisha na kilimo na ufugaji na kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana, wilaya ina mifugo ya aina mbalimbali zaidi ya 150,000, ng’ombe
wakiwa 145,000.
CHANZO: HABARI LEO